FC Twente imeandika katika tovuti yake kwamba wakati wowote kuanzia sasa, Kapombe anayetumika kama beki wa kushoto siku hizi, atakuwa huko kwa majaribio.
Kapombe aliyezaliwa Januari 28, mwaka 1992 aliibukia katika klabu ya Polisi Morogoro kabla ya kujiunga na Simba SC miaka mitatu iliyopita ambako anatarajiwa kumalizia Mkataba wake Desemba mwaka huu.
Twente imejiridhisha klabu yake imekubali kumpa ruhusa kwenda kufanya majaribio nchini humo. “Tumepewa ruhusa kumuita kwa majaribio Ulaya na tunamtakia mafanikio,”imesema taarifa katika tovuti ya Twente, ambayo kwa sasa haina mchezaji Mwafrika kwenye kikosi chake cha kwanza.
Kapombe mwenyewe ameonyesha nia thabiti ya kucheza Ulaya na amekuwa akikataa ushawishi wa timu nyingine za Tanzania zinazotaka kumng’oa Simba SC kama Yanga na Azam FC ili kusikilizia nafasi ya Ulaya.
FC Twente maskani yake yako Enschede, ikicheza Ligi Kuu ya Uholanzi, maarufu kama Eredivisie na ilianzishwa mwaka 1926. Hawa ni mabingwa wa Kombe la KNVB na Johan Cruijff Schaal mwaka 2011, na wamekuwa mabingwa wa Eredivisie msimu wa 2009–2010.
Timu hiyo, inayotumia Uwanja wa nyumbani wa De Grolsch Veste tangu 1998, pia imeshika nafasi ya pili mara tatu Eredivisie na walikuwa pia washindi wa pili wa Kombe la UEFA msimu wa 1974–1975 na kwa ujumla wametwaa Kombe la KNVB mara tatu.
No comments:
Post a Comment