MICHEZO24---TFF YATEMBEZA RUNGU KWA WACHEZAJI LIGI KUU


                       
WACHEZAJI WAWILI VPL, FDL WAPIGWA FAINI

     Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imewapiga faini na kuwafungia mechi wachezaji wawili wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa kufanya vitendo kinyume na kanuni zinazotawala ligi hizo.

      Mshambuliaji Haruna Chanongo wa Stand United amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 kwa kumpiga teke mwamuzi wa mechi dhidi ya Polisi Morogoro iliyochezwa Januari 3 mwaka huu Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 37(3) ya Ligi Kuu.


Kipa Amani Simba wa Oljoro JKT amepigwa faini ya sh. 300,000 kwa kukataa kupeana mkono na viongozi wakati wa kusalimia kabla ya kuanza mechi kati ya timu yake na Toto Africans iliyofanyika jijini Mwanza. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa kanuni ya 14 ya FDL.

Timu ya Polisi Mara imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki wake wakati wa mechi ya FDL dhidi ya Mwadui ya Shinyanga iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma. Pia Polisi Tabora imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki wake kwenye mechi namba 40 dhidi ya Geita Gold, adhabu ambazo zimetolewa kwa mujibu wa kanuni ya 41.

12 WAPELEKWA KAMATI YA NIDHAMU YA TFF
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limewapeleka wanamichezo 12 wakiwemo viongozi, makocha na wachezaji kwenye Kamati ya Nidhamu kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu kutokana na matukio mbalimbali kwenye Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na michuano ya Kombe la Taifa la Wanawake.

Wachezaji Dihe Makonga, Swalehe Idd Hussein, Ramadhan Mwinyimbegu na Shaibu Nayopa wa Oljoro JKT, na Nassib Lugusha wa Polisi Dodoma wanalalmikiwa katika Kamati ya Nidhamu kwa kushambulia waamuzi na kufanya vurugu kwenye benchi la timu pinzani katika mechi zao za FDL.

Mtunza Vifaa (Kit Manager) wa Polisi Mara, Clement Kajeri analalamikiwa kwa kuongoza mashambulizi dhidi ya waamuzi kwenye mechi kati ya timu yake na Mwadui iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma.

Naye Mtunza Vifaa (Kit Manager) wa Rhino Rangers, Albert Mbunji anapelekwa katika Kamati hiyo kwa kupinga maamuzi na kuwatukana waamuzi kwenye mechi dhidi ya Polisi Dodoma iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

Pia Mtunza Vifaa (Kit Manager) wa Oljoro JKT, Eliud Justine Mjarifu analalamikiwa kwa matukio mawili; alimpiga Kocha wa Burkina Faso, CR Mwakambaya kwenye mechi ya FDL iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Pia alimtukana mwamuzi akiba (fouth official) Mussa Magogo kwenye mechi dhidi ya Toto Africans iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Kocha wa Polisi Tabora, Kim Christopher analalamikiwa kwa kumtolea mlugha chafu mwamuzi wa mechi kati ya timu yake na Panone FC iliyochezwa Uwanja wa Ushirika mjini Moshi.

Msimamizi wa Kituo cha Musoma, Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mara (FAM), Mugisha Galibona naye anapelekwa katika Kamati ya Nidhamu kwa tuhuma za kutotoa ushirikiano kwa maofisa wa mechi na kuchochea maofisa hao (waamuzi) kupigwa.

Kwa upande wake, Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake ya TFF imependekeza Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Simiyu, Emmanuel Sologo, na Kaimu Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Singida (SIREFA), Gabriel Gunda kupelekwa kwenye kamati ya Nidhamu kwa matukio mbalimbali yaliyojitokeza kwenye mechi za Kombe la Taifa la Wanawake.

Sologo anatuhumiwa kumpiga kibao mwamuzi wa mechi ya marudiano kati ya timu yake ya Simiyu na Shinyanga iliyochezwa mjini Shinyanga, tukio ambalo lilimfanya mwamuzi huyo avunje mchezo.

Naye Gunda analalamikiwa kwa kushindwa kuhakikisha timu yake ya Singida inaingia uwanjani kwenye mechi ya marudiano dhidi ya Dodoma iliyokuwa ifanyike kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida.

SDL KUANZA MZUNGUKO WA PILI JANUARI 31
Mzunguko wa pili wa Ligi Daraja la Pili (SDL) sasa utaanza Januari 31 mwaka huu, badala ya Januari 24 mwaka huu kama ilivyopangwa awali ili kutoa fursa kwa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia usajili wa dirisha dogo.

Timu zinazocheza ligi hiyo katika makundi manne tofauti ni; Milambo FC, Mji Mkuu FC (CDA), Mvuvumwa FC, Singida United, na Ujenzi Rukwa (Kundi A),  Arusha FC, Bulyanhulu FC, JKT Rwamkoma FC, Mbao FC, na Pamba SC (Kundi B).
Nyingine ni Abajalo FC, Cosmopolitan, Kariakoo Lindi, Kiluvya United, Mshikamano FC, na Transit Camp (Kundi C), wakati Kundi D ni Magereza Iringa, Mji Njombe, Mkamba Rangers, Town Small Boys, Volcano FC, na Wenda FC.


IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

About HABARI24 TV

Post a Comment
Powered by Blogger.