Friday, October 3, 2014

MAANDAMANO YA BAWACHA YAPIGWA MARUFUKU NA POLISI

                      JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
JESHI LA POLISI TANZANIA




KUSITISHA KUFANYA MAANDAMANO YA AMANI TAREHE 04/10/2014 BARAZA LA WANAWAKE WA CHADEMA (BAWACHA) KWENDA IKULU

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limepokea taarifa kwa maandishi toka Baraza la Wanawake la CHADEMA (BAWACHA) yenye kusudio la kufanya maandamano ya amani kuelekea IKULU kwa nia ya kumwomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Jakaya Mrisho Kikwete asipokee RASIMU YA KATIBA.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum limefanya utafiti wa kina juu ya jambo hili na kugundua mambo yafuatayo: 


1.    Kwa vile kusudio la kufanya maandamano ya Amani kwenda Ikulu ni kupeleka ujumbe wao wa kumwomba Mhe. Rais asipokee Rasimu ya Katiba, hawakutoa sababu za msingi za kisheria kwa nini asipokee Rasimu hiyo.

2.    Kutokana na sheria ya mabadiliko ya Katiba Sura ya 83, hakuna mtu; chombo; au taasisi yeyote yenye uwezo kisheria kuzuia mchakato wa kupatikana Katiba.

3.    Mnamo tarehe 01/10/2014 katika Sherehe za ufunguzi wa Barabaara ya Bagamoyo-Tegeta ambayo ilihudhuriwa na Mbunge wa Kawe Mh Halima Mdee ambaye pia ni Mwenyekiti BAWACHA – Taifa, alipewa fursa na Mhe. Rais aende akamwone Ikulu juu ya masuala mbali mbali yanayohusiana na Katiba au BAWACHA.  Anashauriwa atumie fursa hiyo ya kumwona Mhe. Rais kumweleza masuala ya Katiba pamoja na BAWACHA na siyo maandamano.

4.    Suala la Maandamano katika kipindi hiki cha mchakato wa kupatikana Katiba, halina nafasi na litaleta uvunjifu wa Amani kwa vile linagusa watanzania wote bila kujali itikadi zao.  Aidha, katika barua yao waliomba maandamano hayo yaanzie ofisi za CHADEMA Makao Makuu kinondoni kupitia barabara za Kinondoni, Ally Hassani Mwinyi, Sea View, Ocean Road hadi Ikulu. Maandamano ya aina hiyo yatasababisha usumbufu kutokana na msongamano wa magari na watu.

Kutokana na sababu zilizotajwa hapo juu, Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Polisi D’Salaam amezuia maandamano haya chini ya Kifungu 43 (1-6) cha sheria za Polisi na Polisi Wasaidizi sura 322 kama ilivyorekebishwa mwaka 2002.  Hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka amri hii.
Kama hawajaridhika na maamuzi hayo wanashauriwa kukata rufaa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi chini ya Kifungu 34 (6) cha sheria niliyotaja hapo juu.


POLISI WAIMARISHA USALAMA WAKATI WA SIKUKUU YA IDD EL HAJI - 2014.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeweka mikakati ya mpango kazi kama ifuatavyo:-
·        Limepanga kushirikiana na vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama ikiwa ni pamoja na Kikosi cha Zimamoto na uokoaji, Kampuni binafsi za ulinzi, Vikosi vya uokoaji wakati wa majanga, na vikundi vya Ulinzi Shirikishi ili kuhakikisha kuna udhibiti wa matukio ya uhalifu au fujo zinazoweza kujitokeza.


·        Tumejipanga kutumia Kikosi cha FFU kikijumuisha askari na magari ya washawasha, Askari wa Mbwa na Farasi. Kikosi cha Polisi Wanamaji nacho kitakuwepo. Pia Vikosi vya Kuzuia Dawa za Kulevya, askari wa kawaida (GD), askari wa Usalama Barabarani, na askari Makachero. Wote hawa wamepewa maagizo maalum ya kuchukua hatua kabla matukio ya uhalifu hayajajitokeza na sio kungoja tukio lifanyike. Kwa mantiki hiyo, dalili zozote za uvunjifu wa amani litashughulikiwa bila kuchelewa.

·        Zitakuwepo doria za Miguu na doria za pikipiki  katika barabara zote muhimu.

·        Sambamba na hatua hizo, vikosi vyote vya Polisi vikihusisha askari wa vyeo vyote vitakuwa barabarani.


·        Wananchi wanashauriwa kusherehekiea siku ya IDD EL HAJ katika ngazi ya familia au kukusanyika katika mitaa wakisherehekea kwa amani  na utulivu.

·        Aidha kutokana na sababu za kiusalama na matishio mbalimbali katika ukanda wa Afrika ya Mashariki, Jeshi la Polisi limepiga marufuku disko toto katika kumbi mbalimbali kutokana na sifa za kumbi hizo kutokidhi viwango vya kiusalama.


·        Wananchi wanapoona dalili zozote au maandalizi ya uvunjifu wa amani watoe taarifa mapema iwezekanavyo katika vituo vya Polisi vya karibu ili hatua zichukuliwe kwa haraka.

·        Aidha, madereva wanatakiwa kuzingatia sheria za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kutoendesha vyombo vya moto kwa mwendo kasi, kutoendesha vyombo hivyo wakiwa wamelewa, magari au pikipiki zenye sauti kali/zenye kuleta mshtuko nazo ni marufuku.


·        Aidha, Kikosi cha Polisi Wanamaji (Marine Police) kitafanya doria kwenye fukwe za Bahari na maeneo yote ya Bahari jijini Dar es Salaam.


·        Polisi watatoa ulinzi katika fukwe za bahari, kwa kuweka vituo vya Polisi vya muda vinavyohamishika (Mobile Police Station) ili kutoa msaada wa haraka pindi unapohitajika. Pia askari wa kutosha watakuwepo kuhakikisha wananchi wanasherehekea kwa amani. 


·        Aidha, kwa urahisi wa mawasiliano wananchi wasisite kutoa taarifa za uhalifu kwa namba muhimu za simu zifuatazo:      
1.    RPC ILALA:    MARY NZUKI – SACP                 0715 009 980
2.    RPC TEMEKE: KIHENYA – SACP                               0715 009 979
3.    RPC K’NDONI:CAMILLIUS WAMBURA – ACP     0715 009 976
4.    AMIR KONJA - ACP  0764 168 772 (Mkuu wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalum Dar es Salaam).

ZINGATIA: “Utii wa Sheria bila Shuruti”

“NAWATAKIA NYOTE HERI YA IDD EL HAJ - 2014”.


S. H. KOVA
KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM

DAR ES SALAAM

No comments: