.

WABUNGE WANNE WA CHADEMA WAKAMATWA ARUSHA


Jeshi la polisi mkoani Arusha linawashikilia viongozi wanne wa CHADEMA na watu wengine 60 huku likiendelea kuwatafuta wabunge wawili  wa chama hicho na watu wengine.

Kamishina wa Operesheni wa Mafunzo wa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Paul Chagonja amesema licha ya watu hao kukamatwa pia wamekamata pikipiki 106 na baiskeli 16 ambazo zilitelekezwa.

Chagonja amewataja wanne hao waliotiwa nguvuni kuwa ni Tundu Lissu (Singida Mashariki), Mustapha 
Akunai (Mbulu) Said Arfi (Mpanda Mjini) na Joyce Nkya (Viti Maalum).

Chagonja amesema limewatia nguvuni watu hao kwa makosa ya kuhutubia mkutano haramu wakati wa kuwaaga marehemu waliopoteza maisha kwenye mlipuko wa bomu uliotokea katika eneo la Soweto jijini humo mwishoni mwa wiki.

Makosa mengine ni wanayotuhumiwa kwayo ni kufunga barabara na kuwashambulia askari polisi.

Amesema wataendelea kubaki korokoroni hadi uchunguzi utakapokamilika.

Wanaotafutwa ni pamoja na Mwenyekiti CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ambao waliponyoka mikono ya polisi.

Wabunge wengine wanaotajwa kuwepo uwanjani hapo ni pamoja na John Mnyika na Ezekiah Wenje.

Wakati huo huo, habari nyingine zinasema Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (CHADEMA) amepata ajali katika eneo la Kasheki, Hanang' baada ya gari lake kugonjana na basi la abiria na kuharibika vibaya, alipokuwa njiani kuelekea Arusha ili kuungana na wabunge wenziye katika shughuli ya kuwaaga marehemu wa mlipuko wa bomu hilo la Soweto, Arusha. Inaarifiwa kuwa hakuna aliyejeruhiwa katika ajali hiyo.

Awali, Jeshi la polisi liliipiga CHADEMA marufuku ya kufanya shughuli zozote za kuaga miili ya marehemu kwenye viwanja vya Soweto kwani zoezi la uchunguzi bado linaendelea kwenye viwanja hivyo.

Akizungumza ofisini kwake, Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas amesema ilionelewa kuwa si busara kuweka mkusanyiko wa watu kwani kutaharibu upelelezi.

Kamanda Sabas amesema kuwa kwa hiyo jeshi hilo liliwataka viongozi wa chama hicho kuwaeleza wafuasi wao mahali sahihi watakapoweza kufanyia shughuli hiyo lakini si kwenye viwanja hivyo.

Hata hivyo, viongozi wa chama hicho, wanachama na watu mbalimbali walikuwa wakiendelea kukusanyika katika viwanja hivyo kwa ajili ya maombolezo hali iliyosababisha mvutano baina yao na jeshi la polisi na hivyo kusababisha polisi kurusha tena mabomu uwanjani hapo.

About HABARI24 TV

Post a Comment
Powered by Blogger.