Monday, July 4, 2022

MHE. MCHENGERWA SERIKALI KUJENGA STUDIO KILA WILAYA NCHINI

Na John Mapepele

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema Serikali inakwenda  kutengeneza studio kila wilaya kwa ajili ya kurekodia kazi za sanaa.
Mhe. Mchengerwa ameyasema haya leo Julai 3, 2022 wakati akifunga tamasha la kwanza la  kitaifa la utamaduni katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Amesema wizara yake inakwenda  kutekeleza maelekezo ya viongozi wetu ya kuthamini, kuandaa  mavazi ya taifa ili kuhakikisha mila na desturi za mtanzania zinaendelezwa.

"Maelekezo ya viongozi wetu ni sheria, amri iwe jua, iwe mvua  sisi Wizara, tutawajibika kutekeleza bila kusita wala kuchelewa" Amesisita Mhe. Mchengerwa

Pia amesema  wizara imejipanga vizuri kuhakikisha Tamasha la kitaifa la pili la Utamaduni litakalofanyika mwakani litakuwa katika kiwango cha kimataifa.

Ameongeza kuwa kumalizika  kwa tamasha hili ni mwanzo wa kuanza maandalizi ya matamasha kwenye mikoa  na wilaya zote nchini ambapo ametaka maafisa utamaduni kulisimamia hili.

"Ni matarajio yangu kuwa mikoa yote itakaoanza sisi kama wizara tutakuja mara moja. Tunahitaji watanzania wakae katika furaha katika maisha yao" amefafanua Mhe. Mchengerwa

Amewapongeza wakuu wa mikoa  kwa kuwezesha  vikundi  vya Utamaduni kuhudhuria kwenye tamasha.

Amesema  bila Utamaduni taifa hili litaendelea kukopa tamaduni za mataifa mengine.

Aidha, amesema  kufanikiwa kwa tamasha hili kuonekana  ni kutokana na maono ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan 

Amesisitiza kuwa tamasha hili litakuwa endelevu na litakuwa  linafanyika kwa mzunguko kila mkoa.

Pia amesema Wizara imefanikiwa kulitangaza tukio hili kwa  kuwa watu zaidi ya milioni  10 wametazama kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.

"Niseme kwa hili tumefanikiwa" amepongeza Mhe. Mchengerwa

Kwa upande mwingine Selikali imeanzisha Mfuko wa Utamaduni kwa lengo la kuwasaidi wasanii nchini ambapo amesema tayari kwa mwaka 2022/2023 umetengewa shilingi bilioni mbili kwa kazi hiyo.

Amewaomba viongozi wa mila  na wananchi kwa ujumla kuendelea kukemea vitendo ambavyo ni kinyume cha maadili ya mtanzania.

Pia amewataka wananchi kushiriki kwenye sensa.

Katika tamasha  hilo amekadhi zawadi kwa washindi wa ngoma na vyakula ambapo washindi wa ngoma za asili ni mkoa wa
Mwanza ambao umekuwa namba moja, Lindi ambao umekuwa namba mbili na mkoa wa
Mjini magharibi umekuwa wa tatu.

Kwa upande wa vyakula vya asili mkoa Kilimanjaro umeongoza ukifuatiwa na mkoa wa Tanga na mkoa wa Kagera umeshika nafasi ya tatu

   Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa akikabidhi Zawadi kwa  Vikundi vya Ngoma za Asili vilivyofanya vizuri vikiongozwa na Mkoa wa Mwanza, wakifuatiwa na Lindi na mshindi wa tatu ni Mkoa wa Magharibu kutoka Zanzibar katika  kucheza ngoma za Asili kwenye  Tamasha la kwanza la Kitaifa la Utamaduni lililofanyika Julai 01 hadi 03,Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.

No comments: