Habari hii Imeandikwa na
Karoli Vinsent wa Mwandishi wa Mtandao huu na Kusaidiwa na Deodatus Balile
Mhariri wa Gazeti la Jamhuri
Siku za Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Bandari Tanzania, Mzee Madeni Kipande (58), kuendelea kuwa
madarakani zinazidi kuyoyoma baada ya Rais Jakaya Kikwete kukerwa na tabia yake
ya kutumia jina la Rais kuhalalisha matendo yake yenye kukiuka sheria za
utumishi wa umma.
Habari za uhakika kutoka Ikulu na
kwa baadhi ya mawaziri waandamizi, zinasema Rais Kikwete baada ya kupata
taarifa za Kipande kutumia vibaya jina lake, alichukia na kuamua kumwita Waziri
wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, na kumpa maagizo mazito.
“Tena wala haikuwa siri, Rais
alimwita Dk. Mwakyembe kama wiki mbili zilizopita mbele yetu mawaziri kama
wanne hivi akamfokea,” kimesema chanzo chetu. “Alimpa maagizo ya wazi kuwa
hafurahishwi na hataki jina lake litumiwe vibaya na Kipande kukandamizi watu
wengine.
“Alimtaka Dk. Mwakyembe kufuatilia
na kumpa taarifa juu ya utendaji wa kipande, na iwapo alidanganya kiwango cha
mapato kuwa kimeongezeka, unyanyasaji wa wafanyakazi, kukaidi maagizo ya Bodi
akidhani ana kinga ya Rais na kutamba kwenye corridor (viambaza) kuwa
hakuna anayemueza yeye ana mizizi mizito.
“Baada ya maagizo hayo, Dk.
Mwakyembe hakubisha, bali alimwambia Rais kuwa atatekeleza. Ninachokwambia hiki
wala hakitiliwi shaka, hata Mwakyembe mwenyewe hawezi kujitokeza akasema
hajaelekezwa, na iwapo hatatekeleza aliyoelekezwa na Rais basi ni wazi naye
atakuwa anakaidi maelekezo halali ya Mheshimiwa Rais sawa na Kipande
anavyokaidi maelekezo ya Bodi,” mmoja wa mawaziri waandamizi ameumbia Gazeti
moja la wiki ilinalofuatilia Sakata hilo, mwishoni mwa wiki.
Habari za uhakika kutoka Ikulu
zinasema baada ya gazeti hilo la wiki kuchapisha taarifa za unyanyasaji
anaofanya Kipande bandarini na vifo vya wafanyakazi watatu -- Peter
Gwamaka Kitangalala, Dotto Mbega na mwingine aliyefahamika kwa jina la
Oluwochi -- kuwa wamefariki dunia katika kipindi cha miezi mitatu kutokana na
shinikizo la damu lililozaa kiharusi baada ya vitisho vya Kipande, Rais Kikwete
amesikitika mno na kusema hilo halipaswi kutokea.
“Rais alisema mtu anapofika mahala
akasababisha kifo cha mtu, ama moja kwa moja au kwa njia yoyote, basi hiyo
haivumiliki,” amesema mfanyakazi wa Ikulu, akisisitiza kuwa vyombo vya dola
vinapaswa kuchunguza hali hiyo na ikibainika ni kweli hatua za kisheria
zichukuliwe dhidi ya waliosababisha vifo hivyo.
“Baada ya Mtawa na Shaaban Gurumo
kuona moto umewaka, wakaamua kuwaita wahariri wa gazeti linalomilikiwa na
kuhaririwa na wazawa wa Bagamoyo, kwa nia ile ile ya kuendeleza ukabila kama
mlivyoandika, akatumia gazeti linalohaririwa na mhariri anayetoka kijijini kwao
kuthibitisha tuhuma dhidi yake bila kujua,” kimesema chanzo chetu.
Katika gazeti hilo la wiki, chapisho
la Aprili 16 -22, 2014 Kipande hakukanusha tuhuma kuwa alimtukana Balozi wa
Japan, Masaki Okada, au kuwa alimdanganya Waziri wa Uchukuzi, Dk. Mwakyembe,
kwamba mapato ya Bandari yamefikia Sh bilioni 50.
Wiki mbili zilizopita, Madeni
Kipande amemtukana Balozi wa Japan nchini, Okada. Balozi Okada alikwenda
ofisini kwa Kipande kumweleza nia ya Japan kutoa msaada wa kukarabati gati Na.
1-7 kama msaada, lakini kinyume cha matarajio kwamba Kipande angepokea msaada huo,
aliishia kumrushia matusi Balozi wa Japan.
“Kwanza alikuwa amekataa kumuona huyo
Balozi, akisema aonane na wasaidizi wake, lakini Balozi aliposisitiza msaidizi
wa Kipande akamwambia protokali zinamtaka amuone, akakubali kumuona.
Kilichotokea baada ya hapo kilikuwa kituko. Balozi alimweleza kuwa anataka nchi
yake isaidie kukarabati gati Na. 1-7 la bandari. Kipande akamwambia Bandari
ilitangaza zabuni, na Japan kama ilikuwa inataka kufanya hivyo ilipaswa kuomba
zabuni na kuingia kwenye ushindani.
“Balozi alisisitiza kuwa nia yake
ni kutoa msaada si kufanya biashara, Kipande akasema huo ni uongo kwani amezoea
kauli za aina hiyo na ni ujanja wa kupenyeza rushwa na kuzipatia kazi kampuni
za Kijapani kwa njia za panya, hivyo yeye hatakubali kama Japan inataka kutoa
msaada wa ukarabati wa bandari basi isubiri zabuni ijayo.
“Kauli kwamba Japan inataka kutumia
mkondo wa ubalozi kwa njia ya rushwa kuzipatia kampuni za nchini kwake kazi
wakati nchi hiyo ililenga kutoa msaada ilimuuma mno Balozi, na taarifa zilizopo
anataka au tayari ameandika barua kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa kutaka ufafanuzi kwanini nchi yake ya Japan ihusishwe na rushwa kwa
kutaka kuisaidia Tanzania,” kimesema chanzo chetu.
Afisa Mwandamizi wa Wizara ya Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ameiambia Gazeti hilo la wiki
kuwa wizara yake inalishughulikia kwa nguvu suala hilo kunusuru uhusiano wa
Tanzania na Japan.
“Tanzania na Japan zimekuwa nchi
marafiki na taifa hili limekuwa msaada mkubwa kwetu. Leo kumtukana Balozi na
nchi yao ni utovu wa nidhamu wa hali ya juu. Tunalishughulikia hili na Kipande
ni lazima ataondolewa angalau kwa kosa hili linaloweza kuigharimu Tanzania
katika dunia ya diplomasia tusipochukua hatua,” amesema afisa huyo.
Kuhusiana na kifo cha Mbega, gazeti
hilo likimnukuu mtu waliyemwita mtaalamu au daktari wa binadamu, lilikiri
uwezekano wa kifo cha Mbega kutokana na shikizo la Kipande, liliposema: “Kwa
hili [la kifo cha Mbega] naweza kukubaliana na wewe kitaalamu, maana huyu
alikuwa ni mtu wa karibu na hazina ya Bandari na sasa fedha zimeibwa kwa
mamilioni, wewe ndiye uliyekuwa mlinzi wa lango la fedha sasa zimepotea, iwe
umeiba wewe au umeibiwa na hasa kama umeibiwa ni lazima uchanganyikiwe na hata
kupata shinikizo la damu linaloweza kukusababishia kifo,” mtaalamu alifafanua
kupitia gazeti hilo.
No comments:
Post a Comment