Wednesday, April 11, 2018

TANZANIA YALAANI KAULI YA CHIEF RABBI DHIDI YA WAAFRIKA

KAMATI ya Mshikamano wa Tanzania na Palestina inalaani vikali matusi yaliyotamkwa na mkuu wa dini ya Wayahudi nchini Israel, Chief Rabbi Yitzhak Yosef ambaye, wakati wa mahubiri  aliwafananisha Waafrika na kima.
Baada ya Waafrika kufananishwa na Kima kamati ya Mshikamano ya Tanzania na Palestina yatoa Tamko hili
Yosef ni mmoja kati ya wachungaji wawili wakuu wanaoteuliwa na serikali ya Israel. Alipokuwa akihubiri katika hekalu la Kiyahudi hivi majuzi aliwazungumzia Waafrika na akatumia neno “kushi” amabalo katika lugha ya Kiibrania ina maana ya “kima” .

Hii si mara ya kwanza kwa mchungaji huyu mkuu wa Israel kutumia maneno ya kuwadhalilisha Waafrika. Katika mahubiri yake ya Mei mwaka jana alisema wanawake wana tabia ya wanyama kwa sababu ya mavazi yao. Halafu mnamo Machi 2016 alitangaza kuwa watu wasio Wayahudi hawapaswi kuishi nchini Israeli

Mawazo ya mchungaji huyu hayakubaliki, lakini hayashangazi sana kwa sababu wakati wote Israel yenyewe imekuwa na msimamo wa kuwabagua na kuwadhalilisha Waafrika na wazawa Wakipalestina. Ukaburu huu umekuwa ukiongezeka, siyo tu miongoni mwa Wayahudi wa Israeli bali hata miongoni mwa serikali ya Israel na watendaji wake.

Ndio maana hivi sasa Israel iko mbioni kuwafukuza maelfu ya Waafrika wanaoishi na kufanya kazi huko. 

Tayari onyo limetolewa kuwa kuanzia tarehe 1 Aprili 2018 kama Waafrika hao hawataondoka basi watakamatwa na kufungwa gerezani bila kikomo.

Israel imetangaza kuwa Waafrika wanaoishi ni tishio kwa utambulisho wa Kiyahudi. Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyau amekuwa akitaka wafukuzwe na kusema kuwepo kwao nchini Israel ni tishio kwa “amani na usalama”. Amesema Waafrika hao ni magaidi

Naye waziri wake wa mambo ya ndani, Eli Yishai amesema Waafrika walio Israel wanapaswa wajue kuwa nchi “hii ni yetu sisi watu weupe”. Na waziri wa utamaduni na michezo , Miri Regev amesema Waafrika ni sawa na maradhi ya “saratani”

Hii ni Israel, nchi ya kikaburu ambako wanafunzi katika chuo cha uhandisi wanaulizwa suali kuhusu mapanya wanaopaswa kukamatwa na kuangamizwa. Mapanya hao si wengine bali ni Waafrika

Hii imefanyika katika chuo kikuu cha Ben-Gurion ambako mkuu wa kitivo cha uhandisi, “Profesa” Moshe Kaspi ametoa suali kwa wanafunzi wake likisema katika kazi ya kuchimba mtaro ili kujenga reli ya chini ya ardhi jijini Tel Aviv, wanakutana na mapanya wengi. Inaamuliwa kuwasafirisha panya hao hadi Afrika ambako wanahitajika katika utengenezaji ya chanjo ya kichaa cha mbwa. 

Na ndio maana duniani kote kumekuwepo na kampeni ya kulaani ukaburu huu wa Israel katika mtandao wa jamii  (#IsraeliApartheidWeek). Huko Afrika Kusini kampeni hii iliendeshwa kati ya tarehe 12 na 18 Machi pamoja na mikutano katika miji kadha. ili kupata habari kamili kuhusu huu ubaguzi na ukaburu wa Israel dhidi ya Waafrika

Hata katika jiji la Tel Aviv watu takriban 25,000 wamekusanyika kupinga sera ya Israel ya kuwafukuza Waafrika ambao wameomba hifadhi. 
Mabango yalibebwa yakisema “Hakuna tofauti kati ya damu zetu, ni kwa sababu sisi sote ni wanadamu”

Walikuwa wanapinga sera ya Israel ya kuwasafirisha Waafrika hadi Rwanda na Uganda . Kati yao ni watu karibu 38,000 kutoka Eritrea na Sudan ambao tayari wamepewa notisi yaa kuondolewa na kupelekwa Uganda na Rwanda.

Hata Waafrika walioingia Israel kwa kudai wao ni Wayahudi nao wanakabiliwa na tishio la kufukuzwa. Chini ya ukaburu wa Israel sasa wanaambiwa wao sio Wayahudi
Almuradi Israel si tofauti na Afrika Kusini wakati wa utawala wa makaburu. Ndio maana ulimwengu leo unaendesha kampeni ya kuwawekea vikwazo kama ilivyofanyika wakati ule wa makaburu wa Afrika Kuini (BDS)


Aidha, Kamati inaungana na jumuiya ya Kimataifa katIka maadhimisho ya siku ya ARDHI YA PALESTINIA kwa kulaani uendeleaji wa uporaji wa ardhi ya Wapalestina. Katika maandamano ya Amani ya kuadhimisha siku ya ARDHI  yaliofanyika huko Ukanda wa Gaza Wapalestina 17 waliuliwa

Maandamano hayo yanaendelea huko Gaza na jumla ya Wapalestina 30 wameuliwa na mamia kujeruhiwa na wanajeshi wa Israel wanaotumia risasi za moto, vifaru na mabomu ya machozi. Kati ya waliouawa ni mwanahabari wa Kipalestina aliyevaa nguo zilizomtambulisha kuwa ni mwandishi na Waandishi wengine watano wamejeruhiwa
Tunalaani kwa nguvu zote mauwaji hayo. 

Kamati inasikitika  kwa jumuiya za kimataifa kukaa kimya licha ya mauaji haya ya waandamanaji wasio na silaha yanayoendelea hadi  leo.
Kamati inaiomba serekali na Jamii ya Watanzania kuzidi kupaaza sauti zao katika kulaani na kupinga ukandamizwaji na mauwaji wanaofanyiwa ndugu zetu wa Palestina na watawala wa Israel

Kamati inawaomba Watanzania wasikae kimya katika suala hili na tukumbuke maneno yafuatayo ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Ikiwa kweli tunataka kumuenzi tuyatekeleze maneno yake kwa vitendo.
"Hatujawahi kusita katika kuunga mkono haki ya watu wa Palestina kuwa na ardhi yao. Kizazi chetu kilikuwa ni kizazi cha harakati za kitaifa kwa ajili ya uhuru wa nchi yetu na hivyo ndivyo tulivyokuwa. Lakini masaibu ya Wapalestina ni mabaya zaidi na yasiyo halali, wanaporwa nchi yao, wao ni taifa bila ardhi. Na kwa hivyo wanastahili uungwaji mkono wa Tanzania na Dunia kwa ujumla."
-Mwalimu Nyerere

AHSANTENI
ABDULLAH M.OTHMAN
MWENYEKITI.
KAMATI YA MSHIKAMANO WA TANZANIA NA PALESTINA

No comments: