Wednesday, January 10, 2018

SERENGETI WASHUSHA NEEMA LIGI YA WANAWAKE NCHINI

,Makamu wa Rais wa TFF Bwana Michael Wambura,Pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Serengeti SBL,Bi Helene Weesie wakibadilishana mikataba mara baada ya shughuli ya kusaini kumalizika leo Jijini Dar es salaam,
Kampuni ya Bia nchini Tanzania ya Serengeti Kupitia Kinywaji cha Serengeti Lite wamekuwa kampuni ya kwanza kudhamini ligi kuu ya soka la wanawake nchini Tanzania ukiwa ni udhamini utakaozinufaisha Timu zote zitakazokuwa zinashiriki ligi hiyo ya soka la wanawake nchini.

Udhamini wa Serengeti kwa ajili ya Ligi hiyo umegharimu kiasi cha Shilingi za Kitanzania million mia nne na Hamsini ikiwa ni udhamini utakaozinufaisha Timu zote za ligi hiyo ambapo udhamini huo utadumu kwa muda wa miaka mitatu mfululizo.
Akizungumza wakati wa kutiliana saini kati ya Uongozi wa Kampuni hiyo ya Bia na Shirikisho la soka Tanzania,Makamu wa Rais wa TFF Bwana Michael Wambura amesema kuwa Udhamini huo umekuja kipindi muhimu ambacho Shirikisho hilo linajipanga kuhakikisha kuwa soka la wanawake linakuwa na hadhi nchini Tanzania ambapo amesema kusainiwa kwa mkataba huo ni moja ya chachu itakayoinua soka la wanawake nchini.

Wambura amesema pamoja na kuwa soka la wanawake nchini Tanzania linakuwa tena kwa kasi lakini bado inahitajika nguvu ya ziada kuhakikisha kuwa watanzania wanakuwa na hamasa ya soka hilo ambapo amesema kuwa ujio wa Serengeti katika soka hilo itakuwa njia moja wapo ya kuliinua soka la wanawake nchini Tanzania,huku akiwataka wale wote wanaohusika na soka la wanawake nchini kuchukulia udhamini huo kama dira mpya ya kutambua ni wapi soka la wanawake linapotakiwa kuelekea kwa sasa.
Akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Serengeti SBL,Bi Helene Weesie amesema kuwa pamoja na udhamini huo wa million mia nne na hamsini ambao utagawanywa kwa timu zote za ligi kuu hiyo kwa miaka mitatu lakini pia Serengeti itaendelea kufanya jitihada za kipekee katika kuitangaza ligi hiyo na kuitambulisha Zaidi kwa watanzania ili kuikuza na kuifanya iwe miongoni mwa ligi pendwa nchini Tanzania.


Ameongeza kuwa mpira wa miguu  sio tu burudani miongoni mwa wahusika lakini pia ni moja ya njia za kuwaunganisha wanadamu pamoja na kuwaongezea kupato hivyo Serengeti inajiskia furaha kuwa moja ya kampuni itakayofanikisha hilo kupitia udhamini wake katika ligi ya wanawake nchini Tanzania.

No comments: