Akikumbushia historia kali ya mji wa Berlin
uliyogawika wakati mmoja, rais Barack Obama amezitahadharisha Marekani na Ulaya
dhidi ya kuridhika kunakosababishwa na amani, huku akiapa kupunguza silaha za
nyuklia.Rais Obama pia alitangaza kuwa programu yake ya udukuzi wa mawasiliano
iliyozua zogo duniani, imenusuru maisha katika pande zote za Atlantiki.
Akihutubia umati uliokusanyika katika lango kuu la Brandenburg, Obama alisema
ipo haja ya kupunguza kwa sana tu, silaha za nyuklia za Marekani na Urusi, ili
kuondoka katika hali ya kivita inayoendelea kuchochea kutoaminiana baina ya
serikali za mataifa hayo."Tunaweza tusiishi katika hofu ya maangamizi ya
nyuklia, lakini maadam silaha za nyuklia bado zinaendelea kuwepo, hatuna
usalama wa kweli," alisema Obama wakati akihitimisha ziara ya siku tatu
barani Ulaya, ambayo ndiyo ya kwanza tangu aliposhinda muhula wa pili. Obama
anakabiliwa na migogoro ya ndani pamoja na changamoto za sera ya kigeni,
ambavyo vinamvurugia malengo yake ya muhula wa pili. Masuala mawili - vita
vikali vinavyoendelea nchini Syria, na program ya udukuzi wa mawasiliano -
vilimzonga Obama wakati wa ziara yake nchini Ujerumani, na vile vile katika
mkutano wa kundi la mataifa nane yalioendelea kiviwanda, G8 mjini Belfast,
Ireland ya Kaskazini mapema wiki hii.
Ujerumani, nchi inayolinda sana faragha, ilitaka hasa
majibu kutoka kwa Obama kuhusiana na Programu hiyo inayoendeshwa na shirika la
usalama wa taifa la Marekani NSA. Kansela Angela Merkel, alitumia mkutano wake
na Obama kwa waandishi wa habari, kutaka kuwepo na uangalifu, katika kutathmini
wasiwasi kuhusu faragha, inagwa aliepuka kukwaruzana hadharani na rais.
"Kunahitajika kuwepo uwiano, haya ni mapambano
ambayo yataendelea," alisema Merkel. Obama alitoa utetezi mrefu wa
programu hiyo iliyoidhinishwa na mahakama, akiielezea kama juhudi makhsusi
ambayo imesaidia kunusuru maisha. "Tunafahamu kuhusu mashambulizi
yasiyopungua 50 ya kigaidi yaliyozuiwa kwa kutumia taarifa hizi, si tu nchini
Marekani, bali pia katika maeneo mengine kama hapa Ujerumani."Tukio kuu la
ziara ya Obama lilikuwa hotuba ya mchana katika lango la Brandenburg, ambako
kulikuwa na ukuta wa Berlin uliyougawa mji huo kati ya mashariki na magharibi.
Obama, aliesimama nyuma ya kidirisha cha bilauri isiyopita risasi, alizungumza
kutoka upande wa mashariki wa lango hilo, eneo ambalo enzi hizo haikuwa rahisi
kwa rais wa Marekani kukanyaga.
No comments:
Post a Comment