Thursday, August 28, 2014

MICHEZO--HIVI NDIVYO EMMANUEL OKWI ALIVYOREJEA SIMBA




Mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi akitambulishwa na mwenyekiti wa kamati ya usajili ya klabu ya Simba Zakaria Hans Pope.
Staili ile ile waliyotumia mahasimu wao Dar es salaam Young Africans kumpata mshambuliaji mganda Emmanuel Arnold Okwi ndiyo ambayo klabu yake ya zamani, wekundu wa Msimbazi Simba SC imeitumia kumrejesha kundini Mganda huyo hii leo
“Tumewaandikia barua TFF kuomba kumtumia mchezaji huyu kwa muda wakati kesi yake na Yanga inaendelea, tumeambatanisha na barua yake ambayo yeye anatuomba kucheza kwetu kulinda kipaji chake,”amesema Poppe.


Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba wamemsaini mchezaji huyo baada ya kupitia kwa kina suala lake na Yanga SC na kugundua haki ipo upande wa mchezaji
“Baada ya kulipitia suala lake na Yanga kwa undani kabisa na vielelezo ambavyo mchezaji mwenyewe ametupatia, tumejiridhisha tuko sahihi kumsaini ili acheze mpira kunusuru kipaji chake kipindi hiki ambacho ana matatizo na Yanga SC,”amesema Poppe
Tayari Simba SC imetuma jina la mchezaji huyo katika usajili wake TFF na ataungana na mganda mwenzake, Joseph Owino, Warundi Pierre Kwizera na Amisi Tambwe na Mkenya, Paul Kiongera katika wachezaji watano wa kigeni
Kwa upande wake Okwi ambaye ameahidi makubwa msimu huu mara baada ya kurejea hii leo alianza kuichezea Simba kwa mara ya kwanza akiwa kinda wa miaka 17 akitokea Sports club Villa ya Uganda mnamo mwaka 2009 kabla ya Januari mwaka jana kuuzwa kwa dola za Kimarekani 300,000 Etoile du Sahel ya Tunisia
Etoile haikulipa fedha hizo Simba SC na baadaye ikaingia kwenye mgogoro na Okwi, aliyedai hakulipwa pia mishahara yake kwa miezi mitatu na hivyo Okwi akawafungulia Etoile kesi FIFA na akaomba wakati mgogoro wao unaendelea, aruhusiwe kuchezea timu yoyote kulinda kipaji chake, ndipo akajiunga na SC Villa ya kwao
Akiwa SC Villa ndipo aliposaini Yanga Desemba mwaka jana na pamoja na mapingamizi yaliyoanzia ndani, na baadaye klabu yake, Etoile- lakini Okwi aliidhinishwa kuichezea timu hiyo ya Jangwani
Okwi aliichezea Yanga SC mechi 11 na kuifungia mabao matano- lakini kuelekea mechi tano za mwisho za Ligi Kuu msimu uliopita akaingia kwenye mgogoro na klabu hiyo
Okwi alisusa kushinikiza amaliziwe fedha zake za usajili na mgogoro wao umeendelea huku mchezaji huyo akiwa amesusa tangu mwezi Machi, ikiwa ni miezi minne tangu asajiliwe.
Lakini majaliwa ya mshambuliaji huyo mwenye kasi ya kutisha na uwezo wa kufumania nyavu kuichezea Simba kwa sasa yako mikononi mwa TFF na FIFA.


No comments: