Thursday, November 14, 2013

TAMKO LA WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII MHE. DKT. HUSSEIN A. MWINYI (Mb) LA SIKU YA KISUKARI DUNIANI, TAREHE 14 NOVEMBA 2013



WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII MHE. DKT. HUSSEIN A. MWINYI
                        JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA


WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII

            TAMKO LA WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII MHE. DKT. HUSSEIN A. MWINYI (Mb) LA SIKU YA KISUKARI DUNIANI, TAREHE 14 NOVEMBA 2013

       Ndugu Wananchi,
endelea hapa


Siku ya kisukari Duniani, huadhimishwa duniani kote kila mwaka tarehe 14 ya Mwezi Novemba.
Kaulimbiu  ya  Maadhimisho ya  Siku ya  kisukari Duniani mwaka 2013 ni“Linda Maisha yajayo dhidi ya ugonjwa wa Kisukari”   Kauli mbiu hii inalenga kuhamasisha jamii juu ya matatizo mbalimbali yanayotokana na ugonjwa wa kisukari katika jamii.

Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani inaadhimisha siku hii, kwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kushirikiana na Chama cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania  kutoa elimu ya umuhimu wa kuzuia na kujikinga na madhara mbalimbali yatokanayo na ugonjwa wa kisukari.

Ndugu Wananchi,
Ugonjwa wa Kisukari ni hali ambayo hutokea wakati sukari katika damu inapokuwa nyingi kupita kiwango cha kawaida kwa muda mrefu. Sukari hutumiwa na mwili ili kupata nishati lishe. Ili mwili uweze kutumia sukari inayotokana na vyakula, unahitaji kichocheo cha insulin. Insulin husaidia sukari kuingia kwenye chembechembe hai ili kutengeneza nishati lishe. Ugonjwa wa kisukari unasababishwa na kichocheo hiki kupungua au kutofanya kazi kama inavyotakiwa, hivyo kiwango cha kisukari kinabaki kikubwa kwenye damu kwa sababu sukari haikuwezeshwa kuingia kwenye chembechembe hai za mwili


Ndugu Wananchi,
Tafiti za ugonjwa wa kisukari zinaonyesha kuwa mwaka 2007 kulikuwa na wagonjwa 246 milioni duniani. Ttakwimu za mwaka 2012 zinaonyesha kuwa kulikuwa na wagonjwa 371 milioni ulimwenguni kote, ambapo nusu ya wagonjwa hawa walikuwa hawajaanza matibabu. Asilimia 80 ya wagonjwa wote wa kisukari ulimwenguni wanaishi katika nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania.
Utafiti uliofanyika mwaka 2012 na kuhusisha wilaya 50 nchini Tanzania ulionyesha ya kuwa asilimia 9.1 ya Watanzania wenye umri wa miaka 25 na kuendelea wana ugonjwa wa kisukari.
Katika nchi 10 zinazoongoza kwa kisukari barani Afrika Tanzania inashika nafasi ya 8.




Ndugu Wananchi,
Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya kisukari duniani kwa mwaka 2013, inalenga kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu kinga dhidi ya ugonjwa wa kisukari pamoja na kubainisha mambo ambayo yanaongeza uwezekano wa kupata maradhi yasiyo ya kuambukiza ikiwemo kisukari. Magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza yanayoendana na kisukari ni pamoja na magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, saratani na magonjwa sugu ya njia ya hewa.
Mambo yanayoongeza uwezekano wa kupata magonjwa haya yasiyo ya kuambukiza ni pamoja na ulaji usiofaa hasa matumizi ya chumvi kwa wingi, mafuta na sukari, uzito uliozidi, unene uliokithiri, kutofanya mazoezi, uvutaji wa sigara na bidhaa zitokanazo na tumbaku, unywaji pombe kupita kiasi na msongo wa mawazo.

Ndugu Wananchi,
Ulaji usiofaa  ni kula chakula bila kuzingatia aina na kiasi kulingana na mahitaji ya mwili. Hii huweza kusababisha kupungua au kuzidi kwa virutubishi mwilini. Ulaji usiofaa ni pamoja na kula vyakula vyenye mafuta mengi hasa yale yatokanayo na wanyama, kula vyakula vyenye chumvi nyingi, sukari nyingi, kula chakula kupita kiasi, kukoboa nafaka na kutokula mbogamboga na matunda kiasi cha kutosha. .
Kutofanya Mazoezi ya mwili chakula kinacholiwa kwa kawaida hutumika na mwili kufanya kazi mbalimbali. Iwapo chakula hakitatumika hubadilishwa na kuhifadhiwa mwilini kama mafuta na hatimaye husababisha uzito kuzidi. Mambo yanayochangia mwili kutotumia chakula kilicholiwa ni pamoja na kukaa muda mrefu bila kufanya mazoezi ya mwili, kwa mfano : kuketi ofisini, darasani, kukaa na kuangalia runinga kwa muda mrefu, kutumia lifti kwenda ghorofani badala ya ngazi, kupanda gari mahali pa umbali mfupi badala ya kutembea kwa miguu, na kutoshiriki katika michezo.
Uzito na unene uliozidi uzito unakuwa umezidi pale ambapo uzito wa mtu unakuwa asilimia 20 zaidi ya uzito unaotakiwa. Ili kupima hali hiyo viashiria mbalimbali hutumika; njia inayotumika mara nyingi ni ile ya uwiano wa uzito na urefu wa mwili kulingana na viwango maalumu vilivyowekwa.
Msongo wa mawazo huweza kusababisha ulaji usiofaa na huweza kufanya mifumo mbalimbali ya mwili kutofanya kazi vizuri.
Matumizi ya pombe huchangia katika kuongeza uzito mara nyingi. Unywaji wa pombe za aina zote huendana na ulaji wa vyakula kwa wingi ambayo huchangia kuongeza uzito. Pombe yenyewe ikizidi inaweza kuharibu maini, kusababisha utapiamlo kwa wale wanaoishia kunywa pombe zaidi ya kula chakula.
Uvutaji wa Sigara na matumizi ya bidhaa zitokanazo na Tumbaku  licha ya kuwa ni matumizi yasiyo na tija, tumbako husababisha madhara mengi mwilini yakiwemo magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, saratani na magonjwa sugu ya njia ya hewa.



Ndugu Wananchi,
Ili kuzuia ugonjwa wa kisukari na maradhi mengine yasiyo ya  kuambukiza ni muhimu kufuata kanuni za afya ambazo ni ulaji bora, na mtindo bora wa maisha ambao ukifuatwa vyema huweza kwa kiasi kikubwa kuzuia mtu kupata kisukari au kwa mtu ambaye tayari ana ugonjwa wa kisukari hupunguza uwezekano wa kupata madhara makubwa ya kiafya.

Ndugu Wananchi,
Serikali inaendelea na utekelezaji wa Sera ya Afya (2007) ambayo inalenga kutoa huduma kwa magonjwa yasiyo ya  kuambukiza ikiwemo kisukari kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani ya nchi na wa kimataifa. Aidha, serikali, sekta binafsi, mashirika ya kimataifa na taasisi zinazotoa huduma bila faida zinaendelea kuandaa na kurekebisha sheria, kanuni na taratibu zinazoimarisha uzuiaji na udhibiti wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inatumia  maadhimisho   haya kuwa sehemu ya uhamasishaji kwa jamii kama ilivyo kwenye nchi zote duniani. 

Ndugu Wananchi,
Serikali inaeendelea kuandaa miongozo na mikakati ya kisera kwa kushirikisha jamii katika kudhibiti magonjwa  yasiyo ya kuambukiza, ikiwemo kisukari.

Serikali imeimarisha ushiriki wa sekta mbalimbali za umma na za binafsi katika kukabiliana na vyanzo vinavyosababisha magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Ndugu wananchi,
Kwa kutambua gharama za kutibu ugonjwa wa kisukari, kuanzia mwaka 1993, serikali ilitoa msamaha kwa wagonjwa wote wa kisukari kutochangia gharama za matibabu na inajitahidi kwa uwezo wa bajeti yetu pamoja na wahisani wetu kuhakikisha kuwa dawa muhimu zinapatikana. Kwa sasa watoto wote na vijana chini ya miaka ishirini na miwili walio na kisukari wanapata mahitaji yao yote kupitia kliniki za kisukari zilizopo nchini.
Kuanzia mwaka 2012, serikali pamoja na washirika wake inatekeleza mpango wa kuthibiti ugonjwa wa kisukari nchini. Lengo ni kuwa na kliniki hizo hadi katika hospitali za wilaya kwa sasa zipo kliniki za kisukari kwenye ngazi za mikoa na kuwapatia wananchi elimu ya ugonjwa wa kisukari ili waweze kushiriki kikamilifu kwenye kinga na tiba ya magonjwa haya.
Tanzania inaungana na mataifa yote duniani kutekeleza azimio la Umoja wa Mataifa la mwaka 2011 la kuhakikisha ya kuwa kuna mpango kabambe wa kuthibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Nchi yetu inaungana na mataifa mengine kuhakikisha ya kuwa  magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanapungua kwa asilimia 25 ifikapo mwaka 2025. Sasaunaandaliwa mpango huo  kwa kukishirikiana na wadau wengine wahusika.

Ndugu wananchi,
Kama nilivyosema mwanzoni, wengi wetu hawajitambui ya kuwa wana ugonjwa huu. Wengine wanakuwa na dalili lakini hawachukui hatua mapema. Dalili za kisukari ni rahisi kuzitambua nazo ni: kiu isiyoisha, kukojoa mara kwa mara, kupungua uzito, kusikia njaa kila wakati na mwili kukosa nguvu. Ukiwa na dalili hizi nenda hospitali ukapime sukari.
Ndugu wananchi,
Kwa bahati mbaya, unaweza kuwa na ugonjwa huu kwa muda mrefu bila kuwa na dalili nilizotaja hapo awali. Hata hivyo, jinsi sukari inavyokuwa juu, inaharibu mishipa ya damu na ya fahamu, macho, figo na kusababisha upofu, moyo na figo kushindwa kufanya kazi, na miguu kufa ganzi, kuwa na vidonda.
 Hivyo ninatoa wito  kwa kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa anapima afya yake kwa kuwa ugonjwa huu unaweza usionyeshe dalili yoyote mapema. Ni vyema kila mmoja akapima afya yake mara kwa mara ili kutambua hali yake ya afya. Endapo utatambuliwa kuwa una ugonjwa wa kisukari tumia huduma za afya kulingana na ushauri utakaopewa na wataalam wa afya.
Kwa wale ambao  wameshajitambua kuwa na matatizo ya kisukari lakini hawatumii huduma za afya ipasavyo, nawaasa watumie huduma za afya zilizopo kwa manufaa ya afya zao na kuepusha athari zinazotokana na ugonjwa ya kisukari.

                      ASANTENI  KWA KUNISIKILIZA

No comments: