Saturday, January 3, 2015

TAMKO LA POLISI MUDA HUU KUHUSU PANYA ROAD




                                 JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
                                                 WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
                                                               JESHI LA POLISI TANZANIA

                                                                                                    
                                                             03/01/2015.
                                                                                      
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ndugu zangu wanahabari;

Napenda nichukue fursa hii kutoa ufafanuzi wa taharuki iliyotokea jana tarehe 02 Januari, 2015 katika jiji la Dar es Salaam ikiwahusisha baadhi ya vijana wanaojikusanya kwenye vikundi na kujiita Panya road na pengine kusababisha hofu kubwa kwa wananchi.

Chanzo cha taharuki hiyo, kulitokana na kuuawa kwa kijana mmoja ajulikanae kwa jina la Mohamed Ayub na wananchi tarehe 01/01/2015 katika maeneo ya Tandale kwa Mtogole kwa tuhuma za wizi wakati wa mkesha wa sikukuu ya mwaka mpya. Tarehe 02/01/2015 majira ya saa tisa mchana yalifanyika mazishi ya kijana huyo katika makaburi ya Kihatu Kagera Mikoroshini na taarifa zilizokuwa zimelifikia Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam ni kwamba baada ya mazishi hayo vijana wenzake na marehemu walijipanga kufanya fujo ili kulipiza kisasi cha mwenzao kuuawa. Aidha, kabla vurugu hizo hazijafanyika na kwa vile Polisi walishaona dalili ya vurugu hizo, tayari walifanikiwa kuzidhibiti.

Baada ya vurugu hizo kudhibitiwa na Polisi, vijana hao walitawanyika kwa kukimbia katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam na kuzua taharuki kubwa kwa wananchi kwamba huenda kila walipokimbilia wanampango wa kuwafanyia fujo raia wema, jambo ambalo wasingeweza kulifanya kwa vile Polisi walikuwa wameimarisha ulinzi katika maeneo yote ya jiji.

Kufuatia hali hiyo na Jeshi la Polisi nchini likiwa linaendelea na msako mkali wa kuwabaini na kuwakamata wote wanaojihusisha na uhalifu huo, tunawaomba wananchi watulie, wasiwe na hofu na waendelee na majukumu yao kama kawaida. Mpaka sasa tunawashikilia watuhumiwa 36 kwa mahojiano na uchunguzi utakapokamilika tutawafikisha mahakamani mara moja.

Aidha, Jeshi la Polisi linatoa onyo kwa vijana hao wananojihusisha na vikundi hivyo kuacha tabia hiyo mara moja. Tumejipanga vizuri katika mikoa yote kuhakikisha kwamba nchi inaongozwa kwa kufuata utawala wa sheria, hatutamwonea muhali mtu yeyote ama kikundi cha watu wanaotaka kuvuruga amani ya nchi na kutia hofu wananchi.

Wananchi waendelee kutupa ushirikiano kwa kutoa taarifa kupitia namba ya simu 0754  78 55 57, namba za makamanda au katika kituo chochote cha Polisi.


Imetolewa na:-
Advera John Bulimba  - SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.








No comments: