MIAKA 50 YA MUUNGANO,HAYA NDIYO MANENO YA ZITTO KABWE JUU YA MUSTAKABALI WA MUUNGANO WETU

      Muungano miaka 50 ya Matumaini, Malalamiko, Hofu na Mabadiliko

         Haikutarajiwa na mataifa mengi kuwa Tanzania itafika miaka 50 ikiwa moja na Jamhuri ya Muungano. Mataifa ya aina ya Tanzania kama Muungano wa Senegal na Gambia, British Somalia na Italian Somalia yalivunjika ama kwa sababu za kutoaminiana au kwa sababu za ukosefu wa demokrasia na vurugu. 


          Nchi iliyobakia na Muungano kama Tanzania ni Jamhuri ya Muungano wa Kameruni ambayo baadaye ilijiita Jamhuri ya Kameruni. Kama ilivyo Tanzania, Kameruni nayo ina watu wanaotaka mabadiliko na hata kutaka British Cameron ijitenge na kuwa Nchi huru.
 

        Mwaka 1964 ulikuwa wa matumaini makubwa sana kwa Afrika baada ya ndoto za wana umajumui wa Afrika kuonekana kutimia kwa kuunganisha mataifa mawili huru Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika. Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Karume walikubaliana kwa niaba ya wananchi wa nchi zao kuunda nchi moja inayoitwa Tanzania.

             Leo miaka hamsini imetimia na watu wanaoishi katika eneo hili la jiografia zaidi ya asilimia 80 walizaliwa Tanzania. Hata hivyo matumaini makubwa ya kujenga Taifa moja imara kutoka mataifa mawili yamekuwa yakififia mwaka hata mwaka. Hii inatokana na kurundikana kwa kero mbalimbali za Muungano ambazo kutotatuliwa kwake kunaleta hisia za upande mmoja wa Muungano kufaidika zaidi kuliko upande mwingine
 

             Mwaka 1984 kulikuwa na kilichoitwa kuchafuka kwa hali ya kisiasa Zanzibar baada ya Makamu wa Rais wa Muungano Alhaj Aboud Jumbe kutaka mabadiliko kwenye muundo wa Muungano. Hii ilikuwa ni nafasi adhimu kwa chama tawala CCM kufanya mabadiliko na kuongoza mabadiliko hayo. 
           Hata hivyo hoja ya mabadiliko hayo ndani ya vikao vya chama haikujadiliwa na hatimaye Makamu wa Rais na Rais wa Zanzibar kuondolewa kwenye nafasi zake zote kwa kulazimishwa kujiuzulu na baadaye kuwekwa kizuizini. 

         Aboud Jumbe mwenyewe aliandika kuhusu miaka 30 ya Muungano kama miaka ya dhoruba katika Muungano. Maandiko yake ya mwaka 1994 Leo yanarejewa na watu ambao hata hapo mwanzo walimwona Jumbe kama msaliti tu.

             Inawezekana kabisa historia ikamsafisha Aboud Jumbe kwa msimamo wake wa kutaka muungano wa Serikali Tatu. Hata hivyo suala kama ataona Serikali tatu ndani ya uhai wake ni suala ambalo lina wingu zito. 

         Miaka hii ya dhoruba ni miaka ya malalamiko kutoka pande za Muungano na hasa upande wa Zanzibar. Kuongezeka kwa mambo ya muungano kumeendelea kuminya uhuru wa Zanzibar katika kujiamulia mambo yake na hasa masuala ya kiuchumi na hivyo kudumaza maendeleo ya kiuchumi ya visiwa hivyo. 
            Malalamiko haya yameleteleza kufikiwa kwa mapendekezo kubadili muundo wa Muungano kuwa muungano wa Serikali tatu. Baadhi ya hatua zilizochukuliwa na upande wa Zanzibar kujibu malalamiko haya zimeleta hofu.
 

           Hofu za kuvunjika kwa Muungano kunatokana na hatua za Zanzibar kubadili katiba yake na kuitambulisha Zanzibar kama nchi. Kitendo cha kuwa na nchi mbili kimeleta ukakasi kwa upande wa wananchi wa Tanganyika na hivyo kupelekea nao kutaka 'nchi yao'. 
          Kuna hofu kubwa kwamba iwapo Tanganyika itakuwa nchi nayo basi uwezekano wa Muungano kuendelea kuwepo utakuwa mdogo sana. Wenye hofu hii wanataka muundo wa sasa wa Muungano kuendelezwa. Swali la msingi ni je, hofu hii haiwezi kujibiwa ndani ya muundo Mpya wa serikali tatu?
 

          Miaka hamsini ya muungano imefika wakati kuna mjadala mkubwa ulioligawa Taifa kuhusu Muungano wenyewe. Ni mwaka wa mabadiliko kwani hata huo Muungano wa Serikali mbili hauwezi kubakia ulivyo sasa katika katiba Mpya iwapo itapita. 

       Kura ya maoni iliyoendeshwa na Shirika la Twaweza inaonyesha kuwa wananchi wa Zanzibar wanapoulizwa kama wanakubali serikali tatu, asilimia themanini wanaunga mkono. Wananchi wa bara ni asilimia 46 tu wanaunga mkono. 

          Wananchi hawa wakipewa uchaguzi wa miundo kadhaa ya Muungano, uungwaji mkono wa Serikali tatu kwa Zanzibar unaporomoka mpaka asilimia 46 kwa Zanzibar na asilimia 26 kwa Tanganyika. Hata hivyo iwapo watatakiwa kuchagua rasimu ya katiba asilimia 65 ya watanzania wataikubali. 
       Rasimu inataka Serikali tatu. Hii inaonyesha dhahiri namna gani wananchi wenyewe wamechanganyikiwa kuhusu Muungano wa Tanzania. Hivyo kazi kubwa ya kisiasa inatakiwa ili kujenga mwafaka wa kitaifa kuhusu muungano.
 

           Tume ya Marekebisho ya Katiba inasema tatizo la msingi la Muungano ni muundo wake. Baada ya miaka hamsini watu wachache sana wanataka Muungano kuvunjika. Hivyo tunaweza kushughulika na Muundo wa Muungano kwa amani kabisa bila wasiwasi kwani uungwaji mkono wa Muungano ni mkubwa sana. Baada ya malalamiko na hofu, turejeshe matumaini kwa kufanya mabadiliko makubwa ya Muungano wa Tanzania ili watoto na wajukuu zetu washerehekee miaka Mia Moja ya Muungano. 

       Ni mabadiliko tu ndio yanaweza kuendeleza lulu hii Muungano.

About HABARI24 TV

Post a Comment
Powered by Blogger.