Monday, April 27, 2015

KAMATA KAMATA DAR-WAZUNGU WAWILI WADAKWA KWA UTAPELI.SOMA HII

  
RAIA WATATU WA KIGENI WAKAMATWA KWA MAKOSA YA WIZI WA MTANDAO KATIKA MABENKI JIJINI DAR ES SALAAM.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watuhumiwa watatu raia wa kigeni kwa makosa yanayohusiana na wizi wa mtandao kwa lengo la kuiba  katika vyombo vya fedha kama mabenki, maduka ya kubadilishia fedha (Bureau de Change) au kuingilia miamala ya fedha zinazosafirishwa na wateja kutoka nje na ndani ya nchi.
Polisi wa kikosi Maalum cha kupambana na wizi wa mtandao (Cyber Crime) walipata taarifa za kuaminika kwamba watu hao watatu walikuwa katika mazingira ya kutiliwa mashaka na ndipo Polisi walienda Mtaa wa Mindu eneo la Upanga na kuwakamata. Watu hao walikutwa katika nyumba namba 416 iliyopo katika ghorofa ya nne na walitambuliwa kwa majina yafuatayo:
1.      FOTIOS S/O VOGIATZIS, Miaka 32, Mfanyabiashara, Mkazi wa Upanga, Raia wa nchini UGIRIKI mwenye Passport namba AK2669977.

2.      ATHANASIOS S/O VOGIATZIS, Miaka 30, Mfanyabiashara, Mkazi wa Upanga, Mkazi wa Ugiriki mwenye Passport namba AK3049876.

3.      PANAGIOTIS S/O ANGELIDIS,           Miaka 25, Mkazi wa Upanga, Raia wa UGIRIKI mwenye Passport namba AK2644930.
Watu hao watatu ambao ni raia wa nchini Ugiriki kumbukumbu zao zinaonyesha kwamba wamekuwa wakiingia na kutoka nchini Tanzania na kwenda nchi mbalimbali za Afrika na Ulaya katika namna ambayo inaonyesha kuwa ni wahalifu wa kimataifa kupitia mitandao.
Katika upekuzi watu hao wamekamatwa na vielelezo mbalimbali vinavyopashiria njama zao kama ifuatavyo:
1.      Muhuri mmoja wa kughushi ulioandikwa “Inspector General of Police DSM”



















2.     Nyaraka mbalimbali za kughushi za Polisi Tanzania zinazowasaidia  kwa lengo la kupata malipo ya bima nje ya nchi ambazo zina mihuri ya kughushi.


3.      Zimepatikana Kompyuta Mpakato (Laptops) zipatazo tisa ambazo watuhumiwa hawa huzitumia kwa ajili ya mawasilisano pamoja na uhalifu huo wa kimataifa.

4.      Zimekamatwa laini za simu za mkononi (Cheap) za kampuni ya simu ya Airtel ambazo baadhi zimetumika na nyingine hazijatumika.

5.      Aidha, zimekamatwa kadi mbalimbali za benki (Credit Cards) zipatazo 13 zinazotumika kutoa fedha, kuingiza fedha, au manunuzi mengine za ATM.
Pia watuhumiwa hao wamekamatwa na vitabu vitano vyenye kumbukumbu za majina, anwani, pamoja na namba za siri za wateja mbalimbali wa mabenki mbalimbali kutoka nchi za Tanzania, Zambia, Afrika Kusini, Kenya, Uingereza na Nigeria.
Uchunguzi ziadi unaendelea kuhusu raia hao watatu kutoka nchi ya Ugiriki ili kubaini mtandao wao na kugundua matukio mbalimbali ambayo wameyafanya.

TAHADHARI KWA WANANCHI NA WAGENI WENGINE

Pamoja na kuibuka na wimbi hili la wezi wa mtandao bado ni salama kuweka na kutoa fedha katika mabenki hapa nchini. Hata hivyo kutokana na wimbi hili la wizi kwa njia ya mtandao, ni muhimu sasa kuzuia uhalifu wa aina hii kwa ushirikiano kati ya wamiliki wa mabenki  na wateja wao.  Jeshi la Polisi linashauri (pamoja na maelekezo mengine ya benki) njia sahihi ya kwanza ya kuzuia ni kuhakikisha kwamba miamala yote inayofanyika katika akaunti za benki ni lazima ifahamike kwa mteja kwa njia zifuatazo:
1.      Mteja ajulishwe kwa simu ya mdomo ili kuthibitisha muamala.
2.      Mteja atumiwe ujumbe kwa kila muamala unaofanyika kupitia ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) kumjulisha mteja kiasi kilichotolewa, kiasi kilichoingizwa au makato au maingizo yoyote kwa muda ule ule.
Aidha tunawaomba wananchi waendelee kushirikiana na Jeshi la Polisi na wasikubali kutoa nambari za akaunti zao kwa watu wasiohusika au nambari zao za siri hata kwa mtu ambaye ni ndugu wa karibu sana.
Mara baada ya upelelezi kukamilika watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani.

S. H. KOVA,
KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM,
DAR ES SALAAM.



No comments: