Thursday, June 29, 2017

TGNP MTANDAO WATOA SEMINA KWA WANANCHI JUU YA HAKI YA UHURU WA KUJIELEZA.

Mtandao wa Jinsia nchini Tanzania(TGNP) watoa semina kwa wananchi na wanaharakati juu ya kutambua haki yao ya msingi ya uhuru wa kujieleza(Freedom of speech).

Afisa mipango na Mwanasheria toka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Bi. Happines Michael akitoa mawasilisho kwenye semina iliyoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP) Mabibo jijini Dar es salaam

Akitoa mafunzo hayo ndani ya ukumbi wa Mtandao huo, Mabibo jijini Dar es salaam Afisa Program na Mwanasheria toka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Bi. Happines Michael amesema ni muhimu kwa wananchi wote kuitambua haki hii kwa maana ni haki yao kikatiba na inatambulika kimataifa, hivyo wananchi wasiwe na hofu pindi wanapoidai haki yao na wanapotaka kutoa maoni yao ila wasivuke mipaka.

Bi Happines amewambia wananchi na wanaharakati walioudhuria kwenye semina hiyo kuwa kila mwananchi ana haki ya kutafuta kutoa au kupokea taarifa toka katika jamii yake pindi anapohitaji bila kikwazo chochote maana ni haki yake ya msingi kikatiba na inatambulika kimataifa kupitia  mikataba ambayo nchi imeingia, kama vile Tamko la haki za binadamu katika ibara ya 19 na mkataba wa kimataifa wa haki za kisiasa na kiraia katika ibara ya 19.
baadhi ya wageni walioudhuria kwenye semina ilifanyika makao makuu ya Mtandao wa Jinsia nchi Tanzania (TGNP) wakifuatilia semina hiyo kwa makini
"Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 18 haki hii inalindwa kwa raia kupewa uhuru wa kujieleza, kutafuta na kupokea taarifa toka kwa wengine, pamoja na haki ya kusoma Magazeti, kusikiliza Matangazo na kushiriki kwenye mijadala ya Umma au binafsi".alisema Hapiness.
Aidha alizitaja baadhi ya sheria kandamizi ambazo zimewekwa ndani ya nchi na zimekuwa zikinyima uhuru wa wananchi katika kujieleza, kutafuta na kupokea taarifa kuwa ni sheria ya magazeti ya mwaka 1976, Sheria ya usalama wa Taifa ya mwaka 1970, Sheria ya utangazaji ya Tanzania ya Mwaka 1993, na hata sheria za hivi karibuni kama ya makosa ya mtandaoni ya mwaka 2015 bado zinawanyima raia wakiwemo wasanii, Wanahabari na hata wanasiasa uhuru wa kujieleza na kupokokea taarifa toka kwenye vyombo mbali mbali ikiwemo intanet.
Baadhi ya wageni na wanaharakati wakifuatilia semina iliyofanyika mapema jana jijini Dar ers salaam
"Kwa sasa nahisi mmeona kuna baadhi ya waandishi wanashindwa kutoa baadhi ya taarifa kuhofia maisha yao, wasanii nao wanashindwa kutunga baadhi ya nyimbo zenye kukosoa kwa kuhofia kukamatwa yote kutokana na sheria hizi kandamizi.".alisema Afisa.

Hata hivyo aliwataka Wananchi/Wanaharakati kupaza sauti zao pindi wanapoona uhuru huu unakosekana katika jamii kwani Kituo cha Sharia na Haki za Binadamu kimekuwa kikichukua hatua mbali mbali zikiwemo kufungua kesi dhidi ya taasisi au shirika ambalo linakandamiza  haki hiyo na kuitaka serikali ibadilishe au kurekebisha sharia hizo maana zinakwenda kinyume Demokrasia.

                             

                             

No comments: