Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kesho atatangaza Baraza Kivuli la Mawaziri.
“Nitalitangaza baraza langu jipya la mawaziri Alhamisi (kesho) baada tu
ya kukamilisha bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu,” alisema Mbowe jana mjini
Dodoma.
Alisema mawaziri hao wataanza kutekeleza majukumu yao katika Bajeti ya mwaka 2014/2015 kwa kusoma hotuba zao za bajeti.
Kujumuishwa kwa wabunge wa vyama vya CUF na Chadema ni matunda ya
kuundwa kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wakati wa Bunge la
Katiba.
Hivi karibuni, Mbowe alikaririwa na gazeti hili akisema hatua hiyo
imefikiwa baada ya “kila upande kukubali kuwa unamhitaji mwenzake katika
harakati za kuikomboa nchi hii.”
Ukawa ndiyo iliyowaongoza baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu kutoka nje
kususia mchakato wa Katiba Mpya kutokana na kile ilichodai kuwa ni
kutokuridhishwa na jinsi mambo yanavyokwenda.
Wakati huohuo; wabunge wamekubaliana kuwa shughuli za Bunge zitakuwa
zikianza saa 3:00 asubuhi na kusitishwa saa 7:00 mchana na kurejea tena
saa 10:00 alasiri hadi saa 2:00 usiku.
Ratiba hiyo itahusisha pia Ijumaa na Jumamosi.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah alisema utaratibu huo utaongeza nafasi za wabunge kuchangia katika Bunge la Bajeti.
Imeandikwa na Sharon Sauwa, Daniel Mjema na Edwin Mjwahuzi.CREDIT--MWANANCHI
No comments:
Post a Comment