Wednesday, April 23, 2014

HABARI ILIYOTIKISA JIJI---LHRC YABAINI UVUNJWAJI MKUBWA WA HAKI ZA BINADAMU,NI KATIKA REPORT YAO YA MWAKA JANA,IGP AKIRI WAZI KUWA UHALIFU UMEONGEZEKA KWA KIASI KIKUBWA, MADEREVA BODA BODA WATAJWA


Kamishna wa Polisi Isaya Mngulu

Na Karoli Vinsent
         
      INSPEKTA  Jenerali  wa  Polisi (IGP), Ernest  Mangu amesema kuwa, ongezeko  la  wananchi  kutokuheshimu sheria zilizopo limeongezeka katika miaka ya hivi karibuni, tofauti na zamani  kwani waendesha boda boda hivi sasa nao wamekuwa wakishiriki vitendo hivi viovu pindi ajali inapotokea barabarani.

         Akizungumza kwa niaba ya IGP, Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, Kamishna wa Polisi Isaya Mngulu, katika uzinduzi wa taarifa ya haki za binadamu ya mwaka jana ilioandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), alisema watu wamekuwa wakijichukulia sheria mkononi dhidi ya raia wenzao, jeshi la polisi, vituo vya polisi na mali nyingine za umma.


        Alisema, wananchi wamekuwa wakitoa uhai wa raia wenzao kwa tuhuma za uhalifu, mbaya zaidi hata walinzi wa raia na mali ambao ni jeshi la polisi, ambapo askari wake wamevamiwa na kuuawa, vituo vya polisi vine mwaka jana vimevamiwa na wananchi pia mali za umma na binafsi ziliharibiwa vibaya.

      “Kwa kweli hali hii haiwezi kuvumilika kuendelea kutokea katika nchi yetu. Nisihi jamii itambue umuhimu wa kuheshimu utawala wa sheria na kuamini vyombo vya usimamizi wa sheria,” alisema na kufafanua kuwa, kufanya vurugu na kushambulia raia wengine wakati vyombo vilivyowekwa kisheria vipo ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

       Pia alisema kuwa, haki ya kuishi ya raia walio wengi imekatishwa na ajali ambazo mara nyingine zingeweza kuepukika ingawa wahenga wanasema ajali haina kinga, ila barabara zikitumiwa vizuri ina kinga.

      Vile vile alisema kuwa, hivi sasa taifa liko kwenye mchakato wa kutunga katiba mpya, hivyo ni vyema ikatumiwa fursa hiyo ya kuandika katiba mpya kwa kuweka misingi madhubuti ya ulinzi wa haki zote za binadamu hasa zile za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni pamoja na zile za makundi maalum ambazo hazikulindwa na katiba ya sasa.

      Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Helen Kijo-Bisimba alisema kuwa, taarifa hiyo iliyozinduliwa ni ya kumi na moja tangu kuanzishwa kwa uandishi wa taarifa ya aina hiyo mwaka 2002.

       Alisema, taarifa hiyo inatoa maelezo ya kina ya mambo mengi yahusuyo haki za binadamu na hali ya kusuasua katika kuchukuliwa hatua stahiki lakini pia muelekeo wanchi katika kulinda na kusimamia haki zote za msingi.

       “Mfano tumetambua hatua zilizochukuliwa baada ya operesheni tokomeza ambapo kuna mawaziri waliowajibika na kuwajibishwa lakini tunapendekeza serikali isikomee hapo bali waliotekeleza operesheni hizi nje ya utaratibu wachukuliwe hatua katika ubinafsi wao na waathirika walipwe fidia za haki,” alisema.

      Alimalizia kuwa, katika mchakato wa kupata katiba mpya, wanawashawishi watanzania wote kuona umuhimu wa  kufuatilia mchakato hata kwa sasa ambapo unaonekana kutokwenda kama ilivyokuwa imetarajiwa.
“Katiba hii ni yetu na taifa hili ni letu tusipofuatilia ikija katiba mbovu waathirika wa kwanza ni sisi na ikija nzuri wanufaika ni sisi,” alisema


No comments: