Monday, July 24, 2017

SERIKALI YA TANZANIA NA KENYA ZIMEAFIKINA KUONDOA VIKWAZO VYA KIBIASHARA KWENYE NCHI ZAO

SERIKALI za Tanzania na Kenya zimekubaliana kuondoa vikwazo vya kibiashara zilizokuwa zimewekeana kuhusu bidhaa kutoingizwa katika nchi hizo.
Waziri wa Mambo ya Nje, na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga akiongea na waandishi wa habari mapema leo jijini Dar es salaam
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam,  Waziri wa Mambo ya Nje, na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga ameeleza kuwa kuondolewa kwa vikwazo hivyo ni kuzingatia taratibu za kibiashara ambazo zilikubaliwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Akifafanua, Dkt. Mahiga alisema hatua hiyo itaifanya Kenya kuondoa vikwazo kwa bidhaa za unga wa ngano na gesi ya kupikia (LPG) ilivyoviweka dhidi ya Tanzania, na Tanzania kuondoa vikwazo kwa bidhaa za maziwa na sigara zinazozalishwa nchini Kenya.
Baadhi ya waandishi wa habari walioudhuria mkutano huo uliofanyika ukumbi wa Mwalimu JK. Nyerere uliopo Posta jijini Dar es salaam
“Juhudi za awali za serikali ya Tanzania ilikuwa ni kuona vikwazo hivyo vinaondolewa na Kenya kwa wakati lakini  hazikuzaa matunda. Hali hiyo ilisababisha Tanzania nayo kuweka vikwazo kwa bidhaa za maziwa na sigara kutoka Kenya zisiingie katika soko la Tanzania,” alisema Mahiga.

Alisisitiza kwamba kwa kuzingatia mahusiano mazuri ya kindugu yaliyopo kati ya nchi hizi mbili na kwa kujali manufaa mapana ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, viongozi wakuu wa nchi hizi mbili Dkt. John  Magufuli na Uhuru Kenyatta wa Kenya walikubaliana kuviondoa vikwazo hivyo mara moja.

Hatua hiyo ya kuondoa vikwazo hivyo ilifuatia maelekezo waliyotoa viongozi hao kwa mawaziri wao wa mambo ya nje, Dkt. Augustine Mahiga na Dkt. Amina Mohammed wa Kenya.

No comments: