Friday, September 29, 2017

SHEIKH JALALA NA ASKOFU BANZA WAMEZINDUA MPANGO WA KUGAWA MAJI NA VIPEPERUSHI BURE

Leo ikiwa ni siku ya tarehe 29 ya mwezi wa 9 sheikh mkuu wa dhehebu la khoja shia Tanzania Hemed Jalala amezindua program ya ugawaji maji na vipeperushi bure iliyofanyika katika msikiti wa kigogo jijini Dar es salaam.
Akiongea na waandishi wa habari mapema leo msikitini hapo Sheikh Jalala amesema kuwa zoezi hili la kugawa maji linaendana sambamba na kumuenzi Imam Hussein ambaye ni mjukuu wa pili wa Mtukufu Mtume Mohamad ambaye alifariki kwa kuwatetea wanadamu bila kuangalia itikadi zao za kidini, kikabila wala maumbile.

Sheikh Jalala aliongezea kwa kusema kuwa imam hussein amekuwa ni alama kwa dunia kwa kukubali yeye kufa ili watu wapate amani pamoja na kutendeana mema ikiwemo kupendana, kuhurumiana kuheshimiana na alithubutu kuyafanya hayo wakati huo ambao mema yalipungua katika dunia na hakukuwepo amani miongoni mwa wanadamu hao na matokeo yake yalikuwa ni ugomvi na chuki ndani ya kizani hicho.
Maulana Sheikh Hemed Jalala akiongea na waandishi wa habari ambao hawapo pichani mara baada ya kuzindua programu ya kugawa maji na vipeperushi bure mapema leo jijini Dar es salaam
Lakini leo hii Imam Hussein anatufundisha watanzania kuwa ni watu wenye huruma, upendo ushirikiano na amani tuliyopewa kama nuru yetu Watanzania, ndiyo maana msikiti huu umeamua kuanzisha program kama hizi ikiwemo kuwatembelea wagonjwa, kujitolea damu kwa hiari, kwenda kuwapa moyo wafungwa pamoja na kuwaona na kuwapa misaada watoto yatima ikiwa ni miongoni mwa njia za kumuenzi Imam huyo aliyejitoa kwa ajiri ya wanadamu.
Askofu Mkuu wa kanisa la Tanzania Outreach Ministries Banza Suleiman akitoa ufafanuzi wa jambo fulani katika uzinduzi wa kugawa maji na vipeperushi bure zoezi lililofanyika mapema leo Masjid Al Ghadiir Kigogo Dar es salaam.
Akiongezea Askofu Mkuu wa kanisa la Tanzania Outreach Ministries Banza Suleiman amesema kuwa kitendo kilichofanywa na msikiti huo ni chema na kinapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania anaependa maendeleo kwani maisha yetu wanadamu yanategemea maji kwa kiasi kikubwa, hivyo ili kumuunga mkono Rais Magufuli kufikia kuwa na uchumi mzuri wa viwanda ni lazima watu wawe na maji ya kutosha ili waweze kufanya kazi ipasavyo.

Askofu huyo aliendelea kwa kusema kuwa mungu anambariki anaetoa hivyo kwa kujitolea huko mungu atawabariki sana na hata serikali itafurahi kwa kuona hata tasisi za kidini zipo kwa dhumuni la kuwajari wananchi wake kwa kuona kitendo kilichofanywa na msikiti huo, lakini pia hata wananchi wataona ni jambo zuri kwani maisha ya mwana damu yanategemea maji hivyo bila maji hakuna maisha.
Mwenyekiti wa Kata ya Kigogo Mbuyuni Bw. Hassan Nguogani akiongea na waandishi wa habari ambao hawapo pichani mapema leo jijini Dar es salaam.
Na mwisho Mwenyekiti wa Mtaa Kigogo Mbuyuni Bw. Hassan Nguogani alimalizia kwa kusema wanaishukuru sana taasisi hiyo ya Shia kwani imechangia maendeleo ya kata hiyo kwa kiasi kikubwa kwani hujitolea mambo mengi sana kama matibabu bure kwa wagonjwa, husaidia watoto yatima katika kata hiyo ujitolea madaftari na vifaa mbalimbali vya shule kwa wanafunzi na huduma nyingine nyingi.

Lakini pia husaidia juhudi za kimaendeleo kama kupanda miti, kufanya usafi maeneo ya kata hiyo na hata kuchangia ujenzi wa vitu mbalimbali katika kata hiyo, hivyo ufanya majukumu mengi ambayo ni ya serikali lakini hujitolea wao na hivyo wakazi wa kigogo hunufaika na nifahari sana kwa uwepo wa msikiti huo mahali hapo.

 

No comments: