Tuesday, February 4, 2014

SAKATA LA MAWAZIRI MIZIGO,MBOWE AMJIBU JK,SOMA ALICHOKISEMA HAPA.



        MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), FreemanMbowe amemjibu Rais Jakaya Kikwete kwamba asiingize utani katika masuala mazito ya taifa
  Mbowe alisema Katiba ya Tanzania, itaamuriwa na wananchi wenyewe na si Chama Cha Mapinduzi (CM) ambacho kimekuwa na mkakati mkali wa kutaka kuua maoni ya wananchi.Mbowe ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja tu baada ya Rais Kikwete kudai amesikia kiongozi huyo wa upinzani akitangaza kutumia nguvu kupata Katiba mpya.
ENDELEA HAPO-------


     Rais Kikwete alitoa kauli hiyo juzi kwenye uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya, wakati akihutubia sherehe za miaka 37 ya kuzaliwa CCM. Alisema amesikitishwa na kauli hiyo na kuwataka Watanzania kutobabaishwa.


    Kikwete alisema Katiba mpya itapatikana kwa hoja za kila upande kulingana na mapendekezo yake.

      Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Mbowe alisema Rais Kikwete hapaswi kuchukulia utani katika mambo mazito ya taifa.

“Namuomba Rais Kikwete asichukulie utani mambo ya taifa suala la Katiba mpya. Anapaswa kuzungumza mambo ya msingi ambayo yanaleta tija.

“Siku zote Katiba ya nchi inapatikana kwa dhamira nzuri lakini tumebaini wenzetu hawa CCM hawaheshimu hoja za wananchi.

“Hebu tujiulize jinsi Jaji Joseph Warioba alivyotumia fedha nyingi kukusanya maoni ya Watanzania, leo CCM hao hao wanayakataa tuwaeleweje?” alihoji Mbowe.

Alisema Jaji Warioba ametoa hoja za msingi lakini kwa sababu ya uoga wa CCM wanataka kupindisha ukweli wa mambo.

“Mzee wa watu huyu amezunguka taifa zima kwa fedha za walipa kodi wa nchi hii, sasa wanataka watumie wabunge wao kukwamisha mchakato huu,”alisema Mbowe.

Alisema kama utawala wa Rais Kikwete utashindwa kuleta Katiba mpya ambayo inakidhi matakwa ya Watanzania, wao wataendelea kudai utawala mpya utakapoingia madarakani uwe ni wa Chadema au CCM.

“Nawahakikisha Watanzania, ikija Katiba mbaya tutaendelea kuidai kwa nguvu zote iwe CCM imeingia madarakani au sisi, Kikwete awe madarakani au asiwepo hatulali kamwe.

“Katiba ni maridhiano ambayo yanabeba maoni ya Watanzania sasa kwa nini CCM hawataki kuyafuata?” alihoji Mbowe.

Alisema CCM haina hatimiliki ya Katiba mpya na kwamba wakati wa kufanya uamuzi mgumu wa kupindisha maoni ya Watanzania umefika.

“Hawa watu hawana hatimiliki ya Katiba mpya, kwa nini wanajawa uoga kiasi hiki? Wanaogopa serikali tatu, nakwambia sitaki utani kwenye ya msingi,”alisema Mbowe.


               NJE YA BUNGE

         Mbowe alisema atahakikisha wanajadiliana vya kutosha ndani ya Bunge kuona haki inatendeka.

         “Tutabishana kwa kila namna ndani ya Bunge,wakituzidi kete kwa rafu zao bungeni tutarudi kwa wananchi kuwashitaki maana hawa ndiyo walengwa… hatutaki kufika huko kama kila mtu ataweka busara zake chini.

       “Dhamira ya CCM ndiyo inatufanya tutoe kauli hizi lakini nakwambia hapa hakuna mcheza ngumi… hoja ndiyo jambo la msingi tu,tutatumia maandamano nchi nzima maana haya ni haki ya msingi ya kila mtu,”alisema Mbowe.


Chanzo - Mtanzania

No comments: