Monday, November 13, 2017

WAGOMBEA UDIWANI WAPEWA SHERIA KALI NA NEC KATIKA KIPINDI HIKI CHA UCHAGUZI, IKIWEMO MASHARTI YA KUPIGA KAMPENI.


TUME ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) imesema itawachukulia hatua za kisheria wote watakaokiuka sheria na kanuni za uchaguzi mdogo wa marudio wa udiwani unaotarajia kufanyika Novemba 26, 2017 nchini.
Msimamo huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC, Ramadhani Kailima alipokuwa kwenye mkutano na wadau wa vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi huo. Kata 43 zinagombewa.

“Katika kampeni sheria zingine zipo na zinaendelea kama kawaida, usidhani unaweza fanya jambo halafu mamlaka isiweze kukuadhibu kwasababu tume imeruhusu mikutano ya kampeni  ukifanya kosa sheria zingine zitachukua mkondo wake kama zilivyo,”amesema.

Amesema wagombea wanapaswa kufanya mikutano ndani ya Kata zao na si nje ya kata katika Jimbo husika huku akiwataka kufanya kampeni hizo kwa kufuata maadili.

Amesema endapo wakati wa kampeni hizo kutakuwa na uvunjifu wa kanuni na maadili kama kuchana bendera za chama, mabango au mtu kuingilia mkutano usiomhusu wawasilishe malalamiko yao kwenye kamati husika ngazi ya Kata.
Kailima ameongeza kuwa miongoni mwa adhabu za uvunjifu wa kanuni na maadili ya uchaguzi ni chama husika kuomba radhi, kupewa onyo, chama kupewa karipio, kusimamishwa kufanya kampeni za uchaguzi au faini.

“Tume imeruhusu mikutano ya Kampeni na si ya vyama vya siasa kwasababu madhumuni ni kumhamasisha mtu kuchagua mgombea wa chama husika,”amesema.  

Amesema hadi sasa tayari karatasi 5000 zimeshasambazwa katika Kata hizo kwa lengo la kutumia kunadia na kurekebisha kasoro.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage amewasihi wagombea kufanya kampeni kwa kuzingatia maadili na pnapotokea ukiukwaji au uvunjifu wa maadili, chama au mgombea awasilishe malalamiko kwenye Kamati husika kwa mujibu wa taratibu zilizoainishwa kwenye maadili ya uchaguzi.
“Tume imejiandaa vyema kuhakikisha kuwa shughuli zote za uchaguzi mdogo wa madiwani zinzfanyika vizuri kwa kuzingatia muda uliopangwa ikiwa ni pamoja na kufikisha vifaa vya uchaguzi katika maeneo husika kwa wakati,”amesema.


No comments: