Saturday, February 24, 2018

SOMA HAPA KUJUA MADHUMUNI MAKUU YA ZIARA YA ACT WAZALENDO

Tokeo la picha la act wazalendo
Chama cha ACT Wazalendo kimefanya ziara yake yenye lengo la kutembelea kata ambazo zilichagua madiwani wa ACT Wazalendo katika uchaguzi wa mwaka 2015, ziara hiyo iliyoanza toka february 19, 2018 ikiongozwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho.

Viongozi waliopo kwenye msafara huo ni wajumbe wa Kamati Kuu, ndugu Emmanuel Lazarius Mvula, Mwenyekiti wa Kamati ya Sera na Utafiti, Mama AnnaMaryStela Mallack, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge na Serikali za Mitaa, ndugu Janeth Rithe, Katibu wa Kamati ya Bunge na Serikali na za Mitaa, pamoja na Rachel Kimambo, Afisa Utawala wa Makao Makuu ya chama. 

Madhumuni ya ziara hii ni pamoja na:

i. Kuwashukuru wananchi kwa kutupa dhamana ya kuongoza Kata hizi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

ii. Kushiriki kazi za Maendeleo katika Kata, na kushawishi utekelezaji wa maono ya Azimio la Tabora kwenye miradi ya Maendeleo ya Kata zinazoongozwa na ACT Wazalendo.

iii. Kuzungumza na Kamati ya Maendeleo ya Kata kuhusu mipango ya Maendeleo ya Kata na kutafuta majawabu ya changamoto hizo za Maendeleo. 

iv. Kuzungumza na Wananchi wa Kata husika na kusikiliza kero zao, kuzibeba kuzifikisha kwenye mamlaka husika au kuzitatua inapobidi 

v. Kukagua utendaji wa madiwani kutokana na matarajio ya Wananchi na ya Chama. 

vi. Kutambua vikwazo na changamoto za Madiwani wetu Katika kutekeleza kazi zao. 

vii. Kusisitiza Uwazi, Uwajibikaji na Ushirikishwaji wa wananchi kwenye masuala yote ya Kata.

viii. Kufanya tafiti juu ya masuala ya kisera pamoja na miradi ya maendeleo ambayo ACT Wazalendo Taifa tunaweza kuyabeba kusaidia madiwani wetu kupitia Taasisi Maalumu tuliyounda kwa ajili hiyo.

Mpaka sasa tumeshatembelea mikoa miwili, Pwani na Morogoro, yenye kata tano zenye madiwani wa ACT Wazalendo. Tumetembelea kata nne ambazo ni:

1. Kiparang’anda, Halmashauri ya Wilaya Mkuranga
2. Mbwawa, Halmashauri ya Mji wa Kibaha
3. Tomondo, Halmashauri ya Wilaya Morogoro.
4. Kikeo, Halmashauri ya Wilaya Mvomero.

Jana ilikuwa tutembelee Kata ya Luela katika Halmashauri ya Wilaya Mvomero, na hivyo kukamilisha kuzitembelea Kata zote tano, lakini tulishindwa baada ya tukio la kukamatwa na polisi juzi usiku na kulazwa ndani, Kituo Kikuu cha Polisi cha Morogoro, kabla ya kuachiwa kwa dhamana jana asubuhi, Februari 23, 2018. Leo tunaendelea na ziara kwenye Mkoa wa Arusha, kata ya Sale, Wilaya ya Ngorongoro.

Kushikiliwa na Polisi

Baada ya kumaliza ziara ya kikazi katika kata ya Kikeo, msafara wetu ulianza safari ya kupanda milima ya Uluguru kuelekea kata ya Luela. Kutokana na kukosekana kwa barabara ya kuingia na kutoka katika kata hii, tulitembea mwendo mrefu kabla ya kufika eneo ambalo diwani wetu alituandalia pikipiki zilizotufikisha kata ya Luela. Tulipofika tu eneo hilo tulikutana na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Mgeta akitusubiri na kunieleza kuwa ametumwa na wakubwa wake wa kazi kunikamata na kunifikisha kituoni. 

Tulikwenda kituoni, umbali wa kilometa tano kutoka eneo hilo, na hapo tukakutana na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mvomero ambaye alidai kuwa pale kituoni Mgeta hakuna Umeme na hivyo atanipeleka kituo cha Polisi cha Wami Dakawa, wilayani. Hata hivyo tulipofika Morogoro Mjini gari iliyonichukua nikilindwa na maafisa wawili wa polisi ilinifikisha kituo kikuu cha Polisi cha Morogoro.

Nilichukuliwa maelezo yangu na kuelezwa kuwa ninatuhumiwa kufanya mkutano wa hadhara bila kibali na kukiuka kifungu cha 74 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 (Penal Code). Niliwaeleza polisi kuwa sijafanya mkutano wa hadhara na ningefanya wao polisi wangejua kwani tungetoa Taarifa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya siasa, sheria namba 5 ya mwaka 1992. Pia tuliwaeleza polisi kuwa Ziara yetu ni ya kukagua kazi za Maendeleo za Madiwani wetu na kuwasaidia kuondokana na changamoto za maendeleo za kata zao, hivyo hata kama kungekuwa na mikutano ya hadhara kifungu hicho cha 74 hakina mahusiano yeyote na kazi za Kiongozi wa Chama cha Siasa kutembelea kata ambazo Chama chake kimepewa ridhaa na wananchi na kuhamasisha shughuli za Maendeleo. Licha ya dhamana kuwa wazi, nililazwa selo kwa kisingizio kuwa muda ule ni usiku sana na hivyo hawawezi kunipa dhamana.

Watanzania wanateseka sana Mikononi mwa Polisi

Usiku mmoja niliolala Kituo Kikuu cha Polisi Morogoro umenionyesha namna ambavyo raia wetu wengi wanateseka kwa haki zao za msingi kuvunjwa ikiwemo haki ya kufikishwa mahakamani. Nilimweleza RPC wa Morogoro kuwa pale kituoni kuna watu wamekaa mwezi mzima bila kuandika maelezo ya makosa wanayotuhumiwa nayo na bila kufikishwa mahakamani. 

Pia kuna watu wanateswa sana na mmoja nimemkuta hajapelekwa hospitali ilhali akiwa amevunjwa mbavu kutokana na mateso aliyoyapata akiwa mikononi mwa Polisi. Nimempa majina ya kila mtu na suala lake RPC. Nimemwomba ahakikishe wananchi hawa, wawe na makosa au la, wanapata haki zao za msingi. Nitafuatilia utekelezwaji wa hayo.

Diwani na Mtendaji wa Kata wanatishwa na Mkuu wa Wilaya

Taarifa ambazo tumezipata jana ni kwamba Mkuu wa Wilaya ya Mvomero ameanza kuwatisha watendaji wa vijiji na kata tuliyotembelea na kuwahoji kwanini wameshiriki katika ziara yetu. Pia Diwani wetu ameitwa Kituo cha Polisi cha Mgeta kwa mahojiano. Tumesikitishwa sana na hatua hizi za unyanyasaji wa watumishi wa umma ambao wajibu wao ni kuhamasisha maendeleo. 

Mkuu wa Wilaya ambaye hajawahi kufika katika vijiji tulivyokwenda hata siku moja tangu afike Mvomero, anapoamua kupambana na viongozi wanaofika na kuchochea maendeleo inatoa ishara tu kuwa ni Mkuu wa Wilaya asiyetaka Maendeleo bali anayetaka kujipendekeza kwa wakubwa kuwa anadhibiti vyama vya Upinzani.

Hali ya Nchi kiujumla

Hali ya usalama wa wananchi wetu imeendelea kuwa mbaya siku hadi siku. Mauaji ya raia yanaendelea na bahati mbaya sana mauaji haya yana sura zote za kisiasa. Chama chetu kinalaani kwa nguvu zote vitendo vyote vya mauaji dhidi ya wananchi na dhidi ya viongozi wa kisiasa. 

Hivi sasa utamaduni wa mauaji unaanza kuwa wa kawaida kiasi kwamba raia wakihoji mambo haya vyombo vya dola vinasema mbona hamhoji haya mengine kana kwamba mauaji yakitokea kwa wengi ni jambo sahihi. Waswahili husema kifo cha wengi ni harusi, lakini haina maana kuwa upande mmoja wa kiitikadi ukipata maafa basi na upande mwengine upate maafa. 

Tangu mauaji ya kibiti na baadaye kufuatiwa na uokotwaji wa watu kwenye viroba katika fukwe zetu na sasa mauaji ya kutisha ya kutumia risasi za umma na mapanga na mashoka, Chama chetu kimekuwa kikilaani vikali vitendo hivyo. Nchi yetu inapata doa kubwa, na ile sifa yetu ya kuwa nchi ya amani na usalama inaanza kutoweka siku hadi siku.

Tunasikitika zaidi pale tunapoona vyombo vya dola vyenye dhamana ya kufanya uchunguzi vikiwa ni watuhumiwa wa kwanza kwenye mauaji haya ya raia. Tunaumia zaidi tunapoona propaganda za kisiasa zikitumika kwenye misiba, sisi kama Chama cha Utu tunaona kana kwamba tunawadhalilisha marehemu kwa kuweka propaganda mbele zaidi ya utu wao. 

Matukio mengi ya mauaji nchini hayafanyiwi uchunguzi na wala Taarifa za uchunguzi haziwekwi wazi. Itafikia wakati wananchi watapoteza imani kabisa na vyombo vya dola na hapo ndipo nchi yetu itatumbukia kwenye maafa kama tunayoshuhudia kwa nchi jirani.

Hali ya Demokrasia ya Vyama Vingi

Tanzania sasa ina dalili zote za kuvunja mfumo wa vyama vingi. Mahusiano kati ya vyama vya siasa yamekuwa ya uadui zaidi kuliko ushindani wa kisiasa. Hama hama ya wanachama kutoka chama kimoja kwenda kingine ni haki ya kikatiba ya raia lakini namna inavyofanywa sasa inajenga chuki miongoni mwa wananchi na kuleta hasara kubwa kwa Taifa letu. 

Ubinywaji wa haki za kisiasa kwa vyama vya siasa vya Upinzani, ikiwemo kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara ya vyama kinyume na katiba, kunajenga hisia kuwa watawala wa sasa hawataki mfumo wa vyama vingi. Kufanya siasa nchini sasa imekuwa ni jambo la hatari kiuslama. Hizi ni dalili mbaya sana.

Nini kifanyike?

Tunatumia nafasi hii kupendekeza ifuatavyo;

1. Uitishwe Mkutano wa Kitaifa wa maridhiano ya kisiasa ambapo changamoto zote za uendeshaji wa siasa nchini zijadiliwe na kukubaliana kanuni za demokrasia ya vyama vingi. Hii ni kutokana na dhahiri kwamba mfumo wa vyama vingi nchini upo hatarini zaidi kuliko wakati wowote. Asasi za Kiraia, Vyama vya Wafanyakazi, Vyama vya Wafanyabiashara na Vyama vya Wakulima na Wafugaji vinaweza kusaidia sana kuwezesha Mkutano huu wa Kitaifa wa kisiasa (National Political Conference). Hali ya kisiasa ya sasa sio ya kuachia wanasiasa peke yake maana sasa inahusu uhai wa watu na wengine wala hawajihusishi na siasa. 

2. Mkutano huu utoe Azimio la kufanya mabadiliko makubwa kwenye mfumo wa siasa ikiwemo kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi, mabadiliko makubwa ya Jeshi la Polisi ili kulifanya kuwa linatoa huduma ya kulinda raia badala ya kutesa raia (Police Service badala ya Police Force), na mabadiliko makubwa ya Kitengo cha Usalama wa Taifa ili kihusike na kulinda usalama wa Dola letu badala ya kuwa chombo cha chama kimoja cha siasa.

3. Iundwe Tume Huru ya Uchunguzi ili kuchunguza matukio yote ya mauaji ya raia kuanzia Kibiti mpaka mauaji ya siku za karibuni ya raia wa kawaida, viongozi wa kisiasa na hata majaribio ya kuua baadhi ya wabunge ambao wengine sasa wapo hospitali wakiendelea na matibabu. Tume ya Haki za Binadam ambayo ingeweza kufanya kazi hii kwa sasa haina makamishna, baada ya waliokuwepo kumaliza muda wao. Kuna haja ya kushinikiza uchunguzi huru wa Tume ya Majaji, au wa kimataifa chini ya Umoja wa Maarifa kuhusu vitendo hivi vya kinyama katika nchi yetu.

Hitimisho

Nchi yetu ni ya demokarsia ya mfumo wa vyama vingi. Ni wajibu wa kila raia kuulinda mfumo huu kwani una faida kubwa kwa nchi yetu. Kulinda demokrasia yetu ni kulinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa kuwa kuna dalili zote za kurudishwa kwenye mfumo wa Chama kimoja, umefika wakati Watanzania wasimame na kuilinda Katiba. Wajibu wa kuilinda Katiba yetu ni wetu wote, wananchi, askari wetu wa majeshi yote, na hata Jeshi la Polisi, tuutimize wajibu wetu Mkuu wa KULINDA KATIBA. Tuilinde.

Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo 
Februari 24, 2018
Arusha

No comments: