Thursday, November 30, 2017

SARAKASI ZA UCHAGUZI MDOGO ZAWASHANGAZA LHRC,WAIBUKA NA HILI HAPA

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeibuka na kusema wamebaini uvunjifu mkubwa wa haki za Binadamu  katika uchaguzi huo ambapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeshinda kata 42 huku Chadema ikiambulia ushindi wa kata moja.
Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Bi. Anna Henga akiongea na waandishi wahabari mapema leo kuhusu uchaguzi mdogo wa madiwani ulifanyika hivi karibuni.
Pia Kituo hicho kimeitahadharishwa serikali kuwa kama isipokemea vitendo hivyo vya uvunjifu wa Haki za Binadamu ,kutasababisha athari  mbaya kwenye uchaguzi wa serikali za Mitaa utakaofanyika 2019 pamoja na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Akizungumza na Waandishi Habari leo Jijini Dar es Salaam,Kaimu Mkurugenzi wa (LHRC),Anna Henga wakati wakitoa tathmini ya Uchaguzi huo, amesema kituo hicho kimefuatilia kwa ukaribu uchaguzi mdogo wa marudio wa kuchagua madiwani katika kata 43  zilizopo  halmashauri  takribani 36 kwenye mikao 19 nchini na kubaini uchaguzi ulikuwa na kasoro lukuki zilizochangia uvunjifu wa haki za binadamu.

Amesema  pamoja na ukweli kwamba baadhi ya kata uchaguzi ulifanyika kwa uhuru na haki lakini bado kituo hicho wamebaini pia uchaguzi huo kutawaliwa matukio ya watu kutekwa na watu wasiojulikana ,watu kupigwa ,kukamatwa na kujeruhiwa kwa lengo la kuharibu na kuvuruga  uchaguzi na kuwatia hofu wapiga kura.

"Vitendo hivi  vimefanywa  na Vyombo vya Dola,watu wasiojulikana na watu wanaosadikika kuwa wafuasi wa vyama siasa ikiwemo CCM na CHADEMA na vyama vingine vya Upinzani "Amesema Bi Henga.

 Bi Henga ameyataja matukio hayo ni tukio la kukamatwa na kutekwa kwa watu  katika kata ya Kitwiru  ,Iringa Mjini , kuliko fanywa na vijana wana ulinzi wa CCM maarufu kwa jina la Green Gurd.

"Yapo matukio ya ikiwemo kwenye Kata ya Makiba wakala wa Chadema ,Rashid Jumanne na Mwenyekiti wa Chadema  Tawi la Valeska,Nickson Mbise walijeruhiwa vibaya baada ya kushambuliwa  kwa mapanga  mapema asubuhi  walipokuwa wakielekea katika vituo vya kupiga kura"
Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Bi. Anna Henga akionyesha picha za baadhi ya matukio yaliyotokea wakati wa uchaguzi  mdogo wa Madiwani uliofanyika hivi karibuni baadhi ya maeneo hapa nchini.
"Lhrc tumebaini pia kuna matukio yameripotiwa kuhusu viongozi wa vyama vya viasa na Mawakala wa Vyama Kukamatwa mathalani katibu wa Chadema wilaya ya Ubungo ambaye alikuwa mratibu Mkuu wa Uchaguzi wa kata ya Saranga ,Perfeck Mwasiwelwa ambaye alikamatwa na Jeshi Polisi,"

Bi Henga ameendelea kuyataja matukio hayo ni tukio la kukamatwa kwa Meya wa Ubungo na Mwenyekiti  wa Chadema Wilaya ya Ubungo .Boniface Jacob ambaye alikamatwa siku ya uchaguzi ambaye alikuwa ndiye atakayeapishwa kuwa Wakala Mkuu kwenye majumuisho ya kura za Mwisho katika kata.

ARUSHA.
Bi Henga amesema kituo hicho kimebaini rafu katika kata 6 za Jimbo la Arumeru Mashariki ,kata ya Ngobobo,Makiba,Luguruki,Ambureni,Mroroni na Musa ambapo sehemu hizi mawakala wote wa Uchaguzi walitolewa nje ya Vituo vya Kupiga kura wakati zoezi la kupiga kura likiendelea.

Amesema kitendo cha Mawakala wa Vyama vya Siasa kutolewa nje  siku ya Uchaguzi mazingira haya ni viashiria  vya kufanya uchaguzi usio na huru na haki kwani wagombea walikosa haki yao kisheria ya kuwakilisha kuwakilishwa na Mawakala.

Pamoja na hayo,Bi Henga amesema  Kituo Cha Sheria  kinaona matendo hayo sio mazuri ,na yana viashiria vyote vya kukandamiza Demokrasia nchini .

"Kuna hatari ya kukuza utamaduni wa kulipana Visasi kwa Chuki za Kisiasa ambacho kitapelekea uvunjifu wa Amani "Amesema Bi Henga ambaye pia ni Wakili  Msomi.
Baadhi ya waandishi wa habari walioudhuria mkutano huo, wakifuatilia kwa umakini tamko linalotolewa na kituo cha Sheria na Haki za Binadamu mapema leo jijini Dar es salaam
Bi Henga ametoa wito kwa Serikali pamoja na vyombo vya Dola kufanya uchanguzi  wa kina na kuchukua hatua kali za kisheria kwa watakao bainika kuhusika kwa namna moja katika uvunifu wa haki za binadamu na uvurugaji wa Uchaguzi.

"Matukio haya yasipokemewa na Jamii nzima ni kiashiria kibaya na msingi mbaya utakao athiri chaguzi zijazo .Hii itapelekea kutishwa kwa wapiga kura wasijitokeze kutekeleza haki zao za kimsingi za kuchagua viongozi wao,kuchochea uhasama miongoni mwa wananchi na wadau wengine wa uchaguzi pamoja na kufifisha Imani ya wananchi juu vya Vyombo vya Usimamizi wa Uchaguzi na Dola kwa ujumla"Amesema Henga

No comments: