NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
MAKAMU wa Pili wa Rais,Samia Suluhu Hassan, amewataka wananchi wa visiwa vya Zanzibar kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Wabunge na Wawakilishi wa majimbo ili waongeze ari na kasi ya utatuzi wa kero zinazoikabili jamii.
Rai hiyo ameitoa leo katika mwendelezo wa ziara yake visiwani Zanzibar alipokutana na wanachama wa CCM na wananchi wa jimbo la Kikwajuni na kuzungumza nao katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa tanki la maji safi na salama lenye uwezo wa kuhifadhi lita zaidi ya 200,000 katika jimbo la kikwajuni.
Amesema endapo wananchi watakuwa mstari wa mbele kuthamini miradi ya wabunge na wawakilishi kwani inatekelezwa kwa lengo la kumaliza changamoto zinazoikabili jamii.
“Wananchi mkiwa na umoja na kushirikiana kulinda na kuthamini yale yote mazuri yanayofanywa na viongozi wenu basi itakuwa rahisi sana kutatua kero zenu kwa wakati”, amesema Mhe. Samia
Pia amewataka wabunge na wawakilishi wa majimbo mbali mbali kuwa na maelewano mazuri mazuri kwa lengo la kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa ufanisi.
Amesema kitendo cha viongozi hao kutokuwa na maelewano mazuri yanasababisha kukwamisha na kuwacheleweshea wananchi kupata maendeleo kwa wakati.
Makamu huyo wa Rais ameongeza kuwa kuna baadhi ya majimbo ambayo viongozi hao hawana ushirikiano na kwamba wanafikia hatua hawaongeii na kutofikiria kuleta maendeleo.
"Kuna majimbo ambayo wananchi wao wanakumbwa changamoto ya ukosefu wa maji na elimu na kwamba unakuta viongozi hao kati ya Mbunge na Mwakilishi hawafikirii kutatua kero za wananchi hizo kutokana na kuwa hawana ushirikiano,"amesema Samia.
Mbali na hilo katika ziara hiyo Makamu wa Rais aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa tanki la maji safi na salama jimbo la Kikwajuni pamoja na jiwe la msingi la ofisi ya tawi la Chama Cha Mapinduzi(CCM) Jang’ombe Urusi.
Hata hivyo aliwataka wananchi wa jimbo la Kikwajuni kuhakikisha wanatunza miradi ya maendeleo ya maji na kwamba wanatakiwa kuanzisha kamati ya jimbo kwa lengo la kusimamia miradi hiyo ili iwe endelevu.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar, Dk.Abdulla Juma Mabodi, amesema CCM ipo kikazi na inaenda na wakati katika kutatua kero za wananchi.
Ameeleza kuwa CCM inawahakikishia wananchi kuwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar(SMZ) imejipanga kuwatatulia changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji ambapo inaendelea kutekeleza miradi ya maji ili kuhakikisha mikoa yote ya Zanzibar inapata huduma hizo.
Naibu huyo ameeleza katika kipindi hichi cha dharura SMZ na kushirikiana mradi wa Ras Al Khaimah imechimba visima 120 vya maji visiwani Zanzibar.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni, Hamad Yussuf Masauni, amesema kupitia mradi huo wa maji wa awamu ya pili utatatua changamoto ya upatikanaji wa maji unatokana na miundombinu ilioko zamani ambapo nyingi zilikuwa mibovu mengine ilipasuka na kuziba.
"Baada ya kumalizika mradi huu tunafumua mfumo wa maji wa jimbo la kikwajuni na tunaweka mfumo mpya wa kwetu ambao safari hii maji yatapatikana kwa urahisi na wananchi mtafurahi,"amesema Mhe. Samia.
Aidha ametembelea ujenzi wa Tawi la CCM Jang’ombe Urusi na kuwapongeza viongozi wa Jimbo la Jang’ombe kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM na kuwataka wawe walimu wa majimbo mengine.
Wakati huo huo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia ameweka Jiwe la msingi katika Ofisi ya Watu Wenye Ulemavu Jimbo la Shauri Moyo Unguja, na kuipongeza jumuiya hiyo kwa ubunifu wao wa kujenga ofisi ya kuzalisha kipato.
Amezitaka familia zenye watu wenye ulemavu kuwapeleka katika ofisi hiyo ili wajifunze fani mbali mbali zitakazowasaidia katika maisha ya kila siku.
Ameahidi kutatua hatua kwa hatua changamoto zinazoikabili jumuiya hiyo ambazo ni pamoja na ukosefu wa viti vya watu wenye ulemavu, mashine ya photokopi ya rangi na mahitaji mengine.
Katika Hafla hiyo Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Mabodi amesema Ofisi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar imeahidi kuchangia shilingi 500,000 kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za watu wenye ulemavu.
Hata hivyo ametembelea Chuo Cha Mwenge Community Centre kinachotoa mafunzo ya fani mbali mbali yakiwemo ya ushoni, umeme, computer, Uuguzi na Uandishi wa habari kinachomilikiwa na CCM Mkoa wa mjini.
Mapema Katibu wa CCM Mkoa wa Mjini Ndugu Mohamed Nyawenga alisoma na kumkabidhi taarifa ya hali ya kisiasa kwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Bi. Samia Suluhu Hassan.
Kupitia kikao hicho aliwataka viongozi na watendaji wa Mkoa huo kufanya kazi kwa bidii sambamba na kulinda heshima ya Mkoa huo wenye historia kubwa ya uimara wa kisiasa na kijamii nchini.
Pia amewaagiza kutunza vizuri miradi ya maendeleo inayomilikiwa na Mkoa huo ili kwenda sambamba na sera ya siasa na uchumi.
No comments:
Post a Comment