Wednesday, May 14, 2014

SERIKALI IMESEMA MATIBABU YA DENGUE HUTOLEWA BILA MALIPO

Dengue-Mei11-2014
Na Magreth Kinabo – MAELEZO
14/05./2014
 
 Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Said Meck Sadiki, amewataka wananchi wa mkoa huo wanapohisi wana dalili za ugonjwa wa dengue kuwenda katika hospitali za Serikali kwa kuwa matibabu hutolewa bila malipo.
 
Kauli  hiyo imetolewa na Mkuu huyo wakati akizungumza na waandishi wa habari  baada ya kuulizwa swali juu ya gharama   kubwa za matibabu ya ugonjwa huo, kwenye ukumbi wa mkutano wa Mwalimu J.K. Nyerere jijini Dares Salaam.
 
 “Tunaomba wananchi wanapohiisi dalili za ugonjwa huo kwenda katika hospitali za Serikali ,ambazo ni Amana, Mwananyamala na Temeke kwa kuwa matibabu yanatolewa bila malipo” alisema Sadiki.
 
 Akizungumza na mwandishi wa habari hizi,leo Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamwaja alisema vituo vyote vya Serikali vinapaswa kutoa matibabu ya ugonjwa huo bila malipo kwa kuwa  ugonjwa huo ni mlipuko na magonjwa ya milipuko  matibabu yake hutolewa bila malipo.
 
 Mwamwaja pia alisema ikitokea hata vituo vya afya vya binafsi vikapewa vitenganishi  na vifaaa vya tiba na Serikali navyo vinasapwa kutoa matibabu ya ugonjwa huo bila malipo.
 
 Mkuu huyo wa mkoa alisema kwa sasa wanajenga uwezo ili kila wilaya iwe  na vituo vitano kwa ajili ya matibabu ya ugonjwa huo.
 
 Sadick aliongeza kuwa Serikali itanyunyuzia dawa ya (Lavacide) sehemu za mikusanyiko kama vile mashulenina kwenye madimbwi, lakini maeneo ya hotelini na  mabaa watapaswa kunyunyuzia dawa kwa gharama zao.
 
“ Kwa upande wa wizara, idara na taasisi za Serikali wanapaswa kunyunyuzia dawa  kwa gharama zao,(yaani matumizi mengineyo)” alisisitiza huku akisema hata kwenye ofisi yake wamefanya hivyo kwa gharama zao.
 
Aidha Sadiki aliwataka viongozi wa mitaa na watendaji wengine kuwahimiza wananchi kuhusu usafi wa mazingira ili kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo.
 Alisema wananchi wanapaswa  kuhakikisha vifuu vya nazi visoda kwani maji kidogo yanayokaa  katika vitu husababisha mbu  wanaosabbaisha ugonjwa huo kuzaliana , hivyo vinatakiwa   visitupwe ovyo na kufunika maji safi wanayoyahifadhi.
 
 Alisisitiza hatua ya kwanza kuzuia ugonjwa huo ni usafi wa mazingira,hivyo dawa ni hatua ya mwisho.

No comments: