Mheshimiwa
Spika, Frank Herbert aliwahi kusema
“Utawala bora, kamwe hautegemei Sheria bali
sifa binafsi za wale wanaotawala. Vyombo vya Serikali mara zote vipo chini ya
wale wanaowaongoza. Kwa hiyo sifa muhimu ya Serikali ni namna ya
kuteua/kuchagua viongozi”
Serikali
ya awamu ya nne, imeshindwa kuwajenga viongozi wake katika misingi bora na ndio
maana pamoja na matatizo ya kimfumo, wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea
kubadilisha viongozi na matokeo ya ufanisi wake yamekua ni kioja na dhihaka
katika utendaji.
2.0
UTEKELEZAJI WA MAAZIMIO
16 YA BUNGE
Mheshimiwa
Spika, kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ilileta
Bungeni taarifa yake tarehe 20 Disemba 2013 liyowasilishwa na Mwenyekiti wake,
Mhe. James Lembeli kuhusu uchunguzi wa matatizo katika utekelezaji wa
Operesheni Tokomeza Ujangili, iliyokua na maazimio kumi na sita (16). Taarifa
hiyo ndiyo iliyomuondoa aliyekua Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis
Kagasheki na mawaziri wengine.
Mheshimiwa
Spika, mojawapo ya maazimio ya Bunge, yaliyoongezwa na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali ni pamoja kuundwa kwa Tume ya Uchunguzi wa Kimahakama. Aidha, ni
takribani miezi zaidi ya mitano kupita tangu Serikali iahidi Desemba mwaka
jana, kuahidi, kupitia kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuunda tume
maalumu ya kuchunguza kilichotokea wakati wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Katika makujukumu yake, Tume hiyo imepewa kazi zifuatazo;
a)
Kuchunguza na
kubaini Operesheni Tokomeza ilivyoendeshwa;
b)
Kuchunguza na
kubaini iwapo sheria, kanuni, taratibu na hadidu za rejea zilifuatwa na watu
waliotekeleza operesheni hiyo.
c)
Kuchunguza na kubaini
kama kuna mtu aliyekiuka sheria, taratibu na hadidu za rejea wakati wa
operesheni;
d)
Kuchunguza
na kubaini kama kuna watu ambao walikiuka sheria yoyote wakati wa utekelezaji
wa operesheni hiyo na kupima kama hatua zilizochukuliwa dhidi yao au mali zao
zilikuwa stahiki;
e)
Kupendekeza hatua
zozote zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya mtu ambaye itabainika alikiuka sheria,
taratibu na hadidu za rejea pamoja na kupendekeza mambo ya kuzingatiwa wakati
wa kuandaa na kutekeleza operesheni nyingine siku zijazo ili kuepuka kasoro.
Mheshimiwa
Spika, pamoja na kuundwa kwa Tume hii lakini Serikali haikupaswa tena kuipa
tume kazi mpya katika maeneo yote bali yale
yaliyohitaji ushahidi wa ziada wa kijinai, hii ni kwa sababu makosa
mengine yako wazi ambayo Serikali ilipaswa iwe imeshachukua hatua badala ya
kusingizia inasubiri taarifa ya tume. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, sasa
inaitaka Serikali iwasilishe taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge wakati
wa Majumuisho ya Bajeti ya Wizara ili maazimio ya Bunge hili yasiishie kabatini
kama ilivyokuwa kwa mengine ya miaka ya nyuma na ilivyozoeleka sasa.
2.1
Uwajibishwaji Wa
Watendaji Kutokana Na Maazimio Ya Bunge
Mheshimiwa
Spika, aidha katika azimio namba Saba (7), Bunge liliazimia pia kumwajibisha
Mkurugenzi wa Wanyamapori Prof. Alexander Songorwa kwa kutoa taarifa zisizo
sahihi kwenye vyombo vya habari na kuudanganya umma kuhusu mazingira na kifo
cha Emiliana Marrow wa Babati.
Mheshimiwa
Spika, katika hali ya kushangaza Waziri wa Maliasili na Utalii wa sasa, Mhe.
Lazaro Nyalandu ambaye akiwa katika nafasi yake ya unaibu waziri, kipindi kifupi tu kabla ya uteuzi wake, kwa
kasi ya ajabu aliandaa mikutano mingi na ziara mbalimbali huku akiandamana na
lundo la vyombo vya habari kama kumbikumbi,na kutoa matamko makali dhidi ya
ujangili na watumishi wasio waaminifu. Akiwa katika ziara hizo, aliwahi
kuikandia sana Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Ardhi na Maliasili iliyoongozwa na Mhe.
James Lembeli, huku akidai kuwa ilikuwa ya uwongo mtupu. Lakini baada ya
kubanwa zaidi, alikana kutoa kauli za kuikosoa ripoti hiyo ya kamati. Sababu za
kwanini akanushe maneno aliyoyasema zaidi ya mara nne, inabakia kuwa siri yake
mwenyewe.
Mheshimiwa
Spika, Waziri Nyalandu alitoa taarifa za kuwavua nyadhifa zao Mkurugenzi Mkuu
wa Wanyamapori na Mkurugenzi Msaidizi,
Idara ya Matumizi Endelevu ya Wanyamapori nyadhifa zao. Nyalandu anadai kuwa
moja ya sababu za kuwaondoa, ni kutekeleza maazimio ya Kamati ya Lembeli
kutokana na kutowajibika wakati wa Operesheni Tokomeza. Jambo la kujiuliza,
kama aliwahi kusema kuwa taarifa ya kamati ni uongo mtupu, je ni lini
amethibitisha kuwa kile alichodai kwamba ni uwongo, ulikuwa ukweli? Cha ajabu,
aliyeteuliwa kukaimu nafasi ya ukurugenzi, Paul Sarakikya aliyekuwa kiongozi wa
utekelezaji wa operesheni tokomeza na aliyehusika moja kwa moja na kinachodaiwa
kuwa uvunjifu wa haki za binadamu, ndiye amepewa nafasi ya kukaimu
ukurugenzi! Wote tunafahamu ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu na
ukatili uliofanywa katika operesheni tokomeza kiasi cha kusababisha mawaziri
wanne kuwajibishwa kwa kutenguliwa nafasi zao.
Mheshimiwa
Spika, aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza ilitumia vigezo
gani kumteua Sarakikya kukaimu nafasi ya Ukurugenzi wa Wanyamapori huku ikijua
alivyoshindwa kutokomeza ujangili hapa nchini na jinsi aliyoendesha operesheni
tokomeza ujangili iliyokuwa imejaa dhuluma, uporaji, utesaji na udhalilishaji
dhini ya wananchi. Jambo ambalo liliishangaza zaidi Kambi Rasmi ya Upinzani ni
kitendo cha Waziri Nyalandu kumteua Ndugu Sarakikya kukaimu nafasi ya
Mkurugenzi wa Wanyamapori huku akijua kuwa Sarakikya alifanya makosa mengi
katika utendaji wake wa kazi katika
idara hiyo ya Wanyamapori.
Mheshimiwa
Spika, ikumbukwe pia kuwa Ndg. Sarakikya ndiye aliyeongoza kikosi cha kuzuia
ujangili hata kabla ya operesheni tokomeza. Katika kipindi hicho, Tanzania
ilishika nafasi ya kwanza kati ya nchi nane duniani zilizoongoza kwa matukio ya
ujangili. Aidha, ili kuonyesha kwamba Serikali hii haizingatii weledi katika
utendaji, alietuliwa tena kusimamia Operesheni Tokomeza Ujangili.
2.2 Kauli Tata Za Serikali Juu ya Kufukuzwa Kazi kwa
Wakurugenzi
Mheshimiwa
Spika, mara baada ya waziri kutangaza kuwavua nyadhifa zao wakurugenzi hao tarehe
24 Februari 2014, Katibu Mkuu wa wizara hii Bi. Maimuna Tarishi aliwarudisha
kazini wakurugenzi hao huku Serikali nayo kwa kupitia kurugenzi ya habari
maelezo,ikitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa taarifa za kufukuzwa kwa
wakurugenzi hao si sahihi. Pia, Ikulu kwa kupitia Katibu Kiongozi Balozi Ombeni
Sefue, ilitoa tamko la kuitaka Wizara kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za
utumishi wa umma za kumfukuza mtumishi kazi.
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002, Kifungu cha IV (23)
(2) inayozungumzia mamlaka ya Rais kumwondoa mtumishi aliyemteua kazini, amri
ya kumfukuza mtumishi wa umma itatekelezwa iwapo;
(a)hati
ya mashtaka imeandikwa dhidi yake (b)mtumishi wa umma amepewa nafasi ya kujibu
mashtaka hayo
(c)Maombi
yametolewa kwenye hati ya mashtaka kwa mujibu wa taratibu zilizo chini ya
kifungu namba 34.
Swali
la kumuuliza Waziri Nyalandu, je, hatua hizi zilifuatwa katika kuwasimamisha
kazi wakurugenzi hawa? Na je, maamuzi yake ya kumfukuza Prof. Songoro katika
vikao vya kamati na kumdhalilisha hata baada ya Ikulu kutoa maagizo ya Wizara
kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za kufukuza watumishi kazi ni utawala bora?
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka Serikali na Wizara kuhakikisha
kuwa, uamuzi wowote uliofanywa na kuendelea kufanywa katika kutekeleza maazimio
ya Bunge katika kuwawajibisha watumishi hao uzingatie sheria, taratibu na
kanuni kwa kuwa Sheria na Kanuni hizo zinaeleza wazi hatua zinazopaswa
kuchukuliwa. Vilevile, tunasikitishwa na mvutano baina ya waziri na katibu mkuu
wa wizara, hali ambayo inaonesha kuwa kuna mgongano aidha wa kimaslahi na hivyo
kuthibitisha kuwa Serikali ni dhaifu kwa kuwa, Waziri na Katibu Mkuu wa wizara
moja wanafanya kazi bila kushirikiana na kila mmoja akionekana kumvizia
mwenzake hadharani badala ya kukaa kwa pamoja kutekeleza maazimio ya Bunge lako
tukufu.
Aidha,
mvutano huu pia ni ishara kuwa, maazimio ya Bunge yanaendelea kupuuzwa na
Serikali kwa kigezo cha kuzingatia sheria na kanuni huku zikiwaacha watumishi
wenye tuhuma wakihamishwa vitengo na idara na kuendelezea urasimu uleule hata
uko wanapohamishwa.
Mheshimiwa
Spika, ngoma ikivuma sana hupasuka, tena Mungu siku zote hamfichi mnafiki na
debe tupu haliachi kutika (si maneno yangu, bali ya wahenga). Si mara ya kwanza,
kwa Kambi Rasmi ya Upinzani kuhoji juu ya usafi wa Lazaro Nyalandu, Waziri wa
Maliasili na Utalii, na mara kadhaa tumeonesha kwa kiasi kikubwa udhaifu wake na
kutoa vielelezo mbalimbali vinavyotilia
shaka utendaji wake kabla na hata baada ya kukabidhiwa wizara hii nyeti!
3.0
TASWIRA YA TAIFA KATIKA JUMUIA ZA KIMATAIFA
Mheshimiwa
Spika, kwa muda mrefu Kambi Rasmi ya Upinzani imeendelea kutoa taarifa kwa
Serikali juu ya mtandao wa kimataifa wa ujangili ambao pia unahusisha viongozi
waandamizi wa Serikali, maafisa usalama wa taifa, wanajeshi wafanyabiashara
wakubwa, polisi, wanasiasa, Ikulu na watumishi wa umma. Serikali ya CCM imekua
ikitoa kauli za kubeza pamoja na majibu mepesi ya tuhuma hizi huku tatizo la
ujangili likiendelea kulichafua taifa katika jumuia ya kimataifa.
Mheshimiwa
Spika, katika hali ya kushangaza baada ya gazeti la Mail on Sunday la nchini
Uingereza kutoa taarifa kuwa biashara ya ujangili inahusisha watu wa karibu na
Rais wakiwemo wanasiasa, maafisa wa
Serikali na wafanya biashara wakubwa, Serikali ilitoa matamko mbalimbali pamoja
na kulaani taarifa ya gazeti hilo na hatimaye Waziri Nyalandu, alimwalika
mwandishi wa gazeti hilo kujionea mwenyewe shughuli za Serikali za kupambana na
ujangili ikiwemo kutembembelea ghala ya kuhifadhia pembe za ndovu
zilizokamatwa. Mwaliko huo ilikua ni katika kuthibitisha kuwa Serikali ya CCM
haina la kuficha.
Lakini
katika hali ya kushangaza, uchunguzi na taarifa zaidi umeonesha kuwa ndani ya
miaka minane (8) Serikali ya CCM, imekua ikiomba kibali bila mafanikio kutoka
CITES (Convention on International Trade on Endangered Species) cha kuuza
shehena ya pembe za ndovu takribani 34,000 zenye uzito wa tani 125 zenye
thamani ya dola za kimarekani milioni 150 sawa na shilingi Bilioni 244.5 za
kitanzania (kwa wastani wa sh.1630 kwa dola 1).
Mheshimiwa
Spika, jumuia ya kimataifa imeshangazwa na kitendo cha Tanzania kuomba kibali
cha kuuza shehena iliyokamatwa ya pembe za ndovu kwa kuwa ni biashara haramu na
kitendo cha Serikali kuomba kuyauza ni sawa na kuchochea ujangili zaidi kwa
kuwa hali hii itaongeza uhitaji wa pembe za ndovu kwenye soko haramu nchini
China. Jambo hili ni aibu kubwa kwa
taifa kuomba kufanya biashara haramu kwa kuwa imelidhalilisha taifa. Hii ni
sawa na Serikali ikamate madawa ya kulevya, halafu iamue kuyauza ili kupata
fedha.
Mheshimiwa
Spika, kitendo cha waziri wa maliasili na utalii kumwalika nchini mwandishi
aliyesemwa kuwa ametoa taarifa za uongo na kulichafua taifa, ili ajithibitishie
kuwa Tanzania ni safi katika matukio ya ujangili, Bwana Martin Fletcher, na
kumtembeza katika sehemu mbalimbali nchini ikiwa na nia ya kumfunga
mdomo(damage control), haikusaidia bali ilivumbua uchafu mwingi na huu wote
umewekwa wazi katika vyombo vya habari vya kimataifa na kuendelea kuonesha uozo
wa Serikali katika kushughulikia tatizo la ujangili nchini.
Mheshimiwa
Spika, imeelezwa kuwa Raisi ameshindwa kusimamia suala hili vizuri kwa kuwa
wanaohusika na ujangili ni watu wake wa karibu ama rafiki zake. Aidha, taarifa
hizo zimeendelea kubana kauli za Waziri Nyalandu za kuwa anawafahamu majangili
kwa majina na kuwataka majangili hao kuacha ujangili ama watawachukulia hatua
za kisheria. Maswali yanayoulizwa, je, ni kwa nini waziri hawataji watu
wanahousika na ujangili? Pili, inakuaje waziri anawajua kwa majina na hata
sehemu wanazokaa, lakini anashindwa kuwachukulia hatua? Inakuaje waziri,
awabembeleze watuhumiwa wakati kuna sheria, kanuni na taratibu za kuwachukulia
hatua wahalifu? Ni nini kipo nyuma ya pazia katika kuwalinda na kuwaficha
watuhumiwa wa ujangili?
3.1 Kukosekana kwa maafisa utalii katika balozi
mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, kuna taarifa kuwa katika balozi zetu
mbalimbali na muhimu ulimwenguni
kumekuwa hakuna maafisa utalii ambao watakuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa
wanaweza kuhakikisha kuwa tunapata watalii wa kutosha kwa ajili ya kuinua pato
la taifa letu.
Mheshimiwa Spika, katika ubalozi wa Tanzania –Berlin
ni kati ya balozi kubwa ulimwenguni ambao hauna afisa utalii pamoja na ukweli
kuwa ubalozi huu unahudumia nchi nyingine za
Poland,Austria,Hungary,Frankfut,Uswis,Romania,Bulgaria ,Slovakia na Jamhuri ya
Czech , kwa kipindi kirefu sana ubalozi huu umeomba kupatiwa afisa utalii
kutoka wizara ya mambo ya nje lakini mpaka leo hawajaweza kupelekewa maafisa
hao kwa ajili ya kutekeleza kwa vitendo diplomasia ya uchumi ambayo ndio msingi
wetu wa diplomasia ya kimataifa .
Kambi ya Upinzani, inataka kupata majibu ni lini
serikali itawapeleka wataalamu hao katika ubalozi huu kwa ajili ya kuimarisha sekta
ya utalii kwenye nchi zote muhimu ambazo zimekuwa mstari wa mbele katika sekta
ya utalii katika taifa letu. [1]
4.0
BIASHARA HARAMU YA
NYARA ZITOKANAZO NA WANYAMAPORI NA KUKITHIRI KWA TATIZO LA UJANGILI NCHINI
Mheshimiwa
Spika,
Kumekuwa
na ongezeko kubwa na watu wanaojishughulisha na uwindaji na biashara ya nyara
za Serikali bila bila kuwa na kibali au leseni toka mamlaka zilizowekwa
kisheria. Kwa mujibu wa sheria ya
wanyapori kifungu cha 80(1) sehemu ya 10 “mtu yeyote haruhusiwi kujihusisha na
biashara ya nyara (trophies) bila kuwa na leseni ya biashara ya nyara (trophy
dealer license). Na kifungu cha 80(2) kinampa Mkurugenzi wa Idara ya
Wanyamapori mamlaka ya kutoa leseni ya
biashara ya nyara kwa mtu yeyote ambaye
ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kupokea maombi kwenye fomu
maalum na kutimiza masharti yaliyowekwa ikiwa ni pamoja na kulipa ada
zilizopangwa.
Mheshimiwa Spika, leseni
ya biashara ya nyara inayotolewa katika Kifungu hiki haimruhusu mhusika
kuwinda, kuua au kupiga picha mnyama yoyote, badala yake inamruhusu kukamata,
kutengeneza bidhaa inayotokana na nyara, kununua au kuuza nyara – 80(3)”[2].
Mheshimiwa
Spika, licha ya kuwepo kwa sheria hiyo, bado wanyama wetu wanaendelea kuuwawa
kwa kasi ya ajabu. Aidha, kumekuwepo kwa taarifa zinazoonyesha kuwepo kwa
mtandao mpana wa wahusika wa biashara ya wanyama pori na bidhaa za wanyamapori
kutoka katika nchi kadhaa kama vile, Kenya, Msumbiji, DRC, Namibia na Afrika ya
Kusini.
Mheshimiwa
Spika, Kwa mujibu wa maelezo ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Lazaro
Nyalandu aliyoyatoa mbele ya Waandishi wa Habari wakati akiwa Naibu Waziri wa Wizara hii katika Hoteli ya Mount Meru – Arusha mwaka
jana, ni kwamba; kwa kipindi cha miaka mitatu, iliyopita tembo 31348 sawa na asilimia 42 walitoweka katika hifadhi ya
Selous na Mikumi na kwamba kuna mtandao
wa kijangili wa kimataifa (Sophisticated
International Syndicate) unaofanya kazi
hapa nchini. Aidha alitoa agizo kwa bodi ya wadhamini ya mamlaka ya hifadhi za
taifa (TANAPA) itoe maelezo ya kina kuhusu kuwepo watumishi wa ndani ya mamlaka
ya hifadhi wanaosadikiwa kushirikiana na majangili hao kuendesha ujangili ambao
unahatarisha hifadhi zetu na sifa ya nchi yetu.
Mheshimiwa
Spika, Waziri Nyalandu aliirudia kauli
hiyo mkoani Iringa, mwezi Juni, 2013 wakati wa kikao cha siku mbili cha wadau wa
ulinzi wa maliasili juu ya ujangili wa tembo katika mikoa ya Nyanda za juu
na kuahidi kwamba majina ya majangili yakiwemo ya vigogo wanaojihusisha na ujangili
wa tembo yatatangazwa hadharani, lakini mpaka sasa hakuna majina yoyote
yaliyotangazwa hadharani.
Mheshimiwa
Spika, utafiti
uliofanywa na Tanzania Wildlife Research Institute-TAWIRI katika mbuga ya
hifadhi ya Selou na Mikumi inaonyesha kuwa idadi ya Tembo imeshuka kutoka
74,900 mwaka 2006 hadi kufikia 43,552 mwaka 2009. Hii ikiwa na maana kwamba kwa
kipindi cha miaka mitatu takribani asilimia 42 ambayo ni Tembo 31,348 katika
hifadhi mbili tu waliuawa na majangili[3].
Hii ni hatari kubwa sana na kwa kutilia maanani kuwa Tembo mmoja anapatikana
baada ya miaka miwili (yaani Tembo hubeba mimba kwa kipindi cha miaka miwili
ndipo azae)
Mheshimiwa
Spika, biashara haramu ya nyara zitokanzao na wanyamapori hususan tembo
imechangia sana ujangili wa kutisha wa tembo kiasi kwamba idadi ya tembo
imepungua mno kiasi cha kuwafanya tembo wawe miongoni mwa jamii ya viiumbe
waliopo hatarini kutoweka kabisa (endangered species). Nasema hivi kwa sababu
idadi ya tembo kwa uchache, waliokuwepo katika nchi za Kiafrika kwa miaka
ya sabini walikuwa ni takribani milioni moja
na laki mbili (1,200,000) lakini kwa
sasa wamebakia wasiozidi laki tano[4]
Mheshimiwa Spika, hali
ya ujangili nchini imefika pabaya na ina kiasharia kibaya kwa miaka michache
ijayo. Takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2010, jumla ya tembo 10,000 waliuwawa Tanzania,
ikiwa ni sawa na wastani wa tembo 27 kwa siku. Mwaka 2012 pekee, tembo
takribani 23,000 wameuwawa kwa mwaka ambayo ni sawa na tembo 63 kwa siku. Hii
ni sawa na ongezeko la 57% kwa kipindi cha miaka 2. Kwa sasa Tanzania
inakadiriwa kuwa na tembo kati ya 150,000 na 170,000. Kutokana na takwimu hizi, ikiwa Tembo 63
wanauwawa kwa siku, ni dhahiri kwamba
kwa kipindi cha miaka 7 ijayo Tembo
hawa watakuwa wameuawa wote.
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na shirika la
Umoja wa Mataifa la kupamba na madawa ya kulevya na uhalifu (United Nation’s
Office on Drugs and Crime- UNODC-), inaonyesha kuwa nchi zilizo Kusini mwa
Jangwa la Sahara na nchi za Kusini
Mashariki mwa Asia ni wasambazaji
wakubwa wa bidhaa haramu za wanyamapori kwenye soko la China, Marekani na
baadhi ya nchi katika bara la Ulaya.
Bidhaa hizo za wanyamapori ni pamoja na pembe za ndovu, pembe za faru, ngozi za
chui na simba na viungo mbalimbali vya wanyamapori. Kwa mujibu wa utafiti huo
ni kwamba mununuzi hulipa kiasi cha dolla za kimarekani 2,500 kwa kila pembe
moja ya faru.
Mheshimiwa
Spika, tatizo la Ujangili limekuwa gumu kumalizwa kabisa kwa kuna taarifa
zinazohusisha askari wa Jeshi la Polisi
na Jeshi la Wananchi katika matukio ya ujangili na biashara haramu ya nyara na
taarifa hizo zimeripotiwa sana na vyombo vya habari, lakini cha kusikitisha ni
kwamba hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi ya askari wa majeshi hayo (yaani
jeshi la polisi na jeshi la wananchi wa Tanzania). Mpaka sasa Jeshi la Polisi
na Jeshi la Wananchi wa Tanzania hawajakanusha taarifa hizo jambo linaloashiria
kwamba pengine taarifa hizo ni za kweli.
Mheshimiwa
Spika, taarifa za baadhi ya askari walioripotiwa na vyombo vya habari kuhusika
na ujangili ni kama ifuatavyo:
1. Mnamo
Tarehe 7 January 2013, Gazeti la habari leo lilitoa taarifa za askari wawili
kujihusisha na biashara ya meno ya tembo na kuhusishwa na mauaji ya faru katika
mbuga ya Serengeti na mpaka sasa hakuna taarifa rasmi kutoka Serikalini juu ya
hatua zilizochukuliwa dhidi ya askari hao.
2.
Mnamo Januari 20, 2013 Sajenti wa Jeshi la
Wananchi Tanzania, Azizi Athuman Yusufu alikamatwa mkoani Arusha akiwa na pembe
mbili za ndovu na bunduki aina ya Riffle yenye namba 458 huku akitumia gari ya
mkufunzi wa kijeshi kutoka Zimbabwe anayefundisha nchini.
3.
Tarehe 23 Julai, mwaka
2013, walikamatwa watu saba wanaodhaniwa kuwa ni majangili , wakiwamo askari
watatu wa Magereza Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara wakiwa na gari la Magereza aina ya Land Cruiser lenye namba za usajili
STK 4394 lililokuwa limepakia nyara za
Serikali zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 55. Nyara hizo zilikuwa ni
pamoja na Twiga wawili, Pundamilia wawili, Swala, Palapala majike wawili na
Mbuni wawili.
Mheshimiwa Spika, Biashara haramu ya
pembe za ndovu imevuka mipaka ya
nchi na imeanza kushamiri katika ukanda wa
Afrika ya Mashariki jambo ambalo linatishia kutoweka kabisa kwa wanyama hao
ambao ni kivutio kikubwa cha utalii. Taarifa katika mtandao wa habari wa
“Annamiticus” (www.annamiticus.com)
zinasema kwamba mwaka 2012, makontena mawili kutoka Kenya na Tanzania
yalikamatwa huko HongKong yakiwa yamebeba tani 4 (Kilo 4,000) za pembe za
ndovu.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa
taarifa hiyo, kontena lililotoka Tanzania lilikuwa limeandikwa “plastic scrap”
ikimaanisha kuwa lilikuwa na vifaa ya plastiki lakini baada ya kufunguliwa
kulikuwa na vipande 972 vya pembe halisi za ndovu zenye uzito wa kilogramu
1,927 pamoja na kilo moja na nusu ya unga wa pembe za ndovu zilizosagwa.
Kontena lililotoka Kenya lilikuwa limeandikwa “roscoco beans” yaani maharage
aina ya roscoco, lakini lilipofunguliwa kulikuwa na vipande 237 vya pembe za
ndovu sawa na kilogramu 1,884.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa
taarifa hiyo, wingi wa pembe hizi za ndovu zilizokamatwa, unadhihirisha kwamba
tembo takriban 600 kwa uchache waliuwawa.
Mheshimiwa Spika, mwezi Aprili,2013
kontena lingine lilikamatwa likiwa limesheheni pembe za ndovu 113 huko
China zenye thamani ya Dola za Kimarekani 400,000.Kontena hili liliandikwa kwamba
limebeba vipuri (spareparts) toka Burundi. Kwa kuwa Burundi haina bandari, kuna
uwezekano mkubwa kwamba kontena hilo lilipitia bandari ya Tanzania, na hivyo
kuna uwezekano pia kwamba pembe hizo zinatokana na tembo waliouwawa Tanzania.
5.0
MAENDELEO YA SEKTA YA
WA WANYAMAPORI NCHINI
Mheshimiwa
Spika, mchango wa sekta ya wanyamapori katika maendeleo ya uchumi wa nchi yetu
ni mkubwa sana. Takwimu[5]
zinaonyesha kuwa uwindaji wa kitalii kwa miaka mitatu kati ya 2009 na 2012
uliingiza shilingi bilioni 91. Kwa sababu hiyo, Wizara ya Maliasili na Utalii
kupitia idara yake ya Wanyamapori inatakiwa kuilinda na kuiendeleza sekta hii
ili iendelee kuchangia zaidi katika uchumi wetu.
Mheshimiwa
Spika, katika muktadha wa kuilinda na kuiendeleza sekta ya wanyamapori, Bunge lilitunga
Sheria ya Uhifadhi ya 2009, ambayo inatumika pamoja na
sera ya wanyamapori ya mwaka 2007 ili kuratibu na kudhibiti shughuli za
uwindaji wa wanyamapori kwa namna ambayo sekta ya wanyampaori inakuwa endelevu.
Mheshimiwa
Spika, ulinzi wa Sekta ya wanyamapori ni muhumu kwa kuwa sekta inachangia
ukuaji wa uchumi katika Nyanja mbalimbali. Kwa mfano wanyamapori ni kivutio
kikubwa cha watalii ambao hutoa fedha nyingi za kigeni wajapo kutalii hapa
nchini kwa ajili ya kutazama na kuwapiga picha wanyama hao. Aidha sekta ya
wanyama pori inachangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kutoa ajira kwa
wananchi na pia kukuza soko la bidhaa za ndani.
Mheshimiwa
Spika, licha ya umuhimu wa sekta hii, Serikali imekuwa haifuatilii makampuni ya
uwindaji yenye leseni kuona kama wanafuata sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya
2009. Matokeo ya udhaifu wa Serikali katika ufuatiliaji, kumekuwa na uvunjaji
mkubwa wa sheria jambo ambalo limesababisha uwindaji ufanyike kiholela. Kwa
mfano, Kampuni ya Uwindaji ya Green Miles Safaris Limited imekuwa ikiwakimbiza
na kuwakamata watoto wa wanyamapori pindi wanapozaliwa kinyume na kifungu cha
19(1) cha Sheria ya Wanyamapori ya 2009. Aidha Sheria hiyo inapendekeza adhabu
ya kifungo cha miaka mitano gerezani na au faini kati ya shilingi 500,000/=
hadi shilingi 2,000,000/=
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataarifa kwamba Kampuni hii ya Green Miles
Safaris Limited ilishapewa zuio na Mahakama la kufanya uwindaji kutokana na
uwindaji usiozingatia sheria lakini Kampuni hiyo ilipita mlango wa nyuma na
kuomba kilbali cha uwindaji kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori na Mkurugenzi akatoa kibali na hivyo wote wawili wakapuuza
uamuzi wa Mahakama.
Mheshimiwa
Spika, Kampuni hii ya Green Miles Safaris Limited, pamoja na uhalifu mwingi
inaoufanya katika mbuga zetu wakati wa uwindaji, imekuwa ikilindwa na Serikali
ndio maana Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Upinzani Bungeni inashawishika
kuamini kwamba Serikali ndio chimbuko la tatizo la Ujangili na uwindaji haramu
wa wanyamapori hapa nchini.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe maelezo mbele ya bunge
hili ni kwa nini haijaichukulia Kampuni ya Uwindaji Green Miles kwa kufanya
uwindaji haramu hapa nchini?
Mheshimiwa
Spika, Tatizo kubwa la Maendeleo ya Sekta ya Wanyapori ni kwamba Serikali huwa
haifuati hata mapendekezo yanayotolewa na Kamati za zinazoudwa na Serikali
yenyewe. Kwa mfano, mwaka 2006, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii kwa
wakati huo Mheshimiwa Anthony Mwandu Diallo (Mb), aliunda Kamati ya Wataalam
ambayo aliitaka ifanye uchambuzi wa kina wa shughuli za uwindaji wa kitalii
nchini. Uchambuzi huo ulitakiwa uzingatie utendaji kazi katika shughuli za
uwindaji wa kitalii, mafanikio yaliyofikiwa mpaka sasa na matatizo
yanayoikabili tasnia hiyo. Hatimaye, Kamati ilitakiwa kumshauri Mheshimiwa
Waziri namna ya kuleta mabadiliko ndani ya sekta hiyo kwa minajili ya kulinda
uhifadhi, kuwawezesha wananchi kushiriki katika uwindaji wa kitalii kwa lengo
la kuongeza ufanisi na tija ili iweze kutoa mchango mkubwa zaidi katika kuondoa
umaskini na kuongeza Pato la Taifa.
Mheshimiwa
Spika, Hadidu za rejea kamati hiyo ilizopewa ziliitaka Kamati:[6]
(i)
Ipitie utaratibu wa sasa wa uombaji na
ugawaji wa Vitalu vya Uwindaji wa Kitalii pamoja na chombo chake cha ugawaji
kuona kama havibagui wala havisababishi malalamiko kwa wadau mbalimbali;
(ii)
Ichambue kwa makini vigezo na masharti
yaliyopo yanayohusu ukaguzi wa uwezo wa Kampuni za Uwindaji zinazowasilisha
maombi kwa ajili ya Uwindaji wa Kitalii ili kuona kama yanafaa kwa mazingira ya
sasa;
(iii)
Ichambue Mikataba mbalimbali ya kampuni
za uwindaji; ya zamani na inayoendelea kwa lengo la kujiridhisha kama inafaa au
ina upungufu unaohitaji marekebisho ili kulinda uhifadhi na maslahi ya umma.
(iv)
Iangalie Kanuni za Uwindaji wa Kitalii
na zile za Utalii wa picha pamoja na Sheria ya Wanyamapori ya mwaka 1974 na
kushauri namna ya kuondoa migongano ambayo imejitokeza baada ya kuruhusu utalii
wa picha kwenye maeneo ya uwindaji wa kitalii.
(v)
Ichambue Sera na Sheria zinazohusiana na
Wanyamapori na Utalii, na Kanuni za Uwindaji wa Kitalii ili kuona kama Wananchi
wanafaidika na uwindaji huo wa kitalii.
(vi)
Ichambue utaratibu wa ukusanyaji mapato,
kubaini njia ambazo zitaongeza maduhuli ya Serikali, na kutathmini utaratibu wa
ugawaji vitalu kwa njia ya zabuni.
(vii)
Mwisho, Kamati iangalie uwezekano wa
Serikali kuwawezesha Wananchi kushiriki kikamilifu katika tasnia hii ya
uwindaji wa kitalii.
Mheshimiwa
Spika, Mapendekezo ya Kamati hiyo yalikuwa ni kama ifuatavyo:
1. Kuboresha
utaratibu wa ugawaji wa vitalu kwa kuipa Kamati ya Ugawaji Vitalu nguvu za
kisheria na kwa kupanua uwakilishi wake.
2. Kuunda
Wakala wa Serikali wa kusimamia shughuli za uwindaji wa kitalii badala ya Idara
ya Wanyamapori.
3. Kuangalia
upya umiliki wa vitalu ili kuwawezesha wananchi kushiriki zaidi katika uwindaji
wa kitalii kwa njia ya ubia na baadaye kumilikishwa vitalu wakati wageni na
wananchi watafanya kazi ya kuwindisha.
4. Serikali
iwawezeshe Wawindaji Bingwa wa Kitanzania ili waweze kumiliki vitalu na kutumia
ujuzi na uzoefu walionao. Serikali inaweza kuwawezesha wananchi kwa kuzungumza
na mabenki ili wapunguze riba ya kukopa fedha benki na kuruhusu matumizi ya
vitalu kama dhamana. Pia wawindaji bingwa waanzishe bodi yao ya kitaalam.
5. Kuthamini
vitalu vya uwindaji wa kitalii na kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato
ili kuongeza mapato ya Serikali.
6. Kuweka
ukomo wa umiliki wa kitalu wa vipindi viwili vya miaka mitano ili ili kuruhusu
waombaji wapya.
7. Kuboresha
taarifa za sekta ya Wanyamapori kwa kuweka taarifa zote muhimu zinazohusu
shughuli za uwindaji wa kitalii kwenye Tovuti ya Idara.
8. Idara
iimarishe ufuatiliaji na tathmini ya vitalu kwa kuanzisha chombo huru cha
kusimamia shughuli za uwindaji wa kitalii.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili ni kwa kiwango gani mapendekezo ya Kamati hiyo
yametekelezwa na ni mangapi ambayo bado
kutekelezwa na ni kwanini?
6.0
UTALII NA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA
Mheshimiwa
Spika,
Kwa
eneo kubwa la ardhi lililofunikwa na wingi wa misitu pamoja na aina mbalimbali
za maua na viumbe, Tanzania ni mojawapo
ya vivutio vikubwa vya utalii barani Afrika. Nchi yetu ina raslimali nyingi
asilia ikiwemo pamoja na maeneo mengi ya nyika za mapori yenye aina nyingi za banoai.
Mheshimiwa
Spika, Miongoni mwa vivutio vya utalii ni pamoja na Mbuga za wanyama , hifadhi
za taifa, hifadhi zilizozuiliwa na
maeneo ya kihistoria. Hata hivyo kwa sababu ya ongezeko la joto, baadhi
ya hivi vivutio ikiwemo theluji katika kilele cha mlima Kilimanjaro iko katika
hatari ya kupotea. Na baadhi ya wanyama katika mbunga zenye ukame mkubwa
wameanza kupungua na kuathirika.
Mheshimiwa
Spika, Licha ya kuwa na neema ya kuwa na vivutio vingi vya utalii, bado sekta
ya utalii inakabiliwa na chamgamoto kadhaa, zikiwa ni;
(i) Uendelezaji
wa kazi zitakazohakikisha kuendelea kuwepo kwa vivutio mbalimbali vya utalii
kwa kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi;
(ii)
Ukarabati wa miundombinu kama vile
barabara, madaraja, kambi za watalii na upatikanaji wa umeme kwa ajili ya
watalii wa mbugani;
(iii)
Uwezo mdogo wa idara zinazohusika
kusimamia, kulinda vivutio vya utalii, kama vile kuendesha na kutangaza vivutio
vya utalii vilivyopo.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani, inaamini kabisa tatizo la umeme katika vivutio
vya utalii vilivyopo mbugani, suluhisho ni kutumia umeme wa jua (solar energy),
hili ni rahisi katika utekelezaji wake.
Mheshimiwa
Spika, kama ambavyo nitaonyesha hapo baadae makusanyo yanayopatikana kutoka
sekta ya utalii hayana uwiano wa moja kwa moja na uwekezaji katika sekta hiii.
Ndiyo sababu kubwa ya mapato ya sekta kutokuakisi vivutio tulivyonavyo hapa
nchini.
Mheshimiwa
Spika, uwekezaji katika Sekta ya Utalii ni suala lenye tija kubwa katika uchumi
wetu kwa kuwa sekta hiyo imekuwa ikichangia katika uchumi wa Taifa licha ya
uwekezaji mdogo uliofanyika katika sekta hiyo.
Mheshimiwa
Spika, takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa
katika maeneo yote ya hifadhi zetu kwa
sasa kuna kuna hoteli zenye uwezo wa
kutoa huduma za malazi (carrying capacity) kwa watu 6,681 ambapo kwa miaka mitano ijayo
idadi hii itafikia uwezo wa kulaza watu 8,421. Hiki ni kwango kidogo sana cha
huduma za malazi kiasi kwamba tunapoteza fursa ya kunufaika katika sekta ya
utalii.
Mheshimiwa
Spika, japokuwa uwekezaji katika sekta ya utalii ni mdogo lakini sekta
imeendelea kuwa nguzo muhimu katika uchumi wetu. Kwa mwaka 2011 utalii na
usafiri wa kitalii ulichangia asilimia 13 kwenye pato la taifa na kuchangia
takriban asilimia 25 ya fedha za kigeni. Aidha,
Mpango unaeleza kuwa lengo ni kuongeza wageni kwa asilimia 40 kutoka wageni 671,886 kwa sasa hadi
940,640 ifikap June 2016. Aidha Mpango unalenga pia kuzidisha siku za mtalii
kutembelea maeneo yenye vivutio vya kitalii nchini kutoka siku wastani wa siku
11 za sasa hadi wastani wa siku 18[7].
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa tathmini ya mpango huo ili wananchi
wajue tumefanikiwa kwa kiwango gani katiaka kuboresha sekta ya wanyamapori.
Mheshimiwa
Spika, miundombinu ya usafiri na usafirishaji ya ndani ya nchi, uwekezaji
katika ujenzi wa hotel kwenye maeneo muhimu ya utalii kama vile kwenye hifadhi,
mikoa inayozunguka mlima Kilimanjaro kutasaidia sana kuvutia watalii. Hivyo
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuboresha miundo mbinu ya usafiri
hasa wa anga ili na kujenga hoteli za viwango vya Kimataifa katika maeneo yenye
vivutio vya watalii ili kuvutia mashirika ya mengi ya ndege toka nje kuja hapa.
Ni
rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa Serikali kwamba ifufue shirika letu la Ndege
la Taifa ili tuweze kumudu ushindani katika usafiri wa anga na hapohapo
kuongeza idadi ya watalii katika nchi yetu. Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro na
ule wa Julius Nyerere Dar es Salaam vikiboreshwa vinaweza kuwa ni kitovu cha
mashirika mengi ya kimataifa kubadilishia wasafiri kama kuna mkakati makini.
Mheshimiwa Spika, watalii toka nje wanapenda sana kupanda
ndege za nchi wanazotembelea zaidi kuliko kupanda ndege za kuunganisha. Kwa
njia moja au nyingine usafiri huo unawapunguzia gharama. Mfano mzuri ni miaka
ya themanini wakati Air-Tanzania ilipokuwa inafanya safari zake nchi za Ulaya,
watalii wengi walikuwa wanakuja kwa ndege zetu. Hoja ni kwamba Serikali ina
mkakati gani wa kufufua Shirika la Ndege la Taifa (ATC) Kambi Rasmi ya Upinzani
inapendekeza Serikali kuingia ubia na makampuni binafsi kupitia mpango wa Private
Public Pertnership – ( PPP) ili kuboresha huduma za usafiri wa anga hapa nchini
ambao unachoche watalii wengi kuja kwa kuwa kuna usafiri wa moja kwa moja.
7.0
SEKTA YA MISITU
Mheshimiwa
Spika, misitu ina nafasi muhimu ya kumeza hewa ukaa duniani wakati ikizuia
uharibifu wa udongo/ardhi. Ukataji miti na uondoaji misitu uliokithiri
unachangia katika ongezeko la uzalishaji wa hewa ukaa Tanzania. Kupitia misitu
mingi tuliyonayo Tanzania imeendelea kutoa huduma ya kumeza hewa ukaa duniani,
bila ya kuwepo utaratibu wowote wa kimataifa kutoa fidia yoyote.
Mheshimiwa
Spika, mbali ya kuwa na misitu mingi, kumekuwepo na changamoto nyingi
zinazoikabili sekta ya misitu, nazo ni:
a) Kufanya
uendelezaji wa misitu kama raslimali ya kumeza hewa ukaa na kuinufaisha jamii
inayoizunguka;
b) Kuthibiti
ubora na uendelevu wa misitu
c) Jamii
inayoizunguka misitu kunufaika na biashara ya hewa ukaa duniani;
d) Ujenzi
wa uwezo wa kufanya tafiti za uendelezaji misitu nchini;
e) Uendelezaji
wa njia bora zinazowezesha jamii inayozunguka misitu kunufaika na raslimali
hiyo.
Mheshimiwa
Spika, kutokana na changamoto hizo, zinazoikabili sekta hii ya misitu, Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka kuhakikisha kwa kadri misitu ya Tanzania
inavyoendelea kutoa huduma ya kimataifa ya kumeza hewa ukaa duniani, hivyo ni
lazima nchi na wananchi wetu tunufaike kwa kupata kazi na teknolojia
zinazochangia maendeleo endelevu.
Mheshimiwa
Spika, sambamba na hilo ni kwamba, ni muhimu Serikali kuhakikisha unajengwa
uelewa kwa jamii na wadau wa misitu juu ya uwepo wa fursa za kutumia uwezo wa
misitu kumeza kumeza hewa ukaa kama chanzo cha kunufaika na biashara ya hewa
ukaa duniani. Kuhamasisha ongezeko la matumizi ya vyanzo mbadala vya nishati ya
kupikia na kuchemshia na kupunguza msongo kwenye misitu yetu kwa hitaji hilo.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasema kuwa katika kuhamasisha hilo, ni muhimu
kuwepo kwa misitu mfano na miradi mfano katika ngazi za wilaya na vijiji ili
wananchi waone jinsi misitu inavyoweza kuwanufaisha wananchi wanaozunguka
misitu mfano hiyo. Hili linawezekana kama mipango na umakini katika utekelezaji
wake utakuwepo.
Mheshimiwa
Spika, uwekezaji katika kilimo cha miti ni mojawapo ya kilimo ambacho kwa muda
mrefu kinaweza kuleta tija kubwa kwa wananchi hasa hapa nchini, uwekezaji huu
unakabiliwa na chamgamoto kubwa ya kukosekana kwa mikopo ya muda mrefu na
ambayo inaweza kuwa-accommodate wakulima ambao hawana dhamana ya kuweka zaidi
ya umiliki wa kimira wa ardhi husika, jjambo ambalo halikubaliwi na taasisi za
fedha.
Mheshimiwa
Spika, utaratibu huu wa kilimo cha miti ni maarufu sana katika mikoa ya Iringa
na Njombe, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge ni
utaratibu gani hadi sasa ambao wakulima wadogo hasa wa miti wanasaidiwa kupata
mikopo ya muda mrefu katika kukabiliana na tatizo hili la uwepo wa hewa ukaa na
kuongeza kipato.
8.0
MAPITIO YA BAJETI KWA
IDARA NA VITENGO VYA WIZARA
Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/14 wizara ilitarajia kukusanya maduhuli ya jumla
ya shilingi bilioni 148.97 kutoka katika Idara na taasisi zilizo chini yake.
Mwaka huu wa fedha wizara inatarajia kukusanya jumla ya shilingi bilioni 144.6,
ambayo ni pungufu ya shilingi bilioni 4.37 kwa kulinganisha na makadirio ya
mwaka 2013/14.
Mheshimiwa
Spika, randama inaonyesha kuwa Idara ya wanyamapori kwa kipindi cha mwaka
2013/14 ili kadiriwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 28.65, Lakini hadi mwezi Machi, 2014 ilikuwa
imekusanya kiasi cha shilingi bilioni 8.92 ambayo ni sawa na asilimia 31.13 ya
malengo. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2014/15 Idara ya Wanyamapori imepanga
kukusanya jumla ya shilingi bilioni 15.55 kutoka kwenye vyanzo vyake vilivyo
chini ya idara. Makadirio haya ni pungufu ya shilingi bilioni 13.1 kwa
kulinganisha na mwaka 2013/14.
Mheshimiwa
Spika, kwa takwimu hizo ni kwamba Sekta
ya Maliasili na Utalii inashuka kimapato. Kambi Rasmi ya Upinzani
inaitaka Serikali kueleza sababu zilizofanya mapato yatokanayo na makusanya ya
maduhuli kwa shuka kwa kiasi kikubwa namna hiyo. Hii ni kwa sababu kwa mujibu
wa Takwimu zilizotolewa na taarifa ya uchunguzi maalum ni kwamba kwa kipindi
cha kuanzia mwaka 2009 hadi 2012 Idara ilikusanya shilingi bilioni 91 na hali
halisi ni kwamba uwezekano kukusanya zaidi ni mkubwa zaidi.
Mheshimiwa
Spika, kuhusu matumizi ya kawaida, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni
19.163 kwa ajili ya matumizi ya Idara hiyo, ambayo ni sawa na asilimia 22.7 ya
makusanyo yake. Lakini hadi mwezi machi 2014, Serikali imetoa kiasi cha
shilingi bilioni 9.161 tu. Swali hapa ni kwamba idara itawezaje kujiendesha
ikiwa fedha iliyotolewa ni kidogo namna hiyo? Ikumbukwe kwamba Idara hii inasimamia
taasisi/vyuo na wakala zipatazo sita ambazo ni TANAPA, NCAA, TAWIRI,CAWM-Mweka,
PWTI na CBCTC ambazo zinahitaji fedha za kutosha kuziendesha.
Mheshimiwa Spika, fedha za maendeleo
zilizotolewa kwa ajili ya maendeleo kwenye sekta ya wanyamapori, ni kwa miradi
miwili tu ambayo ni mradi wa KILORWEMP unaotekelezwa kwa ushirika kati ya
Tanzania na Serikali ya Ubelgiji. Mwaka 2013/14 zilitengwa jumla ya shilingi
bilioni 1.82, lakini hadi Machi 2014 shilingi milioni 310 ambazo zilitoka
Serikali ya Ubelgiji.
Mheshimiwa
Spika, mradi wa pili ni ule wa Kulinda ushoroba wa Selous-Niassa, ambao
unatekelezwa kwenye wilaya za Namtumbo na Tunduru kwa kushirikiana na Serikali
ya Ujerumani. Kwa mwaka jana hakuna fedha zilizotolewa.
Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/14 Idara ya Utalii ilikadiriwa kukusanya jumla
ya shilingi bilioni 16.896 lakini hadi mwezi mach, 2014 ilikuwa imekusanya
shilingi bilioni 3.25 ambayo ni sawa na asilimia 19 tu ya matarajio kwa mwaka.
Aidha, fedha zilizoidhinishwa kwa ajili ya Matumizi ya kawaida kwa idara na
Taasisi zilizo chini yake ni shilingi bilioni 12.1, lakini hadi Machi, zilikuwa
zimetolewa shilingi bilioni 3.36.
Mheshimiwa
Spika, mwaka wa fedha 2014/15 idara hii ya Utalii inatarajia kukusanya jumla ya
shilingi bilioni 16.91. Aidha, kwa maendeleo Iadara hii imetengewa jumla ya
shilingi bilioni 1.2. Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza inakuwaje Idara
inakusanya shilingi bilioni 16.91 lakini uwekezaji unakuwa wa shilingi bilioni
1.2, aidha uwekezaji huo hauna matokeo ya moja kwa moja na ukuaji wa utalii. Je
ni kwa vipi katika Dunia hii ya ushindani katika sekta ya utalii inaweza kuleta
tija na kuinua uchumi?
9.0
HITIMISHO
Kambi
Rasmi ya Upinzani, haitochoka kuikosoa Serikali kwa kuwa, kwa muda mrefu sasa
katika Wizara hii tumekua tunatoa mapendekezo ambayo yanabezwa. Na kwa kuwa ni
wajibu wetu kuisimamia ipasavyo Serikali ya CCM, tunazidi kusisitiza kuwa ili
sekta ya maliasili na utalii iendelee kuna haja nzima ya kubadilisha mfumo wa
usimamizi, uendeshaji na utekelezaji wa Wizara, ambao utatoa fursa kwa viongozi
waandamizi wa Wizara pamoja na watumishi kutimiza na kutekeleza majukumu yake
bila mashinikizo ya kisiasa.
Ni
rai yetu kuwa, Serikali itayafanyia kazi mapungufu yote ambayo tumekua
tukiyasema kwa muda mrefu sasa na kuisimamia ipasavyo sekta hii hili iwe
mhimili wa uchumi kwa taifa kwa kuongeza mapato pamoja na kutoa nafasi za ajira
kwa wananchi wa taifa letu.
Mheshimiwa
Spika, naomba kuwasilisha.
..................................................
Mch.
Peter S. Msigwa (MB)
Msemaji
Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Wizara ya Maliasili na Utalii.
13.05.2014
No comments:
Post a Comment