Wednesday, October 8, 2014

MFUMUKO WA BEI NCHINI WAPUNGUA

Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Ephraimu Kwesigabo akitoa taarifa ya mfumuko wa bei nchini kwa mwezi Septemba, 2014 leo jijini Dar es salaam. Kulia ni Meneja wa Takwimu za Ajira na Bei wa Ofisi hiyo Bi. Ruth Minja.
Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Septemba 2014 umepungua hadi kufikia asilimia 6.6 kutoka asilimia 6.7 iliyokuwepo mwezi Agosti kutokana na kupungua kwa bei ya bidhaa na huduma katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Bw. Ephraim Kwesigabo amesema kuwa bidhaa za vyakula zikiwemo mchele, mahindi, ulezi, matunda, Sukari na vinywaji baridi zimechangia kupungua kwa mfumuko wa bei nchini
Bidhaa nyingine zilizochangia kupungua kwa mfumuko wa bei nchini ni Sare za shule, Simu za mkononi, runinga na viatu huku akibainisha kuwa Fahirisi za bei kwa maana ya kipimo kinachotumika kupima mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zinazotumiwa na kaya nchini zimeongeka na kufikia 149.93 kwa mwezi Septemba 2014 ikilinganishwa na 140.61 za mwezi Septemba mwaka jana.


Kwa upande wa mfumuko wa bei unaopimwa kwa kipimo cha mwezi ameeleza kuwa umeongezeka kwa asilimia 0.4 kwa mwezi Septemba 2014 ikilinganishwa na asilimia 0.1 za mwezi Agosti kutokana na kuongezeka kwa Fahirisi ya baadhi ya bidhaa zikiwemo samaki, matunda, mbogamboga, mihogo na vinywaji baridi, mkaa, mazulia na dawa za Binadamu kuwa na mchango mkubwa katika ongezeko la fahirisi.

Aidha, amesema mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula nyumbani na migahawani umepungua hadi asilimia 8.3 mwezi Septemba 2014 kutoka asilimia 8.5 za mwezi Agosti 2014 na kuongeza kuwa uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma za jamii kwa mwezi Septemba, 2014 umefikia shilingi 66 na senti 70.

Kwa upande wa mfumuko wa bei wa Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki Bw. Kwesigabo amesema kuwa una mwelekeo unaofanana, Kenya ukipungua na kufikia asilimia 6.6 mwezi Septemba kutoka 8.34 za mwezi Agosti huku Uganda ikiwa na mfumuko wa bei wa asilimia 1.4 mwezi Septemba kutoka asilimia 2.8 za mwezi Agosti.

No comments: