Wednesday, November 1, 2017

WANA GDSS KUWEKA MIPANGO HII KUELEKEA MAADHIMISHO YA SIKU YA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA

Kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia nchini wanaharakati wa GDSS wametakiwa kufanya vitu vitakavyoleta ukombozi katika maeneo wanayoishi. 
Hayo yamesemwa mapema leo na muwezeshaji wa semina hiyo Msafiri Shababi ambae pia ni zao la TGNP Mtandao alipokuwa akiongoza semina hiyo ya nini watakifanya wakiwa kama wanaharakati siku ya maadhimisho hayo.

Maadhimisho hayo yanayotarajiwa kufanyika siku ya jumaa mosi ya tarehe 25 mwezi wa 11 viwanja vya Leaders Club jijini Dar es salaam, na Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan.
Lakini pia maadhimisho hayo kwa mwaka huu yamekuwa na kauli mbiu inayosema kuwa “Funguka ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto haujawahi kumuacha mtu salama”

Katika semina hiyo wanaharakati wamejaribu kukumbushana dhana ya ukatili wa kijinsia pamoja na aina za ukatili ambazo anafanyiwa mwanamke au mtoto na mtu wake wa karibu kama Mzazi, Mlezi, Mume lakini pia na jamii anayoishi nayo.
Aidha wanaharakati hao wameweza kuweka mikakati na mipango mbalimbali ya kuweza kufanya katika kata zao na kuwasilisha mrejesho jumaa tano moja ya mwisho kabla ya siku ya kilele cha maadhimisho hayo ya kupinga ukatili wa kijinsia.

Na miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kutengeneza adithi nzuri za kusisimua na zenye mafunzo kwa kuziweka katika njia ya maandishi lakini pia katika makala fupi za video, na kuzisambaza katika mitandao mbalimbali ya kijamii, ili ujumbe huo uweze kuwafikia watu wengi zaidi na waweze kupata elimu kupitia hadithi hizo.
Lakini pia kwa wale  watakaokuwa na hadithi nzuri zitakazo sisimua watu na kuwa na mafunzo mazuri zaidi watapata fursa ya kuwekewa simulizi zao katika tovuti ya TGNP Mtandao au katika jarida la Ulingo linalotolewa kila mwaka na Mtandao huo na watakuwa wameingia katika historia na hadithi zao zitahifadhiwa huko kama kumbukumbu.



No comments: