Kwa siku za hivi karibuni kumekuwa na mjadala mkubwa hasa kwenye mitandao ya kijamii na vituo vya habari kuhusu suala la watoto waliojifungua kurudi shule. Wengi walisikika wakisema sio kila anayepata mimba huwa alitaka au alijamiiana kwa kupenda, kwamba baadhi walibakwa.
Katika hilo, tukaona kwa ufupi tuelezee maana ya kubaka katika sheria ilivyo. Watu wengi hudhani kuwa, ili upatikane na kosa la kubaka, ni lazima utumie nguvu au kujamiiana na mtu pasipo idhini yake. Lakini katika uwanja wa sheria, kubaka ina maana pana zaidi ya hiyo.
Kuna aina mabalimbali ya matendo ukiyafanya hata kama ulijamiiana na mtu kwa idhini yake, lakini mbele ya sheria itafahamika kuwa ulibaka.
Kwa mujibu wa kanuni za adhabu, mtoto wa chini ya umri wa miaka 10, anachukuliwa kama hawezi kufanya kosa lolote, hivyo hawezi kuwajibishwa kwa alichofanya au kuto kufanya. Aidha, mtoto wa miaka chini ya 12 hatochukuliwa kama alitenda kosa, hadi pale itakapothibitishwa wakati wa kutenda au kutokutenda jambo alikuwa akifahamu.
Kwa mujibu wa sheria, mtoto wa chini ya umri wa miaka 12, anachukuliwa kuwa hawezi kujamiiana.
Kisheria, ni kosa kwa mwanaume kumbaka mwanamke. Na itachukuliwa kuwa mwanaume amembaka mwanamke endapo kitendo alichokifanya kitaangukia katika moja ya mambo haya;
- Si mke wake, au ni mke wake lakini wameachana na hivyo akajamiiana naye bila idhini yake.
- Kujamiiana na mwanamke kwa idhini yake, lakini idhini hiyo imepatikana kwa kutumia nguvu au vitisho kwa kumuweka mwanamke katika vitisho vya kumuua au kumjeruhi wakati umemshikilia kinyume na sheria.
- Kujamiiana na mwanamke kwa idhini yake, lakini idhini hiyo imepatikana wakati akiwa hajitambui ama kwa kupewa madawa na mwanaume au mtu mwingine ili tu kuthibitisha kuwa kulikuwa na makubaliano ya awali.
- Kwa idhini ya mwanamke, lakini mwanaume akijua kuwa yeye si mumewe, na idhini hiyo imepatikana kwa mwanamke huyo kuaminishwa kuwa yeye ni mke wa mwanaune huyo kihalali.
- Kwa idhini au bila idhini ya mwanamke wakati akiwa na umri wa chini ya miaka 18, labda wawe wameoana na mwanamke ana umri wa zaidi ya miaka 15 na wakati wa kufanya tendo hilo hawakuwa wameachana.
Aidha, kama ni kiongozi katika taasisi yoyote ama ya serikali au la, ukituma manufaa ya uongozi wako kumbaka mwanamke, utaadhibiwa kwa mujibu wa sheria.
Ili kuthibitisha kuwa mtu amebakwa, kumuingilia mtoto wa kike au mwanamke, hata kama ni kidogo, inatosha kuthibitisha kuwa amebakwa. Lakini ushahidi wa majeraha katika mwili, hautoshi kuthibitisha kuwa mwanamke alibakwa.
No comments:
Post a Comment