Friday, March 23, 2018

UJUMBE WA ANNA MAKINDA KWA MADIWANI WANAWAKE WA JIJI LA DAR ES SALAAM


Wanawake kote nchini wametakiwa kuwa na umoja na kujenga utamaduni wa kusaidiana bila kuangalia itikadi zao za vyama au dini, kwani wanawake wote duniani wana sifa zinazoshabihiana na matatizo yanayofanana.
Spika wa Bunge Mstafu Anna Makinda akiongea na Madiwani pamoja wanaharakati kutoka kata mbalimbali za jiji la Dar es salaam.

Hayo yamesemwa mapema leo jijini Dar es salaam na Spika wa bunge mstaafu Mh. Anna Makinda alipokuwa akifungua warsha maalumu ya madiwani wanawake wa jiji la dar es salaam iliyoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP).

Mh. Makinda alisema kuwa madiwani wanawake mnatakiwa kuwa na umoja ulio imara kama wa wabunge wanawake ambao umoja huo una lengo la kusaidiana kuhakikisha wanawake wanaendelea kufanya vizuri katika uongozi bila kujali itikadi za vyama vyao.

“Sababu za kuundwa kwa umoja huu ilikuwa ni kuleta ukombozi kwa wanawake kwa kuangalia changamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi kwa pamoja bila kuangalia itikadi za vyama huku lengo likiwa ni kufikia malengo ya kuwa na usawa wa kijinsia kati ya wanaume na wanawake”. Alisema Makinda

Aidha Mh. Makinda alisema kuwa wanawake wanaweza kuongoza vizuri kuliko wanaume kwani mwanamke akiwa Diwani au Mbunge katika eneo analolitumikia ataweka vipaumbele kwenye huduma za jamii kama Maji, Afya, Elimu kwa kuwa anazijua vizuri changamoto zinazowakabili wanawake wenzake kwa kuwa na yeye amepitia changamoto kama hizo.
Semina ikiendelea kutolewa.

Spika huyo mstaafu aliendelea kusema kuwa katika kugombea nafasi mbalimbali kunakuwa na changamoto nyingi zinazowapata wanawake lakini mnachotakiwa ni kutokubali kukatishwa tamaa, kwani mtasikia maneno mengi na wengine watasema mnaenda kutafuta mabwana na siyo uongozi kwani mara nyingi harakati kama hizi wengi wanazihusisha na mambo ya kihuni.

Na mwisho aliwashauri madiwani hao kuwa wasikubali kuachia nafasi za kwa kushindwa na wapinzania wao ila wanachotakiwa kukifanya ni kujipanga vizuri mpaka watakapo amua kuachia wenyewe kama alivyo fanya yeye katika jimbo lake.

“Itakuwa nia aibu sana wewe uliyekuwa ndani kutolewa na mtu aliye nje madiwani wanawake mnatakiwa kusimama imara kutetea nafasi zenu msikubali kutetereshwa na wanaume mpaka mtakapo amua kuachia wenyewe kama nilivyofanya mimi katika jimbo langu” alisema Makinda
Mkuu wa Idara ya Ujenzi wa Nguvu za pamoja wa TGNP Bi. Grace Kisetu akitoa ufafanuzi wa jambo fulani mbele ya wageni mbalimbali mapema leo jijini Dar es salaam katika semina ya kuwafunda Madiwani Wanawake.
Kwa upande wake Mkuu wa idara ya Ujenzi wa nguvu za pamoja wa TGNP Mtandao Bi. Grace Kisetu alisema kuwa wao kama shirika la kutetea haki za wanawake wapo katika mpango kabambe wa kupigania ongezeko la wanawake katika nafasi za uongozi na maamuzi.

Aidha Dada Grace alisema kuwa mwaka 2016 disemba serikali ilipitisha mpango mkakati wa kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto na muongozo uliotolewa unaonyesha watekelezaji ni taasisi binafsi kama TGNP na halmashauri imepewa jukumu kubwa la kusimamia mpango huu.

Grace aliendelea kusema kuwa wao kama TGNP wana jukumu la kufanya chambuzi za bajeti mbalimbali za kisekta na hata bajeti kuu kwa kuangalia upande wa wanawake na watoto wanaangaliwa vipi na bajeti hizo.

Aliongezea kuwa miongoni agenda zetu itakuwa ni kujadili kwa fedha ambazo zilikuwa zikitengwa kwa ajili ya wanawake na vijana ambapo hapo mwanzo mgawanyo ulikuwa ni 5% kwa wanawake na 5% ilikuwa kwa vijana na haikutosha, lakini kwa sasa imegawanywa upya na kuwa 4% kwa wanawake na 4% kwa vijana na 2% iliyobaki kupelekwa kwenye kundi la watu wenye ulemavu.
Semina ikiendelea.



No comments: