TGNP Mtandao
kwa kushirikiana na Taasisi ya Mafunzo ya Jinsia GTI na AWDF wameandaa mafunzo
ya siku tatu kwa wafanya biashara wanawake wa mipakani lengo likiwa ni
kuwajengea uwezo wanawake hawa wa kuingiza maswala ya jinsia katika biashara
zao.
Mafunzo hayo
yamewaleta pamoja zaidi ya washiriki 35 wakiwemo Maafisa wa serikali kutoka
mipaka tofauti tofauti, Asasi za kiraia ili kuwajengea uwezo wa kuzifahamu haki
zao na kukabiliana na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo wafanya biashara
wanawake wa mipakani katika biashara zao.
Akiongea na
waandishi wa habari mapema leo Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtadao Bi. Lilian
Liundi alisema kuwa wameamua kuwapa wafanyabiashara wa mipakani elimu hiyo ili
waweze kufahamu kanuni mbalimbali za Afrika Mashariki na namna ya kuboresha
huduma zao ili kuweza kuyafikia masoko kwa urahisi kuanzia ngazi ya kikanda na
kufikia kimataifa.
Aliongezea
kwa kusema kuwa utafiti uliofanywa na Kituo cha Sera za Biashara Afrika
unaonyesha kuwa biashara imatoa ajira
kwa zaidi ya asilimia 60 ya wanawake, na katika biashara zifanyikazo katika
nchi za jangwa la Sahara, ambapo asilimia kati ya 70 na 80 ya wanawake
wamejikita zaidi katika biashara isiyo rasmi na utafiti wa UN Woman unaonyesha
zaidi ya asilimia 74 ya wafanyabiashara za mipakani katika nchi za maziwa makuu
ni wanawake.
Mkurugenzi
huyo aliendelea kwa kusema kuwa wanawake wanaofanya biashara mipakani
wanakumbana na changamoto nyingi ikiwemo usawa katika mgawanyo wa kipato na
maamuzi juu ya rasilimali katika kufikia zana za uzalishaji kama vile mitaji,
ardhi na teknolojia sahihi na taarifa pamoja na elimu ya mafunzo, vilevile
ukatili wa kijinsia ikiwemo rushwa ya ngono na nyingine nyingi.
Lakini pia
pamoja na nchi zetu kuridhia mikataba mbalimbali ya kitaifa, kimataifa na ya kikanda
ya kuendeleza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake kama mkataba wa Umoja wa
kimataifa wa mwaka 1979, mpango mkakati wa Beijing wa mwaka 1995, Itifaki ya Maputo
ya mwaka 1997 na mkataba wa jinsia na maendeleo wa ukanda wa SADC 1998.
Aidha bi. Lilian
liundi alisema licha ya juhudi hizo zote lakini bado hakuna muungano kati ya biashara
na sera za jinsia kwani mikataba muhimu ya biashara bado inaupofu mkubwa wa
kijinsia, kwa kiasi cha kushindwa kuzingatia mahitaji muhimu ya wanawake,
lakini pia utekelezaji hafifu wa mikataba na kutokuwepo kwa taarifa mbalimbali
za fursa za biashara hii imewaongezea vikwazo wanawake wanaofanya biashara
isiyo rasmi katika mipaka na kwa wajasiliamali wadogo kwa ujumla kuweza kukuza
biashara zao.
Lakini pia
serikali za nchi za afrika mashariki zilitakiwa kukaa chini na kuunda sera na
mipango itakayowasaidia wafanyabiashara hawa wadogo wa mipakani kwa kuwaondolea
kodi kandamizi ili na wao waje kuwa wafanyabiashara wakubwa kwa kuwawekea
mikakati madubuti, kwani wafanya biashara hawa wakiwezeshwa wanaweza kuwa
wakubwa na kuchangia vizuri pato la taifa.
Na mwisho
alimalizia kwa kusema kuwa changamoto hizi zinahitaji sera kufanyiwa maboresho
ili kuunga mkono juhudi za wanawake na kuwapa ujasiri wanawake wa
kuimarisha biashara zao, lakini pia
maboresho hayo yanatakiwa kulenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika biashara
za mipakani kwa kuboresha na kurahisisha mchakato wa kufanya biashara mipakani.
Inatambulika kuwa wanawake hurudisha asilimia kubwa ya pato lao kwa familia na
jamii zao, hivyo juhudi za makusudi zinahitajika katika kuwainua kiuchumi wanawake
hawa na kwa nchi kama za afrika mashariki zinahitajika kuhakikisha kuwa
wanawake wanapata haki na fursa sawa kama wanaume ili kupunguza pengo la
kijinsia, wanawake wanatakiwa kutoa michango yao katika maendeleo ya jamii zao.
No comments:
Post a Comment