Monday, May 25, 2015

HOTUBA YA MHESHIMIWA CECILIA DANIEL PARESSO (MB), MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI WIZARA YA KAZI NA AJIRA KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2015/2016


(Inatolewa kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge kanuni ya 99(9) toleo la mwaka 2013).


1.0        Utangulizi
Mheshimiwa Spika,

Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kunilinda na kunitunza ili niweze kutumikia Taifa langu. Napenda kuishukuru familia yangu kwa msaada mkubwa na uvumilivu hasa ninapokuwa katika shughuli zangu za kisiasa.
Mheshimiwa Spika,
Napenda kutumia fursa hii, kuwashukuru watanzania wote kwa kupokea na kulea harakati za mabadiliko nchini.Shukrani hizi za pekee ziwafikie wenyeviti wenza wa vyama vinavyounda UKAWA,Mh. Freeman Mbowe, Mh. Prof. Ibrahimu Lipumba, Mh. James Mbatia na Mh. Dr.Emanuel Makaidi. Vile vile, shukurani zangu ziwafikie Makatibu wakuu viongozi wa UKAWA; Mhe. Wilbrod P. Slaa, Mhe. Seif Shariff Hamad, Mhe. Masena Nyambabe na Mhe. Tozi Matwange. Sambamba na hao, shukurani zangu ziende kwa timu ya wataalamu wa UKAWA, viongozi, watendaji, wanachama na wapenzi wa vyama vyote vinavyounda UKAWA. Mwisho japo si kwa kumaliza shukurani zangu ziwaendee wabunge wote wa Kambi ya Upinzani bungeni wanaounda UKAWA kwa kazi nzuri ya kutetea na kusimamia maslahi ya wananchi wa Tanzania.  Aidha, bila kuwasahau watendaji wa Kambi ya Upinzani ambao wamekuwa ni msaada mkubwa katika utekelezaji wa shughuli zetu.
Mheshimiwa, Spika,
Napenda kuwashukuru kwa nafasi ya pekee wananchi wa wilaya ya Karatu na wananchi na wote wa mkoa wa Arusha kwa ushirikiano na imani kubwa kwangu wakati nikitekeleza majukumu kama mwakilishi wao. Niliahidi daima nitakuwa “Mtumishi wa watu, kwa Maslahi ya watu na kwa Maendeleo ya watu” na daima nitabaki kuwa hivyo. Ninawashukuru na nawaomba wazidishe imani hiyo kwangu kwani haiwezi kupotea bure. 
Baada ya Shukrani hizo napenda kuanza hotuba yangu kwa kunukuu maneno machache kutoka kwa Baba wa Taifa, ningependa watanzania kuyatafakari hususan kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi oktoba 2015;
“Na hakutakuwa na watu wa kizazi hiki na karne hii ambao watatakiwa kujitoa muhanga kwa ajili ya maisha bora katika siku zijazo wakakubali, wakati wanawaona watu wachache wakiendelea kuneemeka machoni pao bila kujali wakati ujao, wakati wananchi na watoto wao wakiendelea kuishi katika maisha duni na dhalili.”
UKOSEFU WA AJIRA NCHINI
Mheshimiwa Spika,
Kwa muda mrefu tumekua tukionesha jinsi ambavyo Serikali imekua haina mikakati endelevu ya kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira nchini. Aidha, Serikali ya CCM imekuwa ikitumia mikakati ya ‘kupaka mafuta kwa mgongo wa chupa’ kama nadharia iliyozoeleka kwa nia yenye kuwapumbaza wananchi kwa kuwapa matumaini yasiyo na matokeo chanya juu suala zima la utengenezaji wa ajira hapa nchini na hivyo kulifanya tatizo la ajira kuwa ni wimbo uliozoeleka ndani ya masikio ya watanzania. Hili ni jambo la aibu kwa nchi iliyojaliwa utajiri mkubwa wa maliasili na rasilimali.
Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere amewahi kutamka maneno yafuatayo;
Amini nawaambieni enyi waswahili wachache mnaotawala; mnategemea kweli kuwa mtawaongoza watanzania kwa lazima wakati wamepoteza matumaini, na mtegemee kuwa wanasalia wamekaa kimya kwa amani na utulivu?”(Reflections on Leadership in Africa -VUB –University Press, 2000)
Mheshimiwa Spika,
Mwelekeo wa uongozi wa mazoea na wa kuongoza na kuamua mambo kwa matukio ni kuonesha jinsi gani Serikali ya CCM ilivyochoka na kwamba inahitaji kukaa pembeni na kujifunza namna ya kuongoza nchi kwa viwango vya uwajibikaji wenye maslahi mapana kwa jamii ya watanzania. Serikali ya CCM imeshindwa kuzioanisha Sera, Sheria, Mikakati na mipango mbalimbali ambayo kwa pamoja ingeweza kutatua matatizo sugu ya ukosefu wa ajira nchini. Ni Serikali hii ambayo, imeua falsafa ya kujitegemea ‘self reliance’ ambayo Baba wa Taifa aliipigania kwa ajili ya watanzania wote. Je, ni kiongozi yupi wa CCM atakayeweza kusimama na kusema kuwa Serikali ya CCM imekua mdau nambari moja wa azimio la Arusha? Je ni nani kati yenu anayeweza kusema mfumo wa elimu tulionao leo unampa mhitimu uwezo wa kujitegemea? Ni nani anaweza kusimama na kueleza mafanikio ya Serikali ya CCM kuhakikisha kuwa kilimo alichokipigania Baba wa Taifa kinatoa ajira kwa makundi yote? Je, ni nani kati yenu atakayeweza kusimama na kujinasibu kuwa vyuo vikuu mlivyojenga kwa fedha za wachangiaji ambao wengi ni wafanyakazi na wakulima wa nchi hii vimemuandaa mtanzania kukabiliana na changamoto za ajira?
Mheshimiwa Spika,
Serikali yoyote katika hali halisi ya kiutendaji na utawala, itakuwa na walakini kama itaangalia tu utawala au mfumo bila kujielekeza kuangalia pia mchakato mzima katika utawala na mfumo wake. Ni wazi kwamba, Tanzania inahitaji kufanya mageuzi makubwa kwa sababu nchi inahitaji mabadiliko na hii ni kwa kuwa serikali hii inayoongozwa na CCM ina mambo ambayo hayaendani na kasi ya mabadiliko ya sasa ya kidunia.
Mheshimiwa Spika,
Pamoja na kwamba Serikali ya Tanzania inayoongozwa na CCM  kuwa na utaratibu wake, hakika huu ni utaratibu wa kushindwa kuendana na mahitaji ya kiuchumi na kijamii ya watu wake, utaratibu wa kushindwa kuleta maendeleo kwa watu wake, utaratibu wa kushindwa kuleta maendeleo ya amani kwa watu wake na taratibu nyinginezo zenye kunyonya nguvu za watu wake.
Hivyo basi, Serikali ya UKAWA itakapoingia madarakani  imekusudia kudhibiti na kuondoa changamoto hizi kwa kuhakikisha kuwa wananchi wa taifa hili la Tanzania wanatengenezewa ajira za kutosha na  wanaishi na kufanya kazi kwa amani na utulivu na kuondoa umaskini, kuhakikisha kuwa watu wanaishi kwa uhuru na wanafurahia haki za msingi za kidemokrasia na  kwa ufanisi mkubwa, kuhakikisha kuwa mfumo wa uendeshaji serikali kiutawala na kisiasa unaleta maendeleo endelevu ya kiuchumi, na zaidi, mabadiliko hayo ya kiuchumi yanafikiwa katika nchi hii yenye utajiri mkubwa wa rasilimali.
Mheshimiwa Spika,
Katika historia ya sasa; Tanzania imekuwa chini ya utawala wa sheria uliovaa koti la shari, vitisho na mabavu chini ya CCM, na sasa watanzania wanatambua juu ya matokeo ya utawala wa namna hiyo. Hata hivyo, tangu uhuru, watanzania wamekuwa wakiishi kwa pamoja  na kujenga urafiki na ushirikiano baina yao, serikali na  watu wa nchi nyingine katika msingi wa amani.
Mheshimiwa Spika,
Kauli hiyo ya utawala wa sheria uliovaa koti la shari, vitisho na mabavu unadhihirishwa pia na kauli za Kiongozi wa nchi alizowahi kuzitoa huko nyuma Mwezi Mei 2010 alisema:
“.....wafanyakazi wanaotaka kugoma waache kazi.....kwa kuwa kuna watu wengi wanahitaji kazi....”
Mheshimiwa Spika,
 Ni ukweli usiopingika kwamba “soko la ajira” Tanzania limefurika wanaotafuta kazi; lakini si kweli kwamba watu wote wanaotafuta kazi wanasifa stahiki kwa kila kazi. Kiongozi yeyote awaye mwenye mamlaka ya juu ya kiutendaji ana wajibu wa kuchagua maneno yenye hekima; kwa kuwa “hekima ni uhuru”. Wafanyakazi wanapodai haki zao ni vema wasijione wanyonge mbele ya “Mwajiri Mkuu”
Mheshimiwa Spika,
Naomba pia nitumie fursa hii kunukuu maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere aliyoyatoa Dar es Salaam kwenye sherehe za Mei mosi mwaka 1974:
“......tulipoanzisha vyama wafanyakazi, na halafu baada ya uhuru kwa uamuzi wa serikali ya TANU, wafanyakazi wa Tanzania wamelindwa wasinyonywe na matajiri wao, watu binafsi, na hata mashirika ya umma. Na ulinzi huo umezidishwa siku hata siku. Kima cha chini cha mishahara kimewekwa na kimekuwa kikiongezwa mara kwa mara. Sasa ni vigumu sana kumfukuza mfanyakazi, na kila mfanyakazi apate heshima yake kama binadamu......” (Julius K.Nyerere (1974): UHURU NI KAZI, National Printing Company Ltd, Dar es Salaam, ukurasa 15)”
Mheshimiwa Spika,
Kauli ya Baba wa taifa  inatufundisha msimamo wa viongozi wanaojali maslahi ya wafanyakazi na watu wao kwa ujumla na kuwahakikishia wafanyakazi :(1)ulinzi wa ajira zao dhidi ya unyonyaji unaofanywa na matajiri, watu binafsi, na mashirika ya umma; (2) kuweka kima cha chini cha mshahara na kukiongeza kila mara kuendana na mwenendo wa uchumi;(3) kuondoa vitisho vya wafanyakazi kufukuzwa na waajiri;(4)kuwapa wafanyakazi heshima yao kama binadamu[ibara ya 12(2), Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977(2005)]
Mheshimiwa Spika, kauli za viongozi zisizokidhi matarajio ya wafanyakazi zinazotolewa katika siku za dhama hizi zinaonesha wazi kuwa leo wafanyakazi wa Tanzania si kama “Enzi za Mwalimu.” Soko la ajira limewapa nafasi matajiri, watu binafsi, mashirika ya umma na serikali (yenyewe) kunyonya jasho la wafanyakazi, kuendesha vitisho, kulipa mishahara isiyokidhi maisha (na mafao duni ya uzeeni na/au kiinua mgongo), vitisho vya kufukuzwa kazi, na ukosefu wa heshima kwa wafanyakazi! Inawezekana haya ni matunda ya kuliua Azimio la Arusha na mahala pake kuliweka “Azimio la Zanzibar”
Mheshimiwa Spika,
Utawala usiozingatia maslahi ya wafanyakazi wake kwa kiwango cha juu kwa jinsi unavyoendeshwa na CCM, unazuia amani na maendeleo ya pamoja.Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na washirika wake (UKAWA) wanatambua kuwa amani na utulivu katika nchi yoyote hujenga na kuleta maendeleo ya kitaifa na hatimaye maisha bora kwa watu wake, hali kadhalika amani katika dunia inalinda maendeleo ya pamoja na ustawi wa watu wote na mgawo halali katika mafanikio ya maendeleo yao. Katika njia ya kujenga jamii yenye demokrasia yenye mpangilio mzuri na wa kuridhisha,UKAWA watakapotwaa mamlaka ya kuongoza nchi hii watachukulia umuhimu wa kwanza masuala ya maendeleo na ushirikiano na wananchi wa Tanzania na kutambua kuwa ajira na ujira wenye staha ni njia muhimu ya kujenga jamii yenye ustawi wa kisasa.
UKUAJI WA SEKTA YA AJIRA
Mheshimiwa Spika, Mwalimu Nyerere aliwahi kusema:
“To measure a country’s wealth by its gross national product is to measure things, not satisfaction.”[1]
Kwa maana isiyo rasmi ya Kiswahili anasema:
 “Kupima utajiri wa nchi kwa kutumia pato lake (yaani maana ya namba ya GNP), ni kupima vitu na si mahitaji toshelezi ya wananchi wake”.
Mheshimiwa Spika,
 Ukuaji wa Uchumi na Uzalishaji wa Ajira (Economic growth and Employment creation) ni vitu viwili ambavyo haviwezi kutenganishwa katika mahusiano yake. Katika hotuba ya Waziri Mkuu, inaeleza kuwa ‘kwa mwaka 2014, uchumi ulikua kwa asilimia 7.0 ikilinganishwa na asilimia 4.7 mwaka 2006, ukuaji ambao ni mzuri ikilinganishwa na nchi nyingi zinazoendelea’. Lakini ni vizuri kujua kuwa umekuwa ukikua bila kuzalisha ajira nyingi na bila kupunguza umaskini. Hii inatokana na aina ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania. Sekta zinazokua kwa kasi ni zile zinazotumia mashine na mitambo ambazo ukuaji wake kwa asilimia katika mabano ni ujenzi(14.1), usafirishaji na uhifadhi(12.5), fedha na bima(10.8) na nyinginezo.Sekta zinazotumia mashine na mitambo haziajiri wafanyakazi wengi kama zile zinazotumia misuli mfano kilimo, uvuvi, na ufugaji. Kilimo kilikua kwa asilimia 3.4 tu. Pia Sekta zilizokua kwa kasi hazina mwingiliano na sekta zisizokua. Jambo lingine linaloweza kufanya ukuaji wa uchumi usipunguze umaskini ni mgawanyo mbovu wa wa sehemu ya uchumi iliyokua.
Mheshimiwa Spika,
Kimsingi, bajeti lazima zizingatie si tu kukua kwa uchumi bali pia kuhakikisha kuwa ukuaji huu unakuwa shirikishi, unazalisha ajira na kupunguza umaskini. Ni muhimu pia kusisitiza ukuaji wa kijani (green production growth) ambao ni ukuaji usioharibu mazingira (ikolojia).
Mheshimiwa Spika,
Maendeleo ya sekta binafsi na uwekezaji ni muhimu sana katika ukuaji wa sekta ya ajira na kujenga ustawi wa maisha ya watu. Japokuwa Bajeti ya Waziri Mkuu imezungumzia mambo mengi kuhusu maendeleo ya sekta binafsi, ingekuwa vizuri kutambua mambo ya msingi katika sekta binafsi, Uchambuzi katika sekta binafsi unaonesha kuwa sekta hii si kitu kimoja, ina vipande vingi. Hivi ni pamoja na: sekta binafsi ya nje na ya ndani; sekta binafsi kubwa, ya kati na ndogo na sekta binafsi isiyo rasmi.Hatua za kibajeti lazima zitambue ukweli huu kuhusu sekta binafsi. Aina zote za sekta binafsi zikiwekwa katika kapu moja haitakuwa sahihi kwa maendeleo ya sekta hii hasa ile ya ndani, ndogo na isiyo rasmi. Ni vema CCM wakajiuliza maswali na kuachana na mazoea ya utengenezaji hotuba za bajeti kwa namna ambayo haitoi taswira halisia tena kwa fikra zile zile, za miaka ile ile na kwa ujanja ule ule.
Mheshimiwa Spika,
Aidha hatuwezi kupigia kelele ukosefu wa ajira bila kujielekeza katika kuangalia sekta ya uwekezaji. Suala kuu katika sekta ya uwekezaji ambayo CCM imekuwa ikipata ganzi kulifanyia kazi na kuchukua hatua makini za makusudi ni uboreshaji wa mazingira kwa wawekezaji wa ndani na nje, wakubwa kwa wadogo. Hatua mahsusi za kibajeti zinatakiwa katika kuleta na kuboresha mazingira rafiki na wezeshi ya uwekezaji ili kuongeza ajira na ustawi wa maisha ya watanzania.
Mheshimiwa Spika,
 eneo lingine ni maboresho katika sekta ya utalii yanaweza kujenga ajira nyingi kwa watanzania. Tayari sekta ya utalii ni mchangiaji mkubwa kwa uchumi wa Tanzania. Chapisho la Hali ya Uchumi wa Tanzania linalochapishwa Na Benki ya Dunia libainisha kwamba sekta ya utalii inaweza kukua na kujenga ajira zaidi, hususan katika ajira zinazolipa vizuri, pia inaweza kuunganisha biashara na wana jamii wa maeneo husika. Ili kutumia fursa hii, serikali inapaswa kupitia upya wajibu wake kwa kurahisisha mfumo wa kodi na ushuru, na kufanya mgawanyo wa mapato kuwa wazi zaidi.
Mheshimiwa Spika,
sekta ya utalii huajiri moja kwa moja taktribani watanzania nusu milioni na huchangia karibu asilimia 20 ya bidhaa zinazouzwa nje. Huwakilisha takribani asilimia 3.4 ya Pato Ghafi la Tanzania(GDP), lakini kiwango hiki kinaweza kufikia makadirio asilimia 10 unapochukuliwa mchango wake ambao si wa moja kwa moja katika sekta nyingine kama kilimo na uchukuzi. Pamoja na kwamba sekta ina lengo la kuongeza mapato yatokanayo na utalii mara nane ifikapo mwaka 2025, au kuongeza kiwango cha ukuaji wa sekta mara dufu kwa kila mwaka kama inavyoonekana katika miaka hivi karibuni, Lengo hili litafikika endapo tu kutakuwa na mabadiliko katika sera na mitazamo  miongoni mwa wadau wote.
Mheshimiwa Spika,
kama nilivyokwisha sema awali, bila kujenga uwezo wa kitaasisi katika sekta zetu mbalimbali hapa nchini ni vigumu kuzalisha ajira na kuleta maisha ya ustawi kwa watu wetu. Katika kuboresha sekta hii ya utalii ambayo ni moja ya sekta zenye mchango mkubwa wa ajira katika nchi yetu mambo kadhaa yanahitajika. Serikali itakayoundwa na UKAWA imejipanga (1) kupanua shughuli za utalii kuwa anuai tofauti na msisitizo wa sasa ambao unatoa umuhimu kwa watalii wa gharama kubwa katika kanda ya kaskazini na kuzunguka Arusha na Zanzibar ambako asilimia 90 ya shughuli za utalii ndiko ziliko sasa;(2)kuongeza juhudi za kuwaunganisha wana jamii wa maeneo husika na wafanyabiashara wadogo wa utalii katika shughuli za utalii, kupitia michakato ya kugawana faida.
Aidha, Serikali itakayoundwa na UKAWA itaandaa programu za mafunzo na kuunganisha jamii baina ya sekta za umma na binafsi, hii italeta viwango vya juu vya ubora wakati huo huo ikiongeza ushiriki wa wafanyabiashara na wafanyakazi wa maeneo hayo katika shughuli za utalii; na (3) Serikali yetu itafanya mapitio ya mfumo wa sasa wa kodi na ushuru ambao ni mgumu kuuelewa, mapitio hayo pia yatagusa usimamizi wa matumizi yasiyo ya wazi ya mapato yaliyokusanywa kutoka utalii. Vilevile, mfumo wa kodi na ushuru utafanywa kuwa rahisi na kutekelezwa kwa usawa zaidi kwa lengo la kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara na kuziba mianya ambayo inatoa nafasi kufanya malipo haramu. Aidha, mgawanyo wa mapato utarasimishwa ili uwe rahisi kufuatilia na kuongeza manufaa kwa wananchi walio wengi.
Mheshimiwa Spika,
Pamoja na kiwango cha ukuaji wa uchumi wa Tanzania kukua kwa asilimia 7 bado hakiakisi maendeleo halisi ya watu kwenye kaya zao. Hivi sasa maisha yako juu. Bei ya bidhaa na huduma mbalimbali za jamii, ziko juu. Kwa kifupi hali ya maisha ni ngumu. Kambi rasmi ya upinzani inaona kuwa tatizo kubwa la viongozi wa CCM ni kuona kuwa “wizara husika inapaswa kufa kivyake” bila kutambua na kuona pia jitihada za makusudi zinatakiwa kuchukuliwa ili kuwepo na “mfumo unaounganisha wizara, idara, wakala za serikali, na uongozi wa sekta binafsi kufanya kazi kwa umoja” utakaoweza kusaidia kujenga uwezo wa uelewa wa jinsi gani ajira zinaweza kutengenezwa katika nchi.
Serikali ya UKAWA inaahidi kuifanya Wizara ya Kazi na Ajira kuwa bunifu na kuioanisha na vitengo vingine vya utawala pamoja na wataalamu mbalimbali wa wizara zingine katika kufikia lengo la kuongeza ajira kwa watanzania.
Mheshimiwa Spika,
UKAWA tutakapopewa ridhaa ya kuongoza nchi hii tutahakikisha kuwa masuala ya kisera, kisheria na ya udhibiti yaliyo rafiki yanazingatiwa, kwa kuwa na bajeti zinazojikita katika maendeleo ya miundo mbinu kwa upana wake, kuondoa urasimu serikalini na kukuza rasilimali watu inayohitajika kwa sekta binafsi kuwa na ushindani wa kimataifa. UKAWA tutaweza kujenga mfumo imara utakaoweza kujenga uwezo katika utengenezaji wa ajira hapa nchini na kuipaisha Tanzania katika modeli za ukuzaji wa ajira ukilinganisha na hali ilivyo ya sasa ya kufanya kazi kwa mazoea bila kuendana na mabadiliko ya dunia ya sasa.
AJIRA KWA VIJANA
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, watu milioni 200 miongoni mwa wakazi wa Afrika ni vijana wenye umri kati ya miaka 15 na 24. Hii ni katika hali ambayo Umoja wa Mataifa unasema kuwa, idadi ya vijana wasio na ajira barani Afrika ni mara mbili zaidi ya watu wazima. Ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana unawafanya washawishike kujiunga na makundi yenye misimamo mikali tena kwa ujira mdogo tu au hata kwa hasira za kukata tamaa na maisha. Mfano wa hali hiyo unashuhudiwa katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Nigeria na Mali. Inaonekana kuwa, vijana wasio na ajira ni mawindo mazuri kwa makundi yenye kutishia amani. Leo hii siku za karibuni tumeshuhudia kijana wa kitanzania Rashid Charles Mberesero (21), akituhumiwa kuwa mmoja wa wanamgambo wa Al-Shabaab ambao walifanya mauaji katika Chuo Kikuu cha Garissa nchini Kenya na kuua wanafunzi 148. Haya ni matokeo ya kushindwa kwa mfumo wa utawala katika sekta ya elimu unaosimamiwa na Serikali ya CCM ambao ndio msingi wa kumuandaa kijana kifikra na hata kimtazamo.
Mheshimiwa Spika,
Ajira kwa vijana ni suala nyeti katika uchumi wa Tanzania.Ni bahati mbaya kuwa vijana wengi hawajaajiriwa katika sekta rasmi. Katika Hotuba ya Waziri Mkuu aliyoiwasilisha mnamo tarehe 12 Mei 2015 katika bunge hili ni kwa masikitiko makubwa haikueleza kabisa hali ilivyo hivi sasa. Hotuba ya Waziri Mkuu ingepaswa kueleza kwa nini hali iko hivi na nini kinafanyika kupambana na hali hiyo. Zipo sababu nyingi za vijana kutoajiriwa na kujiajiri ikiwa ni pamoja na upungufu wa nafasi za ajira na kukubalika katika soko la ajira. Upungufu huo na kutokubalika katika soko la ajira vina sababu zake ambazo bajeti ilipaswa kuelezea lakini imekaa kimya. Pia uwezo mdogo wa vijana kujiajiri ungepaswa kuelezewa pamoja na hatua zinazochukuliwa na ambazo zimeshachukuliwa miaka ya nyuma.
Mheshimiwa Spika,  wakati wa majadiliano ya bajeti ya wizara ya kazi na ajira mwaka jana tarehe 24 Mei 2014, Waziri Kabaka alielezea kuwa vijana wa kitanzania hasa wahitimu wanategemea kuajiriwa serikalini na mashirika binafsi na hawako tayari kujiajiri. Haya ni ghiriba kwa watoto wa masikini na waziri anapaswa kufuta kauli yake kwa kuwa inavyoonekana leo hii kuwa ni watoto wa vigogo pekee ndio wana haki ya kupata ajira serikalini na watoto wa kimasikini ndio wajiajiri.

Mheshimiwa Spika,
Ajira 200 za uhamiaji zilitangazwa Februari 17, mwaka 2014 ambapo watu 15,707 walijitokeza kuwania nafasi hizo 200, miongoni mwao, waombaji 1,005 waliitwa kwenye usaili na 200 waliothibitishwa waliitwa kazini. Hata hivyo, baada ya tangazo la kuitwa kazini malalamiko yaliibuka kupitia vyombo vya habari na baadhi ya mitandao ya kijamii, kwamba baadhi ya walioitwa katika ajira hizo walikuwa ni watoto, jamaa na ndugu wa maofisa wa Idara ya Uhamiaji.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa si kosa kwa ndugu na jamaa kuajiriwa katika nafasi yoyote iwapo wanakidhi vigezo vyote, lakini inapotokea kwamba hakuna uwazi(transparency) ni dhahiri kwamba kunakuwa na upendeleo kama ilivyotokea.Hii inatokana na ukweli kuwa  idara hiyo haichukui watumishi kutoka Sekretarieti ya Ajira, kwa kuwa wanaohitajika ni askari. Lakini hii ni mojawapo ya ushahidi kuwa nafasi za kazi nchini zimeendelea kutolewa kwa upendeleo na wanaonufaika na nafasi hizo ni vigogo na ndugu zao au watu wenye mahusiano ya karibu na wenye mamlaka hayo.
Mheshimiwa Spika,
Kukosekana kwa takwimu sahihi na taarifa za nguvu kazi nchini kunaleta sintofahamu kubwa katika kutatua matatizo ya ajira nchini. Kukosekana huko kwa taarifa sahihi ndio kunakofanya CCM itake kuwaaminisha watanzania kuwa Mabilioni ya Rais Kikwete yameweza kutatua changamoto za ajira nchini.Tukiwa tunamaliza miaka 10 ya utawala usio wa kimkakati, vijana na nguvukazi ya Tanzania inawakumbuka watawala wa CCM kama wazee wa ahadi, ahadi zenye mashaka! Leo hii tuna Serikali inayokiri kutokua na takwimu za ajira nchini, ni vipi mikakati na sera hizi zitapimwa utekelezaji wake ikiwa takwimu sahihi zinakosekana?
Mheshimiwa Spika,
Mabilioni  ya Kikwete ni mojawapo ya mikakati iliyoshindwa kwa kuwa haikua na nia ya dhati ya kumfundisha mtanzania kuvua bali kuwapatia samaki wa siku moja na ililenga kuwadumaza watanzania kwa kuwaaminisha kuwa Rais Kikwete ana mahela ambayo yanaweza kutatua shida zao na si kuwainua kiuchumi. Kwa bahati mbaya sana Serikali za CCM za Awamu ya Pili, Tatu na hata hii ya Nne, zimekuwa siku zote zikisema zinafufua uchumi. Kila uongozi unaokuja hauishi kutamba kuwa unataka kufufua uchumi.Swali la kujiuliza ni kwamba, ni nani aliyeua uchumi na kuuzika? Na ni nani anayetaka kuufufua? Jibu la haraka ni serikali hiyo hiyo, tena ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) toka Baba wa Taifa akabidhi madaraka kwa marais waliomfuatia.
Mheshimiwa Spika,
Mkazo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na washirika wake (UKAWA) watakapopewa ridhaa ya kuongoza nchi hii Oktoba mwaka huu ni kwamba, pamoja na kiwango cha mchango wa pato letu kwenye kaya za jamii zetu kuwa ni kidogo, tunaweza kupunguza utegemezi na mgawanyo wa ovyo wa rasilimali na kupiga hatua katika utafiti na uendelezaji (Research and Development) na kuweka jitihada kubwa ili kuhakikisha kuwa rasilimali tulizonazo zinatumika kwa kiwango cha juu. Utawala wa UKAWA utajenga uwezo mkubwa wa viwanda vyake vya malighafi, vifaa vya uzalishaji(capital goods) na uzalishaji wa bidhaa za mlaji ili kutosheleza mahitaji ya walaji wa Tanzania na kutoa bidhaa na huduma bora katika soko la kimataifa. Kwa kufanya hivyo pia kutaongeza ajira kwa watanzania.
Mheshimiwa Spika,
Uchumi  wa taifa hili unaongozwa na CCM na CCM ndiyo yenye jukumu la kuua au kukuza uchumi. Serikali ya Awamu ya nne baada ya kuingia madarakani, ilikuja na mkakati mahususi wa kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania. Ili kuondoa umaskini, mbali ya kutoa ahadi ya ajira milioni moja kila mwaka kwa vijana, Rais Jakaya Kikwete pia alikuja na mpango wa kutoa mabilioni ya fedha kwa ajili ya kukopesha vikundi vya ujasiriamali. Fedha hizo zilisemekana kuwa zingetolewa kupitia benki, vyama vya akiba na mikopo (SACCOS) na taasisi nyingine za fedha zilizoruhusiwa na Serikali kupitishia mikopo hiyo.Chini ya mpango huo, kila mkoa uliahidiwa kumwagiwa sh bilioni moja.
Mheshimiwa Spika,
Hivi  karibuni wakati akijibu swali la msingi la  Mbunge wa Viti Maalumu, Faida Mohamed Bakari (CCM) ambaye alitaka kufahamu ni wafanyabiashara wangapi wenye ulemavu walipatiwa mikopo kupitia fedha hizo. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Uwekezaji na Uwezeshaji, Christopher Chiza alisema kuwa mpango huo ulikuwa na madhumuni ya kuwezesha wananchi kiuchumi na kuongeza ajira kwa wanawake na vijana vijijini na mijini kwa kuwapatia mikopo bila kujali maumbile yao. Alisema chini ya mpango huo, mikopo ilitolewa katika awamu mbili kupitia benki na asasi za kifedha, zilizoteuliwa na serikali baada ya kukidhi vigezo ambapo jumla ya Sh bilioni 43.69 zilitolewa na kunufaisha wajasiriamali 74,593. Vilevile, cha kusikitisha zaidi ni kuwa Waziri Chiza alieleza kuwa mikopo hiyo haikuwa na kipengele cha utambuzi cha watu wenye ulemavu. Hii inaonesha ni jinsi gani Serikali ya CCM imeshindwa kuwapa vipaumbele walemavu katika mikakati yake ya kuwawezesha kiuchumi na kukuza ajira. Ni hatari kuona kuwa, walemavu kwa muda wa miaka 10 ya utawala wa Kikwete hawajapewa kipaumbele cha kujiajiri wala kuajiriwa bali Serikali imekua ikiwakumbuka kipindi cha uchaguzi pekee. Ndio maana Serikali siku zote hutoa idadi ya walemavu walionufaika na nafasi za kiuongozi na kisiasa na wala si walionufaika na fursa za ajira nchini. Kambi rasmi ya Upinzani inaendelea kuwa mtetezi nambari moja wa haki za walemavu katika masuala ya ajira kwa kuwa watu wenye ulemavu ni sehemu ya jamii yetu na wana haki sawa na watu wote.
Mheshimiwa Spika,
Sasa inatosha! Kambi ya Upinzani Bungeni inapenda kuwaambia watanzania kuwa kwa muda wa miaka 10, matatizo yao yametumika kama mtaji wa Serikali ya CCM na hivyo utatuzi wa matatizo hayo ni sawa na ahadi hewa. Ikumbukwe kuwa Mheshimiwa Kikwete pia katika muendelezo wa ahadi zake zilezile, alitoa agizo mahsusi kwa Wizara hii Jumatano, Aprili 10, 2013 baada ya kuwa ameelezwa na kuonyeshwa video ya Mpango wa Kuwawezesha Wajasiriamali Vijana Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine cha Morogoro katika shughuli iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam. Mpango huo unaogharimiwa na Benki ya CRDB na kuendeshwa kwa pamoja kwa kushirikiana na SUA pamoja na Ushirika wa Wahitimu Wajasiriamali wa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUGECO).  
Mheshimiwa Spika,
Rais Kikwete aliitaka Wizara ya Kazi na Ajira kuwasilisha haraka iwezekanavyo kwenye Kikao cha Baraza la Mawaziri mapendekezo ya kuboresha na kupanua mpango mpya wa uwezeshaji na ajira kwa vijana wanaomaliza vyuo vikuu ambao unalenga kupanua fursa za ajira kwa kutoa mitaji kwa vijana ili waanzishe shughuli zao za uzalishaji. Hii ni kauli ya Kiongozi Mkuu wa Serikali kukubali kuwa mikakati yake dhidi ya tatizo la ajira imekosa vipaumbele vya muda mfupi na mrefu.
“Huu mpango nimeupenda sana. Huu ni bora zaidi kuliko hata ule mwingine wenye mafanikio wa Mabilioni ya Bwana Fulani kwa sababu huu unamwandaa vizuri mjasiriamali ili aweze kukopeshwa. Huu ndiyo aina ya mpango ambao nimekuwa nauzungumzia na kutaka uanzishwe ambako wasomi na wasio wasomo wanajiunda katika vikundi kulingana na ujuzi na elimu ili Serikali iweze kuwawezesha.”

Ikiwa imepita mwaka mmoja toka Rais atoe ahadi ya utekelezaji wa wazo hilo, wizara ina majibu gani?
Aidha, Rais Kikwete aliendelea kusema kuwa
“Serikali yangu iko tayari kuchangia kiasi cha sh. bilioni tano katika mfuko wa kuunga mkono mpango huu.Hii ni modeli nzuri ya kuwezesha vijana, kuzalisha ajira na kuboresha maisha ya watu. Tuendelee kuwezesha vijana katika sekta ya kilimo lakini sasa tuanze kufikiria namna ya kupanuka na kuingia katika maeneo mengine ili kusudi anayetaka kukopa kufanya biashara ya mitumba na ya teknolojia ya habari naye aweze kukopeshwa.’
Mheshimiwa Spika,
Ni jambo la kusikitisha kuona kuwa Rais anakubali kuwa modeli aliyooneshwa ni bora kuliko mabilioni yake ambayo anashindwa kutaja hata jina lake kwa kuwa, mpango wa Mabilioni ya Kikwete si tu umeshindwa kuwa na matokeo mazuri lakini pia umeshindwa kutatua tatizo la ajira nchini na kuwainua wananchi kiuchumi.
MISHAHARA YENYE STAHA KATIKA SEKTA MBALIMBALI NCHINI
Mheshimiwa Spika, kwa miaka yote mitano ya uhai wa Bunge hili Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikiwatetea watumishi wa umma katika nyanja mbalimbali lakini cha kusikitisha ni kwamba Serikali hii ya CCM inayojiita sikivu mara zote imekuwa ikipuuza na kubeza mapendekezo mazuri yanayotolewa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Mheshimiwa Spika,
Miongoni mwa masuala muhimu tuliyopendekeza na serikali kuyapuuza ni kama ifuatavyo:
1.Kima cha Chini cha Mshahara:
Mheshimiwa Spika,
 Kambi Rasmi ya Upinzani kwa muda mrefu imekua ikiishauri Serikali kupandisha kiima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kufikia shilingi 315, 000/= kwa mwezi lakini Serikali imeamua kuziba masikio na mpaka sasa haijatekeleza pendekezo hilo. Inashangaza sana kuona Serikali ikijigamba kuwa imepandisha kima cha chini cha mshahara kutoka shilingi 240,000/= hadi shilingi 265,000/= sawa na ongezeko la shilingi 25,000 tu.
Mheshimiwa Spika,
Pamoja  na matumaini ambayo Rais Kikwete aliwapa wafanyakazi mwaka 2005 na 2010, leo hii anapoondoka madarakani hata walimu ambao waliamini Rais kwa nafasi yake kama mkuu wa nchi atawapa alichowaahidi, leo wanambebea bango na kumuuliza kwa machungu ‘Shemeji unatuachaje’? hii inasikitisha sana .
Mheshimiwa Spika,
Leo hii Rais anaondoka madarakani watu wakiwa hawana shauku tena na Mei Mosi zaidi ya Taasisi za Serikali kwa kuwa maadhimisho haya hayana maana tena kwao. Maadhimisho haya kwa muda wa miaka 10 hayajakata kiu ama shauku ya mfanyakazi kupunguziwa kodi ya mapato wala kusikia ongezeko la mshahara wenye staha. Je ni nani kati yetu anayeweza kuishi kwa shilingi 265,000 kwa mwezi, akalipia kodi ya nyumba, ada ya watoto, huduma za umeme, maji na afya na kujikimu kwa chakula kwa kiasi hicho? Ipo hapi azma ya baba wa Taifa ya kujenga Taifa la wafanyakazi? CCM inaondoka madarakani ikiwa imeharibu misingi iliyojengwa na Mwalimu, ni nani wa kusimama na kujivunia hayo?
Pamoja na kuahidi kuwa Serikali itaongeza mshahara, Mhe. Raisi anashindwa kutamka hadharani iwapo ongezeko la mshahara litafikia 315000, na hata kama halitafikia bado anatoa matumaini kwa watanzania kuwa ataongeza. Hii ni mbinu ya kudaka kura za watanzania kwa mara nyengine.
KODI YA PATO LA MSHAHARA (PAYE)
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa utaratibu wa kodi ya mapato ya wafanyakazi ni kati ya asilimia 12 na 35 ya mshahara wa mfanyakazi. Kwa mujibu wa CAG katika mwaka 2013/2014 mamlaka ya kodi ta Tanzania ilikusanya jumla ya trilioni 15 kama kodi itokanayo na mapato (PAYE). Aidha, mdhibiti na mkaguzi mkuu wa serikali alionesha kwamba katika kipindi hicho, serikali ilitoa msamaha kwa walipa kodi wakubwa na makampuni ya nje liliyofikiwa kiasi cha shilingi trilioni 1.5 sawa na kodi iliyokusanywa na Serikali kutoka kwa wafanyakazi. Hii ina maana kwamba kama Serikali isingetoa misamaha hiyo ya kodi, mapato ya serikali kutoka kwa walipa kodi wakubwa nchini yangeongezeka maradufu na hivyo kumpunguzia mfanyakazi mzigo wa kodi.
Mheshimiwa spika,
Kutokana na ukuaji mbaya wa uchumi, mfumuko wa bei pamoja na kupanda kwa gharama za maisha, kodi itokanayo na mapato ya wafanyakazi imekuwa mzigo mkubwa na maumivu kwa wafanyakazi wa Tanzania waliopo katika ajira rasmi. Katika maoni yake ya mwaka toka kuanza kwa Bunge lako la 10, Kambi rasmi ya Upinzani, imekuwa ikipendekeza kwamba viwango vya kodi ya mapato ya wafanyakazi vipunguzwe kufikia asilimia 9 hadi 27 respectively. Pendekezo hili bado lina nguvu mpaka leo.  Leo Rais anaondoka madarakani akiacha kiwango cha asilimia 12 huku akiwa hana uhakika wa kutekeleza ahadi zake za kupunguza kodi kwa wafanyakazi. Akihutubia Maadhimisho ya Mei Mosi, Rais Kikwete alisema:
‘Na mwaka huu tutapunguza sijui tutafikia asilimia 9 kama mnavyotaka ila tutakapofikia si pabaya’
Haya ni maneno ya Rais ambayo si tu hayatoi mwelekeo bali hayajibu njaa ya miaka mingi ya punguzo la kodi ili Tanzania iwe sawa na nchi nyingine za Jumuia ya Afrika Mashariki. Ni ahadi yetu kwa wafanyakazi wote nchini ambao Mwalimu Nyerere aliwapigania kwa moyo wake wote bila kujali itikadi zao kuwa, UKAWA itayatekeleza haya kwa kuwa maoni ya CAG kwa mwaka 2013/2014 yalieleza dhahiri kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kupunguza misamaha ya kodi bila kuathiri mapato ya Serikali kwa namna yoyote ile.
WAKALA BINAFSI WA AJIRA NCHINI
Mheshimiwa Spika,
Kwa muda mrefu sasa Kambi ya upinzani imekua ikiwasilisha malalamiko ya watanzania ambao wamekua wakinyonywa nguvu zao na makampuni binafsi yenye kutoa huduma za wakala wa ajira huku wakala hawa binafsi wakinufaika. Katika hotuba yetu ya mwaka 2014/2015 tulielezea kuwa mawakala hawa binafsi wamekua wakitumia kampuni zao kuwaajiri watafuta kazi na si kuwaunganisha watafuta kazi na mwajiri.Hali hii imewakosesha wafanyakazi wanaounganishwa na wakala hawa haki zao za msingi ikiwemo likizo, huduma za matibabu, huduma za mifuko ya hifadhi za jamii na kuwanyima mishahara na posho zao pamoja na stahiki zao nyingine.
Mheshimiwa Spika,
Kwa muda mrefu tumeelezea ni jinsi gani wizara imezembea kuchukua hatua madhubuti za kiutawala ili kuhakikisha wakala hawa wa ajira wanafanya kazi kwa kuzingatia sheria na kanuni za nchi yetu ikiwemo Sheria ya Huduma za Ajira Na. 9 ya mwaka 1999. Aidha, wakala hawa binafsi wengi wameendelea kufanya kazi zao bila kulipa kodi na hivyo kulikosesha Taifa mapato. Mojawapo ya makampuni yaliyokuwa yakiendesha huduma za ajira ni pamoja na Erolink ambayo kwa mujibu wa Waziri wa Kazi na Ajira, Mhe. Gaudensia Kabaka alieleza kuwa iliikosesha Serikali mapato ya takribani Bilioni 3 kwa muda wa miaka mitatu.  Na katia kipindi hiki, makampuni takribani 56 ya wakala binafsi wa ajira yalituma barua za kuomba kibali mara baada ya Serikali kupiga marufuku makampuni ambayo hayana kibali kujihusisha na kazi za huduma za ajira. Ikiwa kampuni moja ya Huduma za ajira imeikosesha Serikali kiasi cha Shilingi za Kitanzania Bilioni 56 kwa miaka mitatu, je makampuni  56 ambayo yalituma maombi ya vibali yatakuwa yameikosesha Serikali kiasi gani cha mapato?
Mheshimiwa Spika,
Ikumbukwe  kuwa wakala binafsi wa ajira pamoja na kuendelea kufanya kazi bila kibali pia zimeendelea kuwanyima haki za msingi wafanyakazi wanaowamiliki kinyume na Sheria na utaratibu uliowekwa.
Mheshimiwa Spika,
Kampuni ya Uwakala wa Ajira inayojulikana kwa jina la ISON BPO (zamani SPANCO BPO) imelalamikiwa kwa muda mrefu kutotoa haki kwa wafanyakazi wapatao 500 wa kitengo cha huduma kwa wateja wa Airtel waliopo jengo la Quality Plaza na Makao Makuu ya Airtel, Morocco jijini Dar Es Salaam. Kampuni hii (ISON BPO), ni kampuni ya uwakala wa ajira inayotokea nchini India, na imepewa jukumu la kusimamia kitengo cha Huduma kwa Wateja na kampuni ya mawasiliano ya Airtel, tangu mwaka 2011 katika mambo yanayohusu voice (sauti), data (internet), na Airtel Money (huduma za kibenki kwa njia ya simu).
Mheshimiwa Spika,
Mnamo mwaka 2013, kupitia Wizara ya Kazi na Ajira, Serikali iliagiza na kutoa maelekezo kuwa wafanyakazi katika Sekta ya Mawasiliano wanatakiwa walipwe kiima cha chini cha Tshs. 400,000/- (laki nne) kama mshahara (basic salary). Lakini la ajabu, la kushangaza na la kusikitisha, ni kuwa kampuni hii ya kigeni imekuwa ikipuuzia maagizo na maelekezo hayo ya Serikali kwa kuendelea kuwalipa wafanyakazi wake mishahara kati ya 150,000/- na 270,000/- kinyume na agizo la Serikali. Aidha, ISON BPO, wamekuwa wakilipa kiwango hicho kwa madai kuwa wao (ISON BPO) hawaendeshi kampuni inayojihusisha na mambo ya mawasiliano, vilevile kwa dai lao lingine ni kuwa hawana hela za kuwalipa wafanyakazi kwa kiwango hicho cha 400,000/- (laki nne) kama ilivyoelekezwa na Serikali. Lakini wakati wakidai hayo kuwa hawana pesa ya kuwalipa wafanyakazi kwa kiwango hicho cha laki nne (400,000/-), wafanyakazi wenye asili ya India wamekuwa wakilipwa mishahara minono ya kati ya milioni tano na milioni kumi.
Mheshimiwa Spika,
Kutokana na mgomo wa wafanyakazi wa Airtel waliopo chini ya Kampuni ya ISON BPO uliotokea siku mbili kati ya tarehe 17 na 18, Aprili, 2015 ili kushinikiza wafanyakazi hao wa Airtel kulipwa malimbikizo yote na mshahara stahiki kama ilivyoagizwa na Serikali kupitia Wizara ya Kazi na Ajira; kwa kuamini watu wa Wizara ya Kazi na Ajira kuwa wangeweza kutatua mgogoro huo ambao umedumu kwa takribani miaka miwili sasa, wafanyakazi hao waliwasiliana na maafisa kazi (labour officers) ili kupata msaada. Maafisa hao wa Wizara ya Kazi walipofika, kwanza waliongea na wafanyakazi, na baadae waliongea na uongozi wa ISON BPO, baada ya mazungumzo ya pande mbili kufanyika katika nyakati tofauti, walikaa wote meza moja ya majadiliano na katika kuhitimisha, maafisa kazi walimpa ISON BPO (mwajiri) njia mbili;
1.    ISON BPO awalipe mshahara wa laki nne (400,000/-) na kama hawezi kulipa kiwango hicho cha fedha, basi ISON BPO wasitishe mkataba na Airtel ili idara au kitengo cha huduma kwa wateja kirudishwe Airtel.
au;
2.    ISON BPO kama mwajiri ajadiliane na wafanyakazi ili angalau awalipe laki tatu na nusu 350,000/-; na wakamalizia kwa kusema wao kama Wizara hawana mamlaka ya kumlazimisha ISON BPO alipe kiwango hicho cha mshahara, na huo ukawa mwisho wa kazi yao kama Wizara.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani tunataka kupata majibu ya  malalamiko ya wafanyakazi hao wapatao 500 kama ifuatavyo;
1. ISON BPO, ilisajiliwa kwa leseni na sheria ipi ya nchi? 2. ISON BPO, kwa nini wanaendelea kukaidi agizo la Serikali kwa kukataa kulipa mishahara stahiki na iliyopendekezwa na Serikali yaani 400,000/- TZs. na badala yake wanalipa mishahara kwa kiwango wanachojua na kutaka wenyewe? 3. Wizara ya Kazi na Ajira, kwa nini inakuwa na kigugumizi na kushindwa kuchukua hatua madhubuti dhidi ya ISON BPO katika mgogoro huu ilhali inajua kinachoendelea kufanywa na hawa ISON BPO ni ukiukwaji wa sheria za nchi na kuisababishia Serikali kupoteza pato la Taifa kupitia P.A.Y.E. ya wafanyakazi hawa?
USALAMA MAHALI PA KAZI (OSHA)
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu katika hotuba zetu tumekua tukionesha wasiwasi wetu juu ya masuala yanayohusu usalama na afya mahali pa Kazi. Ieleweke kuwa, kwa muda mrefu tumekua tukiwasilisha malalamiko mbalimbali yanayoletwa na wafanyakazi lakini Serikali imeendelea kuyapuuza.Maeneo mbalimbali ya kazi yamekua hayazingatii usalama na afya za wafanyakazi wake na hivyo kuhatarisha maisha yao. Leo hii kuna watanzania wengi waliopoteza maisha, watanzania waliopata ulemavu na matatizo makubwa ya kiafya kutokana na kukosa usalama makazini. Lakini watanzania hawa, hawajapewa fidia kutokana na madhara waliyopata na mbaya zaidi wengi wamekua wakiachishwa kazi hasa pale wanapokua wakidai haki zao dhidi ya waajiri.
Mheshimiwa Spika,
Sehemu za migodini, viwanda pamoja na sekta ya ujenzi ndio maeneo yanayoongoza kwa ajali mbaya na za kusikitisha zinazotokea mahala pa kazi. Ikumbukwe kuwa mpaka leo hii Serikali yako baada ya kupokea malalamiko ya wafanyakazi 79 walioachishwa kazi na kampuni ya uchimbaji iliyokuwa ikijulikana kama African Barrick Gold Mining, ni wafanyakazi 10 tu pekee ambao walipimwa afya na Wizara kupitia OSHA.Je, ni nini hatma ya wafanyakazi 69 ambao mpaka leo hawajapimwa? Ni nini hatma ya wafanyakazi wote 79 ambao wanaendelea kupata madhara pamoja na ahadi ya Serikali ya kuwapima wafanyaazi hao na kuhakikisha wanapata haki zao kwa mujibu wa Sheria?
Mheshimiwa Spika,
Wakati Serikali ikiwa busy kuandaa mikutano na semina kwa wenye viwanda mbalimbali nchini, inasahau kuwa baadhi ya viwanda na mahali pa kazi hawatekelezi Sheria kwa kiwango kinachotakiwa. Leo hii Serikali inaeleza kuwa imefanikiwa kufanya kaguzi za kushtukiza sehemu za kazi huku ni ukweli usiopingikiza kuwa baadhi za makampuni na viwanda yana ulinzi mkali na iwapo maofisa wa OSHA watafanya ukaguzi, vikwazo vya ulinzi pekee vinatosha kumuandaa muajiri kukwepa wajibu wake na kujiandaa na ukaguzi kwa kuficha mapungufu yaliyopo mahali pa kazi.

MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika kipindi chote cha miaka mitano tumeshauri mambo yafuatayo kuhusiana na mifuko ya hifadhi ya jamii hapa nchini;
1.Kuunganisha mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii  na kubaki chini ya usimamizi wa Wizara ya Kazi na Ajira lengo  likiwa ni kuirahisishia Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi za Jamii  katika kutekeleza Sheria moja nakuunda vifungu sawa vya kisheria vitakavyosimamia utekelezaji na uendeshaji wa mifuko hii. Tulipendekeza PPF na NSSF iunganishwe na kuwa mfuko mmoja kwa ajili ya Sekta Binafsi vilevile LAPF, PSPF na GEPF iunganishwe na kuwa mfuko mmoja kwa ajili ya Sekta ya Umma.
2. Tumeitaka serikali kuwa na jitihada za haraka kunusuru uhai wa Mifuko ya Hifadhi ya jamii kwa kulipa fedha walizochota kwa ajili ya uwekezaji katika miradi mikubwa kama ambavyo imeonyeshwa katika Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2012/2013, 2013/2014 lakini ripoti ya CAG ambayo imetolewa hivi karibuni ya 2014/2015.
Mheshimiwa Spika,
Ni kweli kuwa sikio la kufa halisikii dawa. Madeni sugu ya serikali yanatishia uhai wa mifuko ya hifadhi ya jamii nchini huku Mamlaka ya Usimamizi ya Mifuko hiyo (SSRA) ikitoa angalizo kwa serikali kuhusiana na hali hiyo kufuatia kuidai Sh. trilioni 8.43 kuwa hali hiyo inaweza kukwamisha mifuko hiyo kuwalipa mafao wanachama wake, kujiendesha yenyewe na kuwekeza katika miradi mbali mbali. Mkurugenzi wa SSRA, Irene Isaka alitoa tahadhari hiyo Oktoba mwaka jana mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kwa kuwakutanisha wakurugenzi wa mifuko ya hifadhi ya jamii, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Mkuu wa Hesabu za Serikali, SSRA na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambapo alieleza kuwa iwapo serikali itaendelea kukopa na kutopeleka michango ya wanachama wake, mifuko hiyo itaathirika kiasi cha kushindwa kulipa mafao kwa wanachama wake.
‘’ tuliyonayo, mifuko yetu ni ya pensheni, hasara ni ya mifuko. Mwanachama hatamsamehe mwenye mfuko kwa kushindwa kumlipia, kadri deni linavyoongezeka ndivyo Mfuko unaumia na baadaye kushindwa kulipa mafao yanayotakiwa,”
Mheshimiwa Spika,
Kauli hii ni ya msimamizi mkuu wa mifuko ya hifadhi ya jamii ambaye ndiye mwenye dhamana ya uhai wa mifuko hii. Mara kadhaa Kambi ya upinzani imeelezea na kuonya jinsi ambavyo madeni haya ambayo ni pamoja na PPF (bilioni 192), NHIF ( bilioni 107), NSSF ( bilioni 467), PSPF ( bilioni 4.29), LAPF ( bilioni 170) na GEPF (bilioni 6.86) yanavyohatarisha uhai wa mifuko hii. Si Raisi Kikwete wala viongozi waandamizi wa CCM wenye kuelewa kuwa, hili ni bomu litakapolipuka muda wowote. Ieleweke kuwa hakuna mpinzani yeyote anayepinga miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa chuo kikuu cha Dodoma (UDOM). Tunachokipinga ni kitendo cha Serikali kutumia fedha za wachangiaji wa mifuko kwa miradi yake ambayo ingeweza kutekeleza ipasavyo kwa kutumia fedha nyingine na  kama ingefuta misamaha ya kodi, ingepigana ipasavyo kuzuia ufisadi na ubadhirifu kama wa ESCROW, EPA, RICHMOND- DOWANS na/ au kama ingeweza kupunguza matumizi makubwa ya serikali.  
Mheshimiwa Spika,
Huwezi kuukataa ukweli kuwa utawala wa awamu ya nne umeshindwa kuipa wizara ya fedha uwezo wa kitaasisi wa kukusanya kodi matokeo yake, serikali inakuwa inakodolea macho fedha za mifuko ya hifadhi ya jamii na hii ni dhambi ambayo haitafutika machoni pa watanzania. Na sasa tunaelewa ni kwa nini serikali ilikuwa inaishinikiza wachangiaji wa mifuko wasichukue pensheni zao mpaka wafikishe umri wa kustaafu ambao ni miaka 60, kwa kuwa wanajua umri wa maisha ya wa watanzania ni miaka 52. Hatuwezi kuwa na serikali ambayo ina trade-off na ustawi wa maisha ya watu wake, hii ni aibu kubwa!
MFUKO WA TAIFA WA HIFADHI YA JAMII (NSSF)
Mheshimiwa Spika, mfuko wa hifadhi ya jamii, NSSF, ni mojawapo ya mifuko ambayo mbali ya kutoa mafao ya kustaafu na huduma zingine kwa kadri dira na dhima yake  lakini bado inajishughulisha katika uwekezaji kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa takwimu zilizopo ni kwamba mbali ya kuwekeza kwenye ujenzi wa majengo ya Chuo Kikuu cha Dodoma na Daraja la Kigamboni, pia NSSF ina miradi ifuatayo ya ujenzi wa nyumba;
     i.        Nyumba  300 za Mtoni Kijichi  (PHASE I &II) –Nyumba hizo zilikwisha uzwa tayari
   ii.        Nyumba 800-Flats 500 na Villas 300 (PHASE III) ambao umegharimu shilingi bilioni 137.
  iii.        Mradi wa AZIMIO SATELITE  -Kigamboni wenye Nyumba 7160 (Flats &Villas) –Utagharimu shilingi bilioni 871
  iv.        Mradi wa Dungu Farm-Kigamboni (Flats 568) Utagharimu  shilingi bilioni 140
    v.        Mradi wa MZIZIMA TOWER nyumba ya Ghorofa 32 unaotarajiwa kumalizika Juni 2017, ambao utagharimu shilingi bilioni 233. Lakini hadi sasa bado mradi haujaanza.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi sio kama inapinga uwekezaji unaofanywa na NSSF, je uwekezaji huo unafanywa kwa kuangalia kipindi ambacho miradi hiyo itarejesha faida za uwekezaji (return on investment)?
Aidha, kwa mujibu wa kifungu cha 3.12 cha mwongozo wa  Msimamizi wa Mifuko ya Hifadhi(SSRA) wa mwaka 2003, pamoja na kanuni zake  kuhusu uwekezaji salama wa mifuko na marejeo yake ya mwaka 2012 ni kwamba, mifuko inatakiwa kuwekeza asilimiai 70 ya mali  zake kwenye dhamana (T-Bills) na hati fungani ( T-Bonds), asilimia 25 ya mali zake kwenye Miundombinu, asilimia 30 ya mali zake kwenye mali isiyohamishika (Real Estates). Je, ni kwa kiasi gani NSSF imefuata Sheria na kanuni kuhusu uwekezaji wake mpaka sasa kwa kufuatia mgawanyo uliotajwa?
Mheshimiwa Spika, NSSF walinunua majengo ya Manji (EPZ-Project) kwa jumla ya shilingi bilioni 47.5 mwaka 2006, kwa mujibu wa taarifa mbalimbali , ni kuwa majengo hayo hayakuwa na thamani hiyo wakati NSSF inayanunua. Pamoja na hayo, mradi huu unasemekana mpaka sasa kutorudisha thamani ya uwekezaji kwa muda. Kambi ya Upinzani Bungeni inahusisha upandishaji huo wa thamani isiyo halisi kuwa ni mojawapo ya mianya ya watendaji wa NSSF kujipatia 10% kwa miradi isiyo na tija. Aidha, kodi ya mwaka ya Jengo hilo inayotokana na upangaji, haijaweza kuakisi marejesho ya faida ya uwekezaji huo kwa kuwa mradi huo mpaka sasa umeshindwa kurudisha hata nusu ya fedha zilizowekezwa na hivyo kuhatarisha uwezo wa mfuko kutoa marejesho kwa wanachama wake.
Kwa mujibu wa sheria ya SSRA, Benki Kuu ndio mamlaka ya kuhakikisha mifuko inafanya uwekezaji makini, je kwa uwekezaji huu ambao taarifa ya CAG ilisema kuwa unauweka mfuko katika hali ya kuweza kufilisika na hivyo wanachama kukosa mafao, Wizara ya Fedha inatoa majibu gani?
Mheshimiwa Spika, kuonesha kuwa uwekezaji wa NSSF umekuwa ukiongozwa na matakwa ya watu binafsi, kuna jengo la ghorofa 4 lililojengwa Kigoma kwa gharama ya shilingi Bilioni 7 na limekamilika sasa ni miaka 2, lakini hadi muda huu halijapata mpangaji. Kambi ya Upinzani inahitaji kupata majibu ya uhakika kuhusu uwekezaji huu usio na tija ni nini hatma ikiwemo uwajibikaji wa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi kwa kushindwa kuusimamia mfuko ipasavyo?
Mheshimiwa Spika, NSSF imenunua ardhi mikoa kadhaa kwa bei ambayo ni zaidi ya ile ya soko (Inflated price) na mwishowe viwanja hivyo vinakosa wanunuzi. Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa NSSF kukataa kuwekeza kwenye dhamana za Serikali na kuwekeza kwenye majengo ni wa kutia shaka na ni mwanya wa watendaji wake kupokea rushwa au makampuni yanayopewa kandarasi za ujenzi ni makampuni yao na hivyo uwekezaji huo kuwanufaisha wao binafsi na si wanachama wa mfuko.
Kambi ya Upinzani Bungeni, inataka majibu ya kina kutoka kwa Wizara juu ya uwekezaji mzima unaofanywa na NSSF bila kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo kwa kuwa ni dhahiri kuwa uwekezaji mkubwa usio na tija unaofanywa na NSSF  unahatarisha kwa kiwango kikubwa uhai wa mfuko huu.
PENSHENI KWA WAZEE.
Mheshimiwa Spika, Wazee nchini wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutokupata matibabu bure,kupoteza mali zao na haki ya kurithi,kuuwawa kwa imani za kishirikina  ikiwemo wazee 2,866 waliouwawa katika mikoa 10 kwa kipindi cha miaka 5 iliyopita sawa na wastani wa wazee 573 kila mwaka au takribani mzee mmoja anauwawa kila siku. Tumeendelea kushuhudia wazee katika nchi hii kupuuzwa, kunyanyasika na kudharauliwa huku wakijisahau kuwa na wao pia ni wazee watarajiwa. Ikumbukwe kuwa ilikua ni ahadi ya uchaguzi ya Rais Kikwete kuwa wazee watalipwa pensheni.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa sensa ya Watu na Makazi, 2012 wazee nchini ni milioni 2,507,568 sawa na asilimia 5.6 ya idadi yote ya watanzania. Ongezeko la wazee nchini na duniani ni jambo lisilowezwa kupuuzwa tena kwani mtu mmoja katika watu tisa ni mzee, hata hivyo idadi hii inategemewa kuongezeka hadi kufikia mzee mmoja katika watu watano ifikapo 2050.
Katika hotuba zetu za miaka mitano mfululizo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tumeendelea kusisitiza umuhimu wa wazee kupewa pensheni, na Serikali imekua ikitoa kauli kuwa utoaji wa pensheni kwa wazee unafanyiwa utafiti ama uko katika hatua za mwisho. Aidha, kauli za Serikali kuwa wazee wapatiwe matibabu bure imekua ni changa la macho kwa kuwa wazee wengi wamepata usumbufu katika kupata huduma za afya na wengine wameshindwa kabisa kupata huduma hizo. Kwa kuwa kauli ya kuwapa wazee pensheni ilitumiwa na CCM katika uchaguzi, tunawataka wazee kuwa makini kwa kuwa CCM hawa hawa, watarudi tena na kauli ya kuwalipa pensheni kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu kwa nia ya kuwaomba kura.Tunapenda kuwakumbusha wazee wetu kuwa ‘zimwi likujualo halikuli likakishwa’. Na iwapo itatokea CCM kuwafata kuomba kura wasisahau kuwakumbusha CCM kuwa ‘baniani mbaya kiatu chake dawa’.
Mheshimiwa Spika,
Baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni naomba kuwasilisha.
  

……………………………..
                          CECILIA DANIEL PARESSO (MB)
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
WIZARA YA KAZI NA AJIRA
25.05.2015

No comments: