Tuesday, February 27, 2018

WACHIMBAJI WADOGO WA DHAHABU MKOANI GEITA WATAKIWA KUWA WATULIVU.

Baadhi ya wachimbaji wadogo wakimsikiliza Naibu Waziri wa madini, Staslaus Nyongo.
Joel Maduka, Geita.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amewata wachimbaji wadogo wa mgodi wa Nyakafulu na Bingwa kudumisha amani na utulivu katika shughuli zao  ikiwemo  kujenga desturi ya kufanya usafi wa mazingira ili kuepukana na magojwa ya mlipuko na  iwapo hawatazingatia hayo migodi  hiyo itafungwa.
Hayo aliyasema wakati wa ziara yake ya kuwatembelea wachimbaji wadogo kwenye wilaya za  Mbongwe na  Geita.
Alisema ni vyema  wachimbaji hao kuzingatia amani na afya zao kwani ndio utaratibu uliowekwa na serikali iwapo ikitokea  magonjwa ya mlipuko kama   kipindupindu migodi hiyo itafungwa  mara moja.
“Mpo hapa  kwa sababu ya kauli ya Mheshimiwa Dkt.John Magufuli lakini vilevile akisikia kwamba hapa hakuna amani na sio wasafi  mimi nitatoa amri ya kufunga mgodi huu kwani wizara yangu ndio inahusika  kutoa leseni hivyo pamoja na hayo  yote amani itawale”alisema Naibu waziri.
Kwa upande wake Rais wa shirikisho la  wachimbaji wadogo wa madini nchini John Bina aliwasisitiza wachimbaji wadogo kujenga desturi ya kulipa kodi ili waweze kuchimba kwa kufata  utaratibu, sheria, na kanuni za nchi bila bugudhi  yoyote na wagawane kwa utaratibu bila kudhulumiana kwa sababu sehemu wanayochimba kuna leseni ya mtu kwa hiyo wachimbe kwa kuweka akiba ili na wao baadae wakate leseni zao za uchimbaji.
‘’Wachimbaji mmekuwa na tabia ya kula bata na kuhonga pesa zote mnapouza madini acheni tabia hiyo wekeni akiba mkate leseni zenu za uchimbaji zitawasaidia hapo baadae”Alisema Bina.
Hata hivyo  wachimbaji hao wamemuomba  Naibu waziri wa madini Nyongo kuwasaidia kupata leseni ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira yao na vitendea kazi kwa sababu wamekuwa wakitumia njia za asili katika kufanya shughuli zao za uchimbaji.
Naibu waziri wa madini,Staslaus Nyongo amemaliza ziara yake ya siku tatu mkoani Geita,kwa kutembelea migodi mikubwa na midogo huku akisikiliza kero za wachimbaji wadogo na kutatua changamoto ambazo zilikuwa zikiyakabili maeneo hayo.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akizungumza na wachimbaji wadogo wa Kijiji cha Nyakafulu wilayani Mbongwe wakati alipokuwa kwenye ziara yake ya kikazi Mkoani Geita.
Naibu Waziri wa Madini,Stanslaus Nyongo akiwa kwenye shimo ambalo linatumika kuingilia ndani kwaajili ya kuchimba.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akizunguka na kukagua baadhi ya maeneo ya mgodi wa Nyakafulu.
Rais wa shirikisho la wachimbaji wadogo wa madini nchini, John Bina akizungumza na wachimbaji wadogo wa Nyakafulu wilayani Mbongwe.
Iddy Mrisho ambaye ni mchimbaji akielezea masikitiko yake na namna ambavyo wamekuwa wakinyanyasika kutoka kwa viongozi wa vikundi.


Wachimbaji wadogo wakiwa wamebeba mabango ambayo yanaelezea kero zao.

No comments: