Tuesday, July 4, 2017

NYOTA WA SIMBA JOHN BOCCO AITWA KUIONGEZEA NGUVU STARS

MCHEZAJI JOHN RAPHAEL BOCCO

Wakati kesho Jumatano Julai 5, 2017 timu yetu ya Tanzania ya mpira wa miguu - Taifa Stars ikicheza na Zambia katika Nusu Fainali ya kuwania Kombe la Castle COSAFA, Kocha Mkuu Salum Shaban Mayanga amemuongeza kwenye kikosi Mshambuliaji John Raphael Bocco.

Bocco kwa sasa yuko Afrika Kusini pamoja na timu hiyo akichukua nafasi ya Mshambuliaji Mbaraka Yussuf Abeid aliyejepata majeruhi kwenye michuano hiyo iliyoanza Juni 25, mwaka huu ambako Tanzania ilikuwa Kundi ‘A’ pamoja na timu za Malawi, Mauritius na Angola.

Tanzania iliibuka kinara katika kundi hilo na kucheza Robo Fainali ambako ilicheza na Afrika Kusini na kuitoa katika hatua hiyo hivyo kwa mujibu wa ratiba, kesho Jumatano Julai 5, mwaka itashindana na Zambia.

Kocha Salum Mayanga amefafanua kuwa mbali ya Bocco kujaza nafasi hiyo, amemwongeza kwenye kikosi ili kuongeza nguvu ya kupambana na Rwanda katika mchezo wa kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani - CHAN.

Mchezo dhidi ya Rwanda utafanyika Julai 15, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza. Mchezo wa marudiano utafanyika baadaye mwezi huu au mapema mwezi ujao na mshindi wa jumla atacheza na Uganda. Mshindi wa jumla kati ya Tanzania na Uganda ndiye atakayefuzu kwa fainali za CHAN zitakazofanyika Kenya, mwaka 2018.
………………………………………………………………………………………….
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA

No comments: