STARS YAJIPIMA KWA BOTSWANA
Timu ya Taifa (Taifa Stars) inacheza mechi ya kirafiki na Botswana leo (Julai Mosi mwaka huu) kuanzia saa 9 alasiri kwa saa za huko.
Mechi itakayofanyika Uwanja wa Taifa jijini Gaborone ni sehemu ya maandalizi ya Taifa Stars kwa ajili ya mechi ya michuano ya Afrika dhidi ya Msumbiji (Mambas) itakayochezwa Julai 20 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inatarajiwa kurejea nchini Julai 6 mwaka huu kuendelea na programu nyingine kwa ajili ya mechi dhidi ya Msumbiji.
Wakati huo huo, kutakuwa na utaratibu maalumu kwa waandishi wa habari za michezo kwa ajili ya kuripoti mechi ya Stars dhidi ya Msumbiji. Hivyo, vyombo vya habari vinatakiwa kutuma majina mawili ya waandishi watakaoripoti mechi hiyo. Mwisho wa kupokea majina hayo ni Julai 8 mwaka huu.
WACHEZAJI WATANO WAOMBEWA ITC
Wachezaji watano wameombewa Hati ya Uhamisho ya Kimataifa (ITC) ili waweze kucheza mpira wa miguu nchini na nje ya Tanzania.
Abdulhalim Humoud kutoka Simba, Crispine Odulla (Coastal Union) na Haji Ugando (Mbagala Market FC) wameombewa ITC na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya (FKF) ili wakacheze nchini humo katika klabu za Sofapaka, Bandari FC na Nakuru All Stars.
Vilevile TFF imemuombea ITC mchezaji Ismaila Diarra kutoka nchini Mali ili aweze kujiunga na timu ya Azam FC. TFF inafanyia kazi maombi hayo, na mara taratibu zote zitakapokamilika itatoa ITC hizo kwa wachezaji wanaokwenda nje ya Tanzania.
SERENGETI BOYS YAJINOA KUIKABILI AFRIKA KUSINI
Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) inaendelea vizuri na mazoezi kujiandaa kwa mechi ya mashindano dhidi ya Afrika Kusini (Amajimbos).
Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili itachezwa Ijumaa ya Julai 18 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Hababuu Ali Omari ameshafanya mchujo wa awali wa wachezaji wa timu hiyo kutoka 39 na kubaki na 31. Timu hiyo imepiga kambi kwenye hosteli ya TFF iliyopo Uwanja wa Karume.
MBEYA CITY, PRISONS KUJARIBU TIKETI ZA ELEKTRONIKI
Timu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) za Mbeya City na Tanzania Prisons zinacheza mechi ya kirafiki Jumamosi (Julai 5 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Mechi hiyo ambayo itakuwa ya kwanza kuchezwa jijini Mbeya katika mfumo wa matumizi ya tiketi za elektroniki kwa washabiki wanaoingia uwanjani itaanza saa 10 kamili jioni.
Kiingilio ni sh. 3,000 kwa majukwaa yote ambapo tiketi zimeanza kuuzwa leo (Julai Mosi mwaka huu).
Wakati huo huo, keshokutwa (Julai 3 mwaka huu) kutakuwa na mafunzo ya matumizi ya tiketi za elektroniki yatakayofanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya kuanzia saa 3 asubuhi.
Washiriki wa mafunzo hayo ni wasimamizi wa mechi katika uwanja huo, viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya (MREFA), meneja wa Uwanja wa Sokoine na msaidizi wake, makatibu wa Tanzania Prisons na Mbeya City, maofisa habari wa Mbeya City na Tanzania Prisons, Ofisa Usalama wa MREFA na wasimamizi wa milangoni (stewards).
BONIFACE WAMBURA MGOYO
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment