Saturday, June 18, 2022

Haya hapa Mapungufu yaliyopo katika Bajeti kuu ya 2022/2023 uchambuzi uliyofanywa na LHRC.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)  Wakili Anna Henga.

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeainisha mapungufu matatu katika Bajeti ya Taifa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 iliyowasilishwa hivi karibuni bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba.

Mapungufu hayo yameainishwa leo Juni 17, 2022 Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC Wakili Anna Henga wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uchambuzi wa makadirio ya mapendekezo ya Bajeti hiyo kwa mtazamo wa haki za binadamu.

Ametaja mapungufu hayo kuwa yanagusa maeneo ya matumaini ya Watanzania kuhusu Bima ya Afya kwa wote, Jinsia na Bajeti ya Taifa ya mwaka 2022/2023 na Ada mpya za ving'amuzi.

Akitolea ufafanuzi kuhusu matumaini ya Watanzania kuhusu Bima ya Afya kwa wote, Wakili Henga amesema kwamba baada ya kilio cha muda mrefu cha Watanzania wa kipato cha chini kukosa huduma za Afya kutokana kutokuwa kwenye mfumo wa Bima,

Kwamba mjadala umeibuka katika miaka ya hivi karibuni juu ya umuhimu wa Bima ya Afya kwa watu wote.

“Mara kadhaa watenaji wa Serikali na Viongozi wamesikika wakieleza juu ya umuhimu wa mpango wa Bima ya Afya kwa wote. LHRC imeshangazwa na ukimya wa Bajeti ya mwaka 2022/2023 kuhusu suala ya Bima ya Afya kwa wote,” amesema Wakili Henga.

Hivyo, LHRC inapendekeza kwa Serikali na Bunge kuzingatia hitaji la kutenga Bajeti kwa ajili ya Bima ya Afya kwa wote.

Kuhusu Jinsia na Bajeti ya Taifa ya mwaka 2022/2023, Wakili Henga amesema kwa watetezi wa haki za binadamu na usawa kijinsia, bajeti ya mwaka 2022/2023 imekuwa na mapungufu kadhaa ya kijinsia.

“Kwa mfano, ingawa Waziri wa Fedha na Mipango amesifu Wanawake kwa kiwango kizuri cha urejeshaji wa mikopo, imekuwa mshangao kuwa bajeti inapendekeza kushushwa kwa asilimia ya mikopo ya Wanawake kupitia Halmashauri kutoka asilimia 4 hadi 2,” amesema Wakili Henga na kuongeza kwamba,

“LHRC inapendekeza kwa Serikali na Bunge kurudisha kiwango cha awali,”.

Pia, amesema baadhi ya bidhaa zitumiwazo na Wanawake ikiwemo nywele za bandia zimeongezwa ushuru wa forodha kutoka asilimia 25 mpaka 35 kwa madai ya kuendana na makubaliano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kwamba mbaya zaidi kwenye taulo za za watotozi (Baby diapers) ambazo ni msaada mkubwa katika malezi ya watoto zinazoagizwa toka nje zimepandishiwa ushuru wa forodha kutoka asilimia 25 hadi 35.

“LHRC inaona kuwa hii sio haki kwa watoto na Wanawake ikizingatiwa kuwa uzalishaji wa ndani ya nchi haukidhi mahitaji kamili na kwamba ubora wake bado ni changamoto. Kijinsia, kupanda kwa ushuru wa forodha kwa taulo za watoto kunahatarisha Afya ya ngozi ya mtoto,” ameongeza Wakili Henga.

Kwa upande wa ada mpya za ving’amuzi, Wakili Henga ameeleza kwamba Wakati Watanzania wakitafakari kuhusu tozo kadhaa ambazo tayari zimepandishwa na mfumo wa kodi nchini, bajeti ya mwaka 2022/2023 inapendekeza kuanzishwa ada mpya ya matumizi ya ving’amuzi ambayo itakuwa ni Kati ya shilingi 1,000 hadi 3,000 kulingana na kiwango cha matumizi.

Wakili Henga amesema, maoni ya LHRC ni kwamba ada hii mpya ni mzigo wa ziada kwa watumiaji wa huduma ya ving’amuzi kwamba Haki hiyo inaweza kukwamisha juhudi za Serikali kuongeza kiwango cha upashanaji habari nchini kinyume na ibara ya 18 ya katiba.

Hivyo LHRC imependekeza kuiondoa kodi hiyo kwa kuwa itaongeza gharama za vufurushi na kuongeza mzigo kwa wananchi na kupelekea kuminya haki ya kupata taarifa.

No comments: