Wednesday, April 23, 2014

WAKATI KATIBA IKIWA KITENDAWILI---HUU NDIO UTAFITI WA TWAWEZA KWA WANANCHI.



UTAFITI WA TWAWEZA: ---Taasisi ya TWAWEZA imefanya utafiti kuhusiana na Rasimu ya Katiba inayojadiliwa bungeni hivi sasa na taarifa yao wameitoa Jumatano hii...

       Sehemu ya muhtasari wao inasema hivi kama nilivyoinukuu kwenye Taarifa ya TWAWEZA kwa Vyombo vya Habari: ----
      Sauti za Wananchi imebaini kuwa, uungwaji mkono ni mkubwa sana miongoni mwa wananchi wa Tanzania Bara kwenye vifungu vingi vilivyowasilishwa katika rasimu ya kwanza ya katiba na vimebaki katika rasimu ya pili.


       Vifungu hivyo ni vile vinavyohusu kuwepo kwa uwajibikaji zaidi kwa watumishi wa umma, kuimarisha utaratibu wa dola ili kudhibiti na kuwajibisha wabunge, hasa wabunge kuwajibika kwa wapiga kura wao, na kuongeza ushindani zaidi wa kisiasa. Utafiti pia unaonesha kuwa Watanzania wangeipitisha rasimu ya katiba bila shida ikiwa Watanzania sita kati ya kumi wameonesha kuwa wangeipigia kura ya Ndiyo.

        Tanzania Bara ni wananchi asilimia 65 na Zanzibar ni wananchi asilimia 62 wanaoikubali rasimu ya sasa. Hata hivyo, suala la muundo wa serikali bado ni tata. Idadi kubwa ya Wazanzibari (80%) walisema wanataka muundo wa serikali tatu, ikilinganishwa na chini kidogo ya nusu (43%) ya wahojiwa kutoka Tanzania Bara.

        Aidha, zaidi ya nusu ya wahojiwa kutoka Zanzibar (53%) walisema kuwa uungaji mkono wa rasimu ya sasa ya katiba utategemea muundo wa serikali tatu. Sauti za Wananchi na Wasemavyo Wazanzibari pia ziligundua kuwa wananchi kutoka Tanzania Bara wamepata fursa kufuatilia midahalo na mijadala ya katiba mpya.

       Wananchi sita kati ya kumi (62%) kutoka Bara wamekuwa wakifuatilia kwenye radio, luninga au mijadala ya wazi, wakati wenzao wa Zanzibar, ni wananchi watatu tu kati ya kumi (30%) ndiyo wamefanya hivyo.

No comments: