Friday, January 16, 2015

DIEGO GUTIERREZ KUONDOKA TIGO TANZANIA NA KUPANDISHWA CHEO MILLICOM


Meneja Mkuu wa Tigo, Deigo Gutierrez (kulia), anayeachia nafasi yake baada ya kuitumikia kampuni kwa miaka mitano, akiwa katika picha na mrithi wake Bi. Cecile Tiano ambaye atakuwa Kaimu Meneja Muendeshaji wa Tigo. Gutierrez amepandishwa cheo kuwa Mkuu wa Huduma za Kutuma na Kupokea Fedha kwa bara la Latin Amerika.
Tigo imetangaza leo kwamba Meneja Mwendeshaji wa kampuni hiyo, Diego Gutierrez, atang’atuka kutoka katika nafasi yake Aprili 1 mwaka huu kwa ajili ya majukumu mengine aliyopewa katika kampuni mama ya Tigo kimataifa, Millicom. Nafasi yake itakayoachwa wazi itachukuliwa na Mkurugenzi Mwendeshaji wa muda Bi. Cecile Tiano atakaye anza kazi nchini wiki hii.

Bw. Gutierrez amepata mafanikio makubwa kuongoza kampuni ya Tigo Tanzania akitokea Ghana mwaka 2009. Alijiunga na Tigo Tanzania kwanza kama Naibu Meneja Mwendeshaji na baadaye akapandishwa cheo kuwa Meneja Mwendeshaji kamili kuanzia mwaka 2012 hadi sasa, na siku zote amekuwa kiungo muhimu katika kuleta maendeleo ya Tigo. 
Katika muda wake, kampuni imekuwa kwa zaidi ya asilimia 100% kufikia  idadi ya wateja milioni 8, pia imesambaza huduma ya kasi ya mtandao 3G, pamoja na huduma ya kutuma na kupokea fedha, vilevile imekuwa kampuni inayoongoza kwa ubunifu kwa kuleta huduma na bidhaa mbali mbali kama Facebook ya bure, wateja kupewa gawio kupitia Tigo Pesa, utumaji na upokeaji wa fedha kwa urahisi zaidi kati ya Tigo na makampuni mengine ya simu, pamoja na huduma ya kutuma na kupokea fedha kati ya Tanzania na nchi za jirani iliyo na uwezo wa kubadilisha ankara ya fedha moja kwa moja. 

Kwa utaalamu huo katika huduma ya kutuma na kupokea fedha, Bw. Gutierrez anapandishwa cheo na kuwa Mkuu wa Huduma za Kutuma na Kupokea Fedha kwa bara la Latin Amerika. 

Bi. Cecile Tiano anajiunga na menejimenti ya Tanzania akitokea kuwa Kaimu Meneja Muendeshaji wa Tigo nchini DR Congo. Kabla ya hapo alikuwa mshauri wa kitalaam kwa kampuni za Tigo Ghana na Tanzania akiwa na uzoefu  wa kufanya kazi kama afisa mwandamizi katika sekta za mawasiliano, habari na intanet.

Akizungumzia kuhusu mabadiliko haya, Makamu Afisa Mtendaji Mkuu wa Millicom kwa bara la Africa Bw. Arthur Bastings alisema kwamba, “Diego amefanya kazi nzuri sana Tigo, ameweza kuleta ubunifu wa kipekee katika soko hili na kuanzisha huduma nyingi sana ambazo zimekuwa za kwanza kuzinduliwa duniani kutoka Tigo Tanzania. Kwa nafasi kubwa jitihada zake zimefanya Tanzania kuwa kinara duniani katika sekta ya Huduma na Kupokea fedha kwa njia ya simu na pia intanet imekuwa ya gharama nafuu kwa idadi kubwa ya watu nchini Tanzania.
 Tunamtakia kila la kheri katika nafasi yake mpya huku tukimkaribisha pia Cecile nchini Tanzania. Cecile ni afisa mwandamizi katika sekta ya biashara aliyeweza kupata mafanikio makubwa katika uzoefu wake wa kazi na nina imani kubwa kwamba ataendelea kuwapatia uongozi mzuri menejimenti ya Tigo Tanzania.” 


No comments: