Sunday, April 20, 2014

HII NDIO KAULI YA JAJI WEREMA KUHUSU RAISI KUWATIMUA UKAWA NA KUTEUA WENGINE



Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema (kulia) akijibu maswali ya waandishi wa magazeti ya Mwananchi Communications Limited nje ya Ukumbi wa Bunge Maalumu la Katiba, mjini Dodoma.

                                                     Kwa ufupi
Jaji Werema alisema Sheria namba 8 ya Mabadiliko ya Katiba ya 2011, ipo kimya kuhusu suala hilo na kwamba kwa maana hiyo Rais hana mamlaka ya kutengua hata ubunge wa wale aliowateua kupitia kundi la wajumbe 201.


Dodoma. Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema amesema Rais Jakaya Kikwete hana uwezo kisheria wa kuwafukuza au kutengua uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.

     Jaji Werema alisema Sheria namba 8 ya Mabadiliko ya Katiba ya 2011, ipo kimya kuhusu suala hilo na kwamba kwa maana hiyo Rais hana mamlaka ya kutengua hata ubunge wa wale aliowateua kupitia kundi la wajumbe 201.

     “Umesoma Sheria ya Mabadiliko ya Katiba? Kaisome maana ili mtu afukuzwe ubunge lazima apungukiwe sifa za nafasi hiyo, lakini kama sheria iko kimya maana yake ni kwamba hana (Rais) uwezo wa kuwafukuza,” alisema Jaji Werema.

        Jaji Werema alikuwa akijibu maswali ya gazeti hili kuhusu hatima ya wajumbe ambao ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao Jumatano jioni waliondoka bungeni kwa madai ya kutoridhishwa na uendeshaji wa Bunge Maalumu.

          Wajumbe waliotoka nje ni wanaotokana na vyama vya CUF, Chadema, NCCR Mageuzi, NRA, NLD na baadhi kutoka kundi la 201. Alhamisi asubuhi, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta alisema utafiti uliofanywa na ofisi yake ulibaini kuwa katika kundi la 201, ni wajumbe 25 tu ambao walitoka nje pamoja na Ukawa.

       Baada ya wajumbe hao kutoka nje, Mjumbe wa Bunge hilo, Mwigulu Nchemba ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, aliomba mwongozo akihoji iwapo Ofisi ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu haiwezi kumwandikia Rais Kikwete ili ateungue uteuzi wa wajumbe katika kundi la 201 ambao waliungana na Ukawa kususia vikao.

    “Ningependa Rais atengue hadhi zao ili kuingiza watu wengine ambao wako tayari kufanya kazi hata bure, sisi tunalipwa fedha nyingi, lakini tunaleta mzaha, watu hawana maji, dawa, madawati, ada za elimu ya juu watu wamekosa, hizi fedha zingetumika huko,” alisema Nchemba mwenye wadhifa mwingine wa Naibu Waziri wa Fedha.

                                              Matakwa ya Sheria
Jaji Werema alisema: “Ili mtu aondolewe katika nafasi yake ni lazima akose sifa za kuwa mjumbe, mathalan kuugua ugonjwa wa akili au kichaa, kuumwa muda mrefu kiasi cha kushindwa kutimiza majukumu yake na kadhalika, lakini sifa hizo kama hazipo kwenye sheria sasa unaanzia wapi?”

           Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya 2011 pamoja na marekebisho yake ya 2012 na 2013 inawataja Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuwa Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kwa mujibu wa nafasi zao.

     Kadhalika sheria hiyo inampa Rais mamlaka ya kufanya uteuzi wa wajumbe 201 kutoka makundi mbalimbali, lakini haitaji sifa wanazopaswa kuwa nazo wajumbe hao.

           Jaji Werema alisema hata kama sheria ingekuwa inaruhusu kufukuzwa au kusitishwa kwa ujumbe wa wabunge hao, hakuna sababu ya msingi ya kuwachukulia hatua hiyo.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: