Tuesday, July 8, 2014

MFUMUKO WA BEI NCHINI UMEPUNGUA – OFISI YA TAIFA YA TAKWIMU.

NBS -1(1)
Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na sensa ya Watu na Makazi Bw. Ephraim Kwesigabo akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu kupungua kwa  mfumuko wa bei nchini.
…………………………………………………………………..
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
Dar es salaam.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu imeeleza kuwa mfumuko wa bei nchini kwa mwezi Juni 2014 umepungua ikilinganishwa na mwezi uliopita kutokana na kupungua kwa bei ya bidhaa na huduma za jamii katika maeneo mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na sensa ya Watu na Makazi Bw. Ephraim Kwesigabo amesema kuwa mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwezi Juni, 2014 umepungua na kufikia asilimia 6.4 kutoka asilimia 6.5.

Amesema kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma mbalimbali kwa mwezi Juni 2014 imepungua ikilinganishwa na ile iliyokuwepo mwezi Mei kutokana na hali ya kupungua kwa bei kwenye bidhaa na huduma
Ameeleza kuwa mfumuko wa bei za bidhaa za vyakula na migahawa kwa mwezi Juni umeongezeka hadi asilimia 8.5 kutoka asilimia 7.9 za mwezi Machi mwaka huu na kuongeza kuwa bei za bidhaa za vyakula na vinywaji baridi imeongezeka hadi asilimia 7.8 kutoka asilimia 7.2 za mwezi uliopita huku badiliko la fahirisi za bidhaa zisizo za vyakula likipungua hadi asilimia 4.9 kwa mwezi Aprili 2014 kutoka asilimia 7.2 iliyokuwepo mwezi uliopita.
Kwa upande wa mfumuko wa bei unaopimwa kwa kipimo cha mwezi Bw. Kwesigabo amesema kuwa umepungua kwa asilimia 0.6 ikilinganishwa na kupungua kwa asilimia 0.4 kama ilivyokuwa kwa mwezi Mei mwaka huu, huku fahirisi za bei za taifa zikiongezeka hadi kufikia 148.98 kwa mwezi Juni 2014 kutoka 140.00 za mwezi Juni 2013.
Amezitaja bidhaa zilizochangia ongezeko la fahirisi za bei nchini kuwa ni pamoja na mchele, mahindi,unga wa Muhogo, Viazi vitamu, dagaa, matunda jamii ya machungwa,mbogamboga na vitunguu maji.
Kuhusu mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula zinazotumika nyumbani na migahawani amefafanua kuwa kwa mwezi Juni umepungua hadi kufikia asilimia 8.7 kutoka asilimia 9.3
Aidha, amesema uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma za jamii kutoka mwezi Septemba 2010 hadi Juni 2014 umeongezeka hadi shilingi 67 na senti 12 kutoka shilingi 66 na senti 72 za mwezi Mei mwaka huu.
“Kupungua kwa bei ya bidhaa kwa mwezi Juni kunamaanisha kwamba, uwezo wa fedha yetu umeongezeka,hii inamaanisha mfumuko wa bei unaposhuka, thamani ya shilingi nayo inapanda” Amesema.
Kuhusu ulinganifu mfumuko wa bei wa Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki amesema kuwa una mwelekeo unaofanana na kueleza kuwa mfumuko wa bei nchini Kenya umeongezeka na kufikia asilimia 7.39 kwa mwezi Juni 2014 ikilinganishwa na asilimia 7.30 za mwezi Mei , huku Uganda ikiwa na mfumuko wa asilimia 4.9 kwa mwezi huu ikilinganishwa na 5.4 za mwezi uliopita.

No comments: