Wednesday, January 10, 2018

SERENGETI LITE KUWA MDHAMINI RASMI WA LIGI YA WANAWAKE TANZANIA

Kampuni ya bia ya Serengeti (SBL), leo imetangaza kuwa mdhamini rasmi wa Ligi ya Taifa ya Soka la Wanawake (Women Premier League). Katika Mkataba uliosainiwa kati ya SBL na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), SBL itatoa jumla ya shilingi milioni mia nne  na hamsini (TZS 450m) ili kuzidhamini timu zote zinazoshiriki katika ligi hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.   
Mkurugenzi Mtendaji wa Serengeti Bi. Helene Weesie akitoa ufafanuzi wa jambo fulani mbele ya waandishi wa habari mapema leo Serena hotel jijini Dar es salaam.
Kama mdhamini rasmi wa ligi hiyo, Serengeti Premium Lite itatoa msukumo kwa timu zote nane za wanawake kwenye ligi ambapo mshindi atakuwa mwakilishi wa taifa katika mashindano ya kikanda na ya kimataifa.  Kupitia udhamini huo, SBL ina matumaini makubwa kwamba itaweza kuwazindua wananchi na hasa mashabiki wa soka na kuwaunganisha pamoja ili kuongeza hamasa katika ligi ya taifa ya wanawake kupitia bia hiyo kipenzi cha watanzania ya Serengeti Premium Lite.  

 “Tunayo furaha kubwa kuwa wadhamini rasmi wa Ligi ya Taifa ya Soka la Wanawake kupitia bia yetu maarufu ya Serengeti Lite. Siku zote tumekuwa tukiamini katika kuendeleza vipaji katika sehemu mbali mbali za nchi na haswa inapokuja katika michezo inayotuleta pamoja. Tunaamini udhamini wetu utawavutia mashabiki wa rika mbali mbali kuiunga mkono ligi ya wanawake na kufikia mafanikio makubwa,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa SBL Helene Weesie.
Makamu wa  Rais wa TFF Bw. Michael Wambura akiongea kwa niaba ya TFF na kuelezea walivyofurahishwa na walivyoupokea udhamini huo uliotolewa na kampuni ya bia ya Serengeti mapema leo jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa, SBL inaamini katika nguvu ya mpiga wa miguu ambayo inawaunganisha watu.

Udhamini wa Twiga Stars unafuatia historia ndefu ya udhamini wa timu ya soko ya wanaume, Taifa Stars ambayo mpaka hivi sasa inaendelea kupata udhamini wa SBL kupitia bia yake mama ya Serengeti Premium Lager. SBL ni sehemu ya kampuni ya Diageo ambayo inauhusiano mkubwa na masuala ya soka duniani ikiwa ni pamoja na udhamini wa Ligi Kuu ya Uingereza kupitia bia ya Guinness
Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya bia ya Serengeti(SBL) akifanya makabidhiano na Makamu wa  Rais wa TFF Michael Wambura baada ya kusaini mkataba wa kuwa Seregeti mdhamini mkuu wa ligi ya wanawake.
Kwa upande wake Makamu wa  Rais wa TFF Michael Wambura Amesema Leo kwa mara nyingine tunashuhudia ushikiano muhimu kati yetu na SBL, kampuni maarufu ya bia na ambayo imekuwa mstari wa mbele kwa kusaidia maendeleo ya michezo nchini. Ushirikiano huu utasaidia sana katika kuendeleza soka letu la wanawake pamoja na mashindano tutakayokuwa tunaandaa. Tunafurahia udhamini huu kupitia bia ya Serengeti Lite na tunaamini utakuwa wa mafanikio makubwa,”

Utiaji saini kati ya pande hizo mbili ulishuhudiwa na Mkurugenzi wa Michezo katika Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, Bw, Yusuph Singo ambaye aliipongeza SBL kwa kujitolea kwake katika kuunga mkono sekta ya michezo nchini na pia kuwataka Watanzania wenye mapenzi mema pamoja na makampuni mengine kuiga mfano mzuri wa kampuni ya SBL.

No comments: