Saturday, September 16, 2017

HOJA YA MBUNGE NKAMIA YA KUTAKA RAIS MAGUFULI AONGEZE MIAKA 7,LAWAIBUA JUKWAA LA KATIBA,SOMA HAPO KUJUA

SIKU chache  baada ya Mbunge wa Kondoa, Juma Nkamia kusema anadhamiria kupeleka hoja binafsi Bungeni ya kutaka kipindi cha Rais kukaa madarakani kuongezwa toka miaka mitano ilivyo  sasa hadi miaka 7 kama ilivyo nchi ya Rwanda,
Hoja yake hiyo imeanza kupingwa na asasi mbali mbali, baada ya Jukwaa la Katiba nchini (JUKATA)  kupinga kauli hiyo na kumtaka Rais John Magufuli kuendeleza mchakato  wa katiba ambao utaweza kuondoa hoja za mbunge Mkamia. 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Mkurugenzi Mtendaji wa JUKATA Hebron Mwakagenda, alisema kutokana na kutotengwa kwa fedha yoyote kwenye bajeti ya Serikali kwa ajili ya mchakato huo ni kwamba matumaini ya Watanzania walio wengi yalikuwa kwamba mchakato wa Katiba Mpya ungeweza kukamilishwa katika kipindi cha kwanza cha Serikali ya Rais Magufuli lakini sasa yameanza kufifia.

"Kwa mazingira yaliyopo, kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, kumebaki fursa finyu sana kuandaa bajeti ya dharura kuipitisha katika kipindi hiki cha cha mwaka 2017. Huko tuendako, maandaliz ya uchaguzi wa serikali za mitaa yanatakiwa yawe yameanza rasmi muda mfupi kuanzia sasa na uchaguzi unatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka 2019," alisema Mwakagenda.

Aidha alisema uchaguzi mkuu ujao utakao fanyika Oktoba 2020 unapaswa kuwa umeanzishwa maandalizi yake kuanzia Januari  mwakani ikiwa ni pamoja na uandikishaji na uhakiki wa wapiga kura.

Jukwaa hilo limesema kama ikitokea hakuna uwezekano wa kukamilisha mchakato huo kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kama ambavyo dalili zinazidi kuonyesha,  kunahitajika marekebisho sita (6) ya msingi katika Katiba ya sasa ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania (1977)  na ya Zanzibar (1984) pamoja na vifungu vya sheria zote zinazohusu uchaguzi ili kushughulikia kasoro zote zinazolalamikiwa katika uchaguzi. 

Akitaja marekebisho hayo, Mwakagenda alisema ni kuwepo kwa Uhuru Kamili wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Free and Independent Electoral Commission), Fursa ya mgombea huru katika Uchaguzi wa Tanzania (Independent Candidate), uwezekano wa kuhoji matokeo ya uchaguzi wa Rais mahakamani. 
Mengine ni kuwezesha vyama vya siasa kuungana kikatiba na kisheria kwa lengo la kusimamisha mgombea mmoja katika uchaguzi, kurejesha mfumo wa ushindi katika uchaguzi wa Rais kwa kigezo cha kupatikana kwa kura zisizopungua asilimia 50 (50% +1) ili kuhakikisha kuwa mgombea Urais anayeshinda anakuwa na ridhaa ya Watanzania waliowengi (Absolute Majority). 

Na kuingiza katika Katiba na kwenye sheria za uchaguzi uwakilishi sawia kati ya wanawake na wanaume katika vyombo vya maamuzi kama vile mabaraza ya Madiwani, Bunge na Baraza la Wawakilishi ili kuakisi dhana na nia iliyomo katika mikataba ya kimataifa iliyoridhiwa na serikali ya asilimia 50 kwa 50.

No comments: