Wednesday, September 18, 2013

WALIOLIPUA BOMU ARUSHA WAWEKWA WAZI

MKUU WA MKOA WA ARUSHA MAGESA MULONGO
              WATUHUMIWA walioingiza mabomu ya kurushwa kwa mkono yaliyotupwa Arusha Mei na Juni katika Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti na kwenyemkutano wa wa hadhara wa Chadema, Soweto mkoani Arusha, wamekamatwa.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, alisema hayo jana katika mkutano wa siku moja wa kuzungumzia fursa za uwekezaji mkoani Arusha, uliofanyika eneo la Olasiti.
 
“Watuhumiwa hawa siku si nyingi Kamanda wa Polisi wa Arusha, ataweka majina hadharani, watu wawajue na si wageni, ila kwa sasa kinachochunguzwa ni kutaka kufahamu waliowatuma kuingiza mabomu hayo na kwa lengo gani."
 
Mulongo alisema kwa sasa Polisi iko katika hatua za mwisho za mahojiano na watuhumiwa hao, ambapo mbali na kutaka kufahamu waliowatuma na malengo yao, pia wanatarajia kupata taarifa za waliorusha mabomu hayo.
 
Malengo mengine kwa mujibu wa Mulongo ni kuwafahamu watu wote waliopewa zabuni ya kuingiza mabomu hayo, ili hatua za kisheria zifuate.
 
        Mulongo aliomba wananchi waendelee kutulia wakisubiri matokeo ya Serikali na hata wakitajwa wahusika waiachie Polisi ifanye kazi yake. Mabomu hayo yalirushwa Mei 5 kanisani Olasiti na Juni 15 uwanja wa Soweto, wakati wa hitimisho la kampeni za udiwani za Chadema mkoani hapa.
 
         Kanisani Mlipuko huo ulitokea muda mfupi baada ya kuanza kwa ibada ya uzinduzi wa Parokia hiyo, ambayo mgeni rasmi alikuwa Balozi wa Vatican nchini na Mjumbe wa Baba Mtakatifu, Askofu Fransisco Mantecillo Padilla.
 
        Mbali na Askofu Padilla, pia alikuwapo mwenyeji wake Askofu Josephat Lebulu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha na waumini zaidi ya 2,000.
 
       Wakati mgeni rasmi akitoka nje ya Kanisa akijiandaa kukata utepe kama ishara ya uzinduzi, mtu alirusha kitu chenye ukubwa wa ngumi, kwenda eneo lenye mkusanyiko wa watu na baada ya kutua, kulitokea kishindo na mlipuko mkubwa uliosababisha taharuki miongoni mwa waumini na kusababisha watu kukimbia ovyo.
 
          Katika tukio hilo, watu wawili walifariki dunia, akiwamo Regina Kurusei (45), mkazi wa Olasiti aliyefariki dunia siku ya tukio wakati akipewa matibabu katika hospitali ya Mount Meru na majeruhi mwingine James Gabriel (16) alifariki dunia usiku wa kuamkia Mei 6.
 
             Bomu hilo lililipuka Juni 15, katika Uwanja wa Soweto wakati wanachama na wapenzi wa Chadema wakiwa wamekusanyika kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani mkoani humo.
 
              Mlipuaji alilipua bomu hilo dakika chache kabla ya Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, kumaliza kuhutubia mkutano huo na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi kisha kuacha maswali mengi.
 
               Mulongo alitaja waliopoteza maisha kuwa ni Judith Mushi (46) ambaye alikuwa Katibu Kata wa Chadema, Kata ya Sokoni One na mkazi wa eneo hilo aliyemtaja kwa jina moja la Justine (16) wa Sombetini ambaye alifariki dunia katika hospitali ya mkoa ya Mount Meru.
 
                Siasa Akizungumza katika mkutano huo wa kukaribisha wawekezaji jana, Mulongo alisisitiza Serikali inahitaji siasa zenye tija na anapotokea mwanasiasa mwenye kupinga maendeleo, atashughulikiwa.
 
“Kila mwanasiasa awe wa kuchaguliwa au kuteuliwa, aliposimama kuomba nafasi hiyo wote waliahidi maendeleo kwa wananchi, hivyo tufanye hivyo,” alisema.
 
        Mulongo alisisitiza kuwa kutokana na umakini wa vyombo vya usalama, wanaomba wawekezaji wasiwe na hofu, wajitokeze kuwekeza maeneo ya mkoani hapo, bila hofu.
 
          Alisema mkoa huo unatangaza fursa za uwekezaji kwa sababu ya kuongeza kipato na ajira kwa wakazi wa Jiji hilo pamoja na kupanua wigo wa masoko na bidhaa zinazozalishwa hapa.

-Habari leo

No comments: