Wednesday, November 13, 2013

MWAKYEMBE AENDELEA KUWA MBOGO,SOMA ALICHOKIFANYA HUKO TAZARA



Na Karoli Vinsent
          
          WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ameingia katika mzani wa kupimwa ubavu na uongozi wa Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA) ambao unasuasua kutekeleza agizo lake la kumtaka Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Ronald Phiri, kutoendelea kuishi hotelini na badala yake apewe nyumba ya kuishi ili kukwepa gharama pamoja na ufisadi.
 ENDELEA HAPA-----


          Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, Ronald Phiri, kwa takriban miezi 6 sasa anatajwa kuishi katika Hoteli ya New Afrika jijini Dar es Salaam kwa gharama ya shirika hilo na hivyo kuteketeza mamilioni ya shilingi.

          Habari zilizopatikana kutoka Ofisi za Makao Makuu ya TAZARA, Dar es Salaam, zinadai kwamba phiri amekuwa akilipia chumba anachokitumia kulala katika hoteli hiyo dola za Marekani 200 (takriban Sh 320,000) kwa siku, sawa na takriban Sh. 9,600,000 kwa mwezi. Kwa hesabu hiyo, kwa miezi hiyo sita ambayo Khiri ameishi hotelini hapo, TAZARA italipa Sh. 57,600,000.

            Hasara yote hiyo kwa shirika la TAZARA inaingiwa wakati Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe amemwagiza Kaimu Mkurugenzi huyo kuhamia katika nyumba ya TAZARA iliyoko Masaki, ambayo ilikuwa ikitumiwa na mtangulizi wake, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Akashambatwa Lewanika.

          Lewanika alistaafu ajira yake mwanzoni mwa mwaka huu na kurejea nchini kwao Zambia, kabla ya Bodi ya TAZARA kumteua Khiri kukaimu nafasi hiyo.

          Akizungumza na wafanyakazi wa TAZARA Oktoba 21, mwaka huu, Dk Mwakyembe alimpa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji huyo, Khiri, muda wa wiki mbili kuondoka hotelini hapo na kuhamia katika nyumba ya shirika.

           Mmoja wa wafanyakazi wa TAZARA ambaye hakutaka jina lake litajwe ameliambia kwenye Blogs hii akisema: “Unajua mpango wa kumweka hotelini (Phiri) ulikuwa ni wa muda wa miezi mitatu tu, lakini kama ujuavyo gharama za kuishi hotelini pale ni dola za Marekani 200 kwa siku.

         Kwa hiyo, miezi mitatu imepita na sasa ni miezi zaidi ya sita.”
Akizungumzia hali hiyo ya kuendelea kuishi hotelini hapo kinyume cha maelekezo ya Waziri Mwakyembe, Kaimu Mkurugenzi huyo wa TAZARA anasema hata yeye hajisikii raha kuishi hoteli hiyo ya New Africa, akisema hali hiyo inamsababishia kuishi mbali na familia yake.

         Khiri anasema: “Ni kweli niliambiwa niondoke hotelini hapa na waziri, lakini mpaka sasa sijaondoka. Hata hivyo, hata mimi mwenyewe sijisikii furaha kuishi hapa hotelini kwa sababu inanifanya niishi mbali na familia yangu.

        “Bodi ya TAZARA ilitakiwa ikutane mwezi Juni kwa ajili ya kujadili suala langu. Lakini Mkurugenzi aliyekuwa akiishi katika nyumba ninayotakiwa nihamie, bado hajaondoa samani zake, kwa hiyo ninachosubiri ni kikao cha bodi kujadili hatima yangu.”

         Kwa upande wake, Mwanasheria wa TAZARA, Marko Mabala, alipo ulizwa alisema: “Hili suala lina mitazamo ya kisiasa na kiutendaji.
Dk Mwakyembe alitoa agizo aondoke hotelini, lakini nyumba anayotakiwa kuhamia bado inashikiliwa na mkurugenzi aliyeondoka na hata funguo ameondoka nazo Zambia.
“Kwa hiyo, ile nyumba imefungwa. Nilimwandikia notisi, akasema hahitaji notisi, bali atakuwa tayari kuachia funguo za nyumba baada ya kulipwa mafao yake yote.
“Pamoja na Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TAZARA aliyeondoka kushikilia msimamo wake huo bado, upande wa Serikali ya Zambia unahoji ni kwa vipi shinikizo la kuachia nyumba liwe kwa Akashambatwa pekee, ilihali aliyekuwa 

         Naibu Mkurugenzi wake, Ayoub Ritti anaishi nyumba ya TAZARA iliyoko maeneo ya Kawe kwa muda wa miaka 15 sasa wakati si mfanyakazi wa TAZARA na halipii pango la nyumba hiyo.
“Naulizwa maswali (Mabala), kwa nini unasema Akashambatwa aondoke wakati hujamlipa haki zake zote, huku Ritti ambaye si mfanyakazi wa 

          TAZARA akiendelea kuishi katika nyumba za shirika wakati halipii pango?”
Ritti alikuwa mfanyakazi wa TAZARA, lakini alifutwa utumishi wa shirika hilo tangu mwaka 1998 na hadi sasa hajaondoka katika nyumba aliyokuwa akiishi na familia yake wakati alipokuwa Naibu Mkurugenzi.

       Habari zinasema wengine wanaoidai TAZARA, ni pamoja na Damas Ndumbaro, aliyekuwa Naibu Mkurugenzi huku Akashashamtwa ambaye kwa taarifa zilizopo ndani ya shirika hilo, anadai dola za Marekani 108,000.
Habari hii imeandikwa na Karoli Vinsent kwa kushirikiana n Gazet la Raia Mwema

No comments: