Saturday, December 20, 2014

STORY SABA MUHIMU KUTOKA TFF LEO

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjXUR7CiO4NZCj7Vt-LcaOkJ-glNBK7ycVnO7nsTGRzMBy2g2u1VWgUKOPLuzvqBK1-rwQGTpil_6k5Rkn0-DwzbwvdbdG-WAuH3dkkhXNxrEd4DXbElEkZYXZmFt-tV-VzR0PvnezgtPX6/s1600/MMG28673.jpgMATUMIZI YA TIKETI ZA ELEKTRONIKI
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana jana (Desemba 19 mwaka huu) jijini Dar es Salaam, imezingatia upungufu uliopo katika utekelezaji wa matumizi ya tiketi za elektroniki.

Hivyo, Kamati hiyo imeiagiza Sekretarieti ya TFF kuwasiliana na benki ya CRDB inayoendesha mfumo huo wa matumizi ya tiketi za elektroniki kuhusu upungufu huo na kuhakikisha unafanyiwa kazi.


MAREKEBISHO YA KATIBA YA TFF
Kamati ya Utendaji ya TFF imerejea mazungumzo kati yake na ujumbe wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) uliokuwa nchini ukiongozwa na Meneja wa Vyama Wanachama wa FIFA, James Johnson.  

Mazungumzo hayo kuhusu Katiba ya TFF yalifanyika Desemba 18 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Kamati ya Utendaji inasubiri rasimu ya Katiba hiyo kutoka FIFA ili iweze kufanya utaratibu wa kuwaarifu wanachama wake juu ya maudhui ya rasimu hiyo.

Shughuli ya FIFA kurekebisha katiba za nchi wanachama wake inaendelea duniani kote, na kwa Afrika kazi hiyo imekamilika katika nchi za Namibia, Zimbabwe na Malawi.

USHIRIKIANO KATI YA TFF NA SAFA
Kamati ya Utendaji imepitia na kupitisha makubaliano ya ushirikiano kati ya TFF na Chama cha Mpira wa Miguu Afrika Kusini (SAFA).

Makubaliano hayo ni ushirikiano katika nyanja za mpira wa miguu wa vijana, maendeleo ya waamuzi, ufundi, menejimenti ya matukio (event management) na utafutaji udhamini (sponsorship).

KANUNI ZA LESENI ZA KLABU (CLUB LICENSING REGULATIONS)
Kamati ya Utendaji imejadili rasimu ya Kanuni za Leseni za Klabu (Club Licensing Regulations), na kuagiza Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ifanye marekebisho ya mwisho, kabla ya kanuni hizo kusainiwa na kuanza kutumika.

UANZISHAJI MFUKO WA MAENDELEO YA MPIRA WA MIGUU (FDF)
Kamati ya Utendaji imepokea taarifa ya maendeleo ya mchakato wa uanzishwaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (Football Development Fund- FDF).

Imeipongeza Kamati ya Mfuko huo inayoongozwa na Rais wa zamani wa TFF, Leodegar Tenga, na kuitaka fanye jitihada za kukamilisha rasimu ya kanuni za uendeshaji mfuko huo.

Mbali ya Tenga, wajumbe wengine wa mfuko huo ni Ayoub Chamshama, Ephraim Mafuru, Frederick Mwakalebela, Tarimba Abbas na Zarina Madabida. Sekretarieti ya mfuko huo inaundwa na Henry Tandau ambaye ni Katibu, Wakili Emmanuel Muga na Boniface Wambura.

FDF ambao ni mfuko utakaokuwa unajitegemea utakuwa unashughulika na maendeleo ya mpira wa miguu kwa vijana, na nyanja nyingine za maendeleo kwa mchezo huo.

MKUTANO MKUU KUFANYIKA SINGIDA MACHI 14
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imepanga Mkutano Mkuu wa Kawaida wa mwaka ufanyike Machi 14 na 15 mwakani mjini Singida.

MGOGORO NDANI YA ZFA
Kamati ya Utendaji imepokea kwa masikitiko taarifa za masuala ya mpira wa miguu Zanzibar kupelekwa mahakamani.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kitendo hicho ni kinyume cha taratibu za uendeshaji mpira wa miguu ambazo zinakataza masuala ya mchezo huo kupelekwa katika mahakama za kawaida.

Kamati ya Utendaji inatoa rai kwa pande zote mbili zinazohusika na mgogoro huo kukaa kwenye meza ya mazungumzo ili kumaliza tofauti zao.

Kamati ya Utendaji imejitolea kutuma ujumbe wake Zanzibar ili ukutane na pande zinazohusika katika mgogoro huo.

Ni muhimu usuluhisho upatikane haraka ili tuweze kujua hatma ya washiriki wetu kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments: