Monday, June 5, 2017

MEYA WA DAR ASAFIRI KWA GARI LA ABIRIA KWENDA KUMZIKA NDESAMBURO


NA CHRISTINA MWAGALA, OFISI YA MEYA WA JIJI

MSTAHIKI Meya wa jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita leo ameondoka
jijini hapa kuelekea mkoani Kilimanjaro kwa kutumia usafiri wa basi
kuhudhuria mazishi ya Mbunge wa zamani wa Jimbo la Moshi mjini na
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Mzee Philemon Ndesamburo
aliyefariki dunia wiki iliyopita.
Meya Mwita ameondoka kwa kutumia usafiri wa basi baada ya gari lake
kupata ajali na kuharibika vibaya Jumapili ya wiki iliyopita alipokuwa
akitokea Dodoma kwenye kikao.
Akizungumza mara baada ya kuondoka katika stendi kuu ya mabasi ya
Ubungo, Meya Mwita alisema kuwa msiba wa mzee Ndesamburo ni pigo kwa
Taifa, Chama, wakazi na wananchi wote wa mkoa wa Kilimanjo  kutokana
na ushawishi mkubwa aliokuwanao katika mkoa huo.
Mbali na hivyo alisema kuwa imekuwa nipigo kubwa pia hata ndani ya
Chama kwa kuwa bado alikuwa akihitajika kutokana na busara na hekima
alizokuwa nazo enzi ya uhai wake licha yakuwa alikuwa amestaafu nafasi
ya ubunge kwenye jimbo hilo.
Wakati shughuli za kuaga mwili wa mzee Ndesamburo zikiendelea leo
mjini Moshi katika viwanja vya Majengo , Meya Mwita anatarajiwa kufika
mnamo saa 10 jioni ambapo ataungana na viongozi mbalimbali wa chama
ngazi ya Taifa, Mikoa, wabunge na familia ya mzee Ndesamburo pamoja na
viongozi mbalimbali watakaoshiriki kwenye msiba huo.
Aidha anatarajiwa kurejea jijini hapa Jumatano wiki hii baada ya
kumalizika kwa shuguli za mazishi hapo kesho.
Mzee Ndesamburo alifariki dunia Mei 31 mwaka huu akiwa njiani
kupelekwa hospital ya Rufaa ya KCMC baada ya kupoteza nguvu  mwilini
na atazikwa kijijini kwake Mbokomu kesho.
Mwishoo.

No comments: