.

RUSHWA YA MIA TANO YAWAUMBUA WALIMU WA SHULE YA MSINGI HUKO MBEYAA

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), mkoani Mbeya imewanasa walimu wawili wa Shule ya Sekondari ya Forest kwa tuhuma za kushawishi na kupokea rushwa ya kati ya Sh500 na Sh1,000 kwa wanafunzi wanaochelewa asubuhi.

Imeelezwa kwamba kutokana na mtindo huo, walimu hao wamekuwa wakijikusanyia wastani wa Sh150,000 kwa siku.

Walimu hao walikamatwa saa 8.30 mchana jana shuleni hapo baada ya baadhi ya wanafunzi kutoa taarifa Takukuru za kuwapo kwa tabia hiyo ya kulazimishwa kutoa fedha wanapokuwa wamechelewa kufika shuleni asubuhi.

Kamanda wa Takukuru wa Mkoa wa Mbeya, Daniel Mtuka, aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake kwamba walimu hao (majina tunayo), walitiwa mbaroni wakati wakiwatoza wanafunzi hao fedha hizo.

Hadi wanakamatwa, walimu hao walikutwa na kiasi cha Sh64,000 walizokuwa wamezikusanya kutoka kwa wanafunzi hao, huku pembeni kukiwa na rundo la fimbo lililokuwa likitumika kuwachapa.


Mtuka alisema waligundua kuwa walimu hao walikuwa wanatengeneza kiasi cha 150,000 kwa siku kutokana na wastani wa wanafunzi 300 waliokuwa wanawachapa. Shule hiyo ina wanafunzi 900.

“Walimu hao wamekuwa na mradi huo wa kuwalipisha wanafunzi na wanaoshindwa kulipa walikuwa wanachapwa viboko visivyokuwa na idadi,” alisema na kuongeza:

“Kwanza walimu hao walikuwa wanachukua majina ya wanafunzi waliochelewa kutoka kwa walimu walioko zamu na kuanza kuwaita kwenye chumba walichokuwa wanakiita ‘Gwantanamo’ na kutoza fedha hizo.”

Walimu hao walichukua jina hilo kutoka Kambi ya Guantanamo Bay iliyoko karibu na Kisiwa cha Cuba, ambako Marekani imeweka kambi ya kijeshi.

Kambi hiyo ilianzishwa Januari, 2002 wakati Marekani ikiwa chini ya George Bush kwa ajili ya kuhifadhi mateka wa kivita kutoka Afghanistan na Iraq.

Kwa nyakati tofauti, wanafunzi walisimulia vituko vya walimu hao.

Mwanafunzi wa kidato cha kwanza, (jina tunalihifadhi), alisema kuwa mwanafunzi ambaye alikuwa hana fedha za kuwapatia, alikuwa anaambiwa kuweka kichwa chini, miguu na miguu juu kisha mwalimu huyo anamchapa kwenye makalio hadi sehemu unapopita uti wa mgongo.

“Baada ya kuona vitendo hivyo vinaendelea, huku uongozi wa shule ukiwa umekaa kimya, tukaamua kuwaambia viongozi wa serikali ya wanafunzi na ndiyo waliokwenda Takukuru,” alisema.

Hata hivyo, Mkuu wa Shule hiyo, Cecilia Kakela alisema alikuwa hajawahi kuviona vitendo hivyo na alikuwa hajui lolote.

Alisema kuwa wanaendelea na mahojiano na walimu hao na baada ya hapo watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani.

About HABARI24 TV

Post a Comment
Powered by Blogger.