Rais wa jamuuri ya muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli mapema leo jijini Dar es salaam anaweka jiwe la msingi la ujenzi wa mfumo wa rada za kuongoza ndege.
Mfumo huo wa rada za kuongozea ndege unajengwa katika vituo vinne vya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA); Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA); Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwanza na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe.
Ujenzi unafanywa na Kampuni ya M/S Thales Las France SAS ya nchini Ufaransa ukigharimu Sh67.3 bilioni fedha zinazotolewa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari amesema leo Jumatatu Aprili 2,2018 kuwa ujenzi utakamilika ndani ya miezi 18.
Amesema mradi huo utasaidia kurahisisha huduma za utafutaji na uokoaji kunapotokea ajali za ndege.
Johari amesema pia utaiwezesha nchi kukidhi viwango na miongozo ya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) na kujenga imani ya watumiaji wa anga ya Tanzania.
Tayari wageni wamewasili eneo la uzinduzi wakiwamo mawaziri, wabunge, mabalozi na wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewasili akiongozana na msanii wa muziki wa kizazi kipya Naseeb Abdul maarufu Diamond.
No comments:
Post a Comment