Sunday, March 25, 2018

KITUO CHA SAUTI YA JAMII CHAIBUKA NA MBINU MPYA YA KUTOA ELIMU BILA MKUSANYIKO, ILI KUKWEPA CORONA

Wakati serikali ya Tanzania ikiungana na mataifa mengine duniani katika kusitisha mikusanyiko isiyo ya lazima, hii ikiwa ni pamoja na kuweka zuio la mikutano, semina na makongamano mbalimbali ili kupunguza maambukizi ya ugonjwa hatari wa Corona unaoisumbua dunia kwa sasa.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sauti ya Jamii Kipunguni Selemani Bishagazi akibandika kipeperushi katika moja ya bajaji, hii ikiwa ni moja ya kampeni yao waliyoipa jina la Waelimishe bila Kuwakusanya.

Katika kutii na kutekeleza agizo hilo la serikali Kituo cha Sauti ya Jamii kilichopo kata ya Kipunguni jimbo la Ukongo jijini Dar es salaam kupitia kitengo chake cha msaada wa kisheria (Paralegal) wamefanya majaribio ya kampeni yake mpya waliyoipa jina la Waelimishe bila kuwakusanya. 

Akiongea na Habari 24 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo 
Bw. Selemani Bishagazi amesema kuwa kampeni hiyo itafanyika kwa kubandika vipeperushi vyenye jumbe mbalimbali zinazoonyesha madhara ya Ukeketaji, Rushwa ya Ngono, Mimba na ndoa za utotoni pamoja na kuwahamasisha wanawake kugombea katika nafasi mbalimbali za uongozi.

 "Vipeperushi hivi tunaviweka maeneo ambayo lazima wanajamii wafike kupata huduma, lengo ni kuendeleza kutoa elimu ili kuzuia ukatili katika mazingira haya haya tunayoishi bila mikusanyiko kama ilivyoagiza Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kutofanya semina wala mikutano ili kukabiliana na Corona". alisema Bishagazi

Ameongeza kuwa inabidi tuendelee kufahamu kuwa baadhi ya watumishi wa serikali ndiyo wapo likizo, lakini watekelezaji wa vitendo vya ukatili hawajaenda likizo wapo na wanaendelea na mambo yao kama kawaida.

Katibu wa Kituo cha Sauti ya Jamii Kipunguni Sada Shifta akibandika kipeperushi katika bodaboda, ikiwani muendelezo wa kampeni ya Waelimishe bila Kuwakusanya.

Hivyo kwa kuwa nasi tunamafunzo yakutosha hatutaweza kuacha jamii ikapotea na ndio maana tumeamua kutumia njia hii mbadala ya kutoa elimu kwa jamii iliyotuzunguka.

Ameendelea kusema kuwa wamekuwa wakitoa elimu hasa kwenye mitandao ya kijamii na kugundua kuwa walengwa wakubwa wa vitendo hivi ni watoto ambao hawana simu janja(smart phone), hivyo njia hii ya vipeperushi itakuwa sahihi kuwafikia na kuwaelimisha kuhusu Viashiria, Madhara, Mbinu za kujiokoa na wapi mahali sahihi pa kutoa taarifa.

Na mwisho ametoa wito kuwa wadau wajitokeze kuibeba kampeni hii ili isambae kwenye Kata zote zilizopo ukonga ukizingatia huu ni  mwaka wa ukeketaji katika maeneo mengi ya jimbo hilo.



Baadhi ya vipeperushi vikiwa vimebandikwa katika maeneo mbalimbali ya biashara katika kata ya kipunguni.

Baadhi ya wananchi wa kata ya Kipunguni wakisoma jumbe mbalimbali zilizobandikwa na viongozi wa Kituo cha Sauti ya Jamii Kipunguni.

No comments: