(Inatolewa
kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge kanuni ya 99(9) toleo la mwaka 2013).
UTANGULIZI
Mheshimiwa
Spika, Kwa
mujibu wa kanuni za kudumu za Bunge, Kanuni ya 99 (9) naomba kuwasilisha maoni
ya Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni ya makadirio ya mapato na matumizi kwa Mwaka
wa Fedha wa 2015/2016 ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.
Mheshimiwa
Spika, kabla ya
kuwasilisha hotuba hii, napenda kuchukua nafasi hii kwa niaba ya Kambi ya
Upinzani Bungeni kuungana na wananchi wa Burundi na wapenda amani duniani kote
kulaani mauaji ya Kiongozi wa Upinzani huko Burundi Zedi Feruzi, mkuu wa Chama
cha Umoja wa Amani na Demokrasia UPD-Zigamibanga aliyeuawa kwa kupigwa risasi
na watu wasiojulikana mjini Bujumbura huku machafuko yakiendelea nchini humo.
Kiongozi huyo aliuawa Jumamosi usiku alipokuwa akiingia nyumbani kwake katika
eneo la Ngagara. Mlinzi wake pia ameuawa katika tukio hilo. Kambi ya Upinzani
Bungeni inalaani mauaji haya kwa kuwa ni mwendelezo wa vyama tawala kudhuru na
hata kutoa uhai wa wapinzani wao pale wanapoona wameshindwa ama hawakubaliki
tena kwa wananchi. Ni wajibu wetu wapinzani kusemea haya kwa kuwa hata nchini
kwetu Tanzania, hatupo salama na tunaamini kuwa Mungu atatusimamia. Na ikiwa
damu yetu itamwagika katika dhuluma na haki, vizazi vyetu vitasimama na kupaza
sauti zao dhidi ya tawala dhalimu. Mwenyezi Mungu azilaze roho za wahanga wote
wa dhuluma za kisiasa mahali pema peponi.
Mheshimiwa Spika, kwa
niaba ya Waziri Kivuli wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Mhe.
Salum Barwany, napenda kumshukuru
Mwenyezi Mungu kwa kunipa uzima na kuendelea kunisimamia katika maisha yangu.
Napenda kuchukua fursa hii pia kuwashukuru, ndugu, jamaa, marafiki na familia
ya Mheshimiwa Barwany kwa kuendelea kuwa pamoja naye kwa hali na mali.
Niwashukuru vilevile wananchi wa Lindi mjini kwa kumpa ushirikiano mkubwa
mbunge wao na napenda kuwahakikishia kwa niaba yake kuwa Oktoba 2015, ataendelea
kuwatumikia kama mwakilishi wao kwa ushindi wa kishindo.
Aidha,
napenda kuchukua fursa kuwashukuru wabunge wote wa Kambi ya Upinzani na
watendaji wake kwa ushirikiano mkubwa, viongozi na wanachama wa vyama vinavyounda
UKAWA kwa nia yao ya dhati ya kuwakomboa watanzania hasa kuelekea uchaguzi Mkuu
wa Oktoba 2015.
Mheshimiwa Spika,
Mwanaharakati wa Haki za Kiraia na Mkulima maarufu wa Marekani Cesar Chavez
aliwahi kusema ;
“ Hatuwezi kutaka
mafanikio kwa ajili yetu tu na kusahau maendeleo na ustawi wa jamii yetu...
Malengo yetu ni lazima yawe makubwa kiasi ili kujumuisha matarijio na mahitaji
ya wengine kwa ajili yao na kwa ajili yetu pia”.
Hii
ni tafsiri ya maneno ya Cesar Chavez kwa nukuu ya lugha ya kiingereza ni kama
ifuatavyo;
“We cannot seek
achievement for ourselves and forget about progress and prosperity for our
community... Our ambitions must be broad enough to include the aspirations and
needs of others, for their sakes and for our own”
Mheshimiwa Spika,
ikiwa tumebakiza miezi michache takribani miezi minne mpaka ufanyike uchaguzi
mkuu ni dhahiri kuwa tutasikia kauli nyingi zenye kulenga kuwaaminisha
watanzania kuwa Serikali ya CCM itaenda kutekeleza matarajio ya watanzania
waliyokuwa nayo chini ya utawala wa Raisi Jakaya Mrisho Kikwete yalitolewa
wakati wa Uchaguzi wa mwaka 2005 na pia uchaguzi Mkuu wa 2010.
Mheshimiwa Spika,
labda tuikumbushe Serikali ya CCM usemi kuwa ‘Mla ndizi husahau ila si mtupa
maganda’. Pamoja na kuwa Serikali ya CCM ilitoa ahadi kemkem zikiwemo za kuinua
maisha ya watanzania kwa kauli ya maisha bora kwa kila mtanzania, mpaka kufikia
leo mwaka 2015, hali za watanzania zimeendelea kuwa duni tangu kuanza kwa
utawala wa awamu ya nne hasa wenye sekta ya maendeleo ya jamii , jinsia na
watoto.
Mheshimiwa
Spika,ni wajibu wetu kuwakumbusha wanaoachia madaraka kuwa watanzania ambao
kwao ni watupa maganda, hawajasahau ulaghai na ahadi zilizotolewa kwao mwaka
2005 na 2010 kwa kuzingatia yafuatayo;
MAENDELEO YA JAMII
Mheshimiwa Spika, ni
dhahiri kuwa kwa hali iliyopo sasa, Taifa letu limekumbwa na mporomoko mkubwa
wa maadili unaoochangiwa na kasi kubwa ya utandawazi.
Mheshimiwa Spika,
Tanzania ni moja kati ya mataifa ya Afrika yenye uwezo wa kutumia historia na
utamaduni wake katika kukuza maadili na jamii yenye staha. Lakini katika miaka
ya karibuni, taifa letu limeshuhudia vitendo vya kuporomoka kwa maadili ambavyo
vimechangia kukithiri kwa vitendo vya ubakaji na ulawiti, wizi na ujambazi,
mauaji, biashara ya ngono, ulevi, ngoma na sherehe zisizo na staha, waathirika wa madawa ya kulevya na
ongezeko kubwa la maambukizi ya UKIMWI na magonjwa mengine ya zinaa.
Vyuo vya Maendeleo
ya Jamii na Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii.
Mheshimiwa Spika,
kwa muda mrefu sasa Kambi ya Upinzani Bungeni imekua ikiitaka Serikali
kuhakikisha kuwa masuala ya kimkakati ya kuzuia ama kupunguza mmomonyoko wa
maadili kwa kuvipa uwezo vyuo vya maendeleo ya jamii pamoja na vya maendeleo ya
wananchi ili kuongeza idadi ya wataalamu na kuwatumia wataalamu hao kwa
maendeleo ya jamii nchini. Ni dhahiri kuwa vyuo vilivyopo vya maendeleo ya na
vyuo vya wananchi havikidhi ongezeko la watu nchini na pia havipewi kipaumbele
katika kuviwezesha kutoa elimu na ujuzi unaofaa kwa wataalamu wa maendeleo ya
jamii nchini kwa kuwa Serikali imeendelea kutenga bajeti finyu. Vyuo vingi
vimeendelea kuwepo katika majengo ambayo ni chakavu, yenye ukosefu wa
miundombinu bora na ambavyo haviwezi kuendelea kutokana na gharama kubwa za uendeshaji.
Upungufu wa Maafisa
Maendeleo ya Jamii Nchini
Mheshimiwa Spika,
tukiwa tunajadili bajeti ya mwaka ujao wa 2015/2016 huku randama ya Wizara hii
ikionesha kuwa maafisa wa maendeleo ya jamii nchini wanakadiriwa kufikia
asilimia 29 tu, huku Sera ya Maendeleo ya Jamii ikitaka kuwepo kwa mtaalamu ama
afisa maendeleo ya jamii kwa kila kata nchini. Hii ni mojawapo ya sababu
inazofanya jamii ya Kitanzania kukumbana na changamoto kama nilivyoorodhesha
awali. Ni jambo la kushangaza kuwa pamoja na kuwa na vyuo vya maendeleo ya
jamii ambavyo kwa mwaka 2014/2015 pekee vilikadiriwa kudaili jumla ya wanafunzi
3594 lakini bado kuna upungufu wa maafisa maendeleo ya jamii nchini. Ikiwa
Serikali inajivunia ongezeko la wanafunzi katika vituo hivi, je ni nini
kinachowashinda Serikali kuajiri wahitimu wa vyuo hivi ili kukabiliana na
upungufu wa maafisa wa maendeleo ya jamii nchini?
Mheshimiwa Spika, maslahi
duni katika fani za maendeleo ya jamii na wananchi ni mojawapo ya sababu
zinazosababisha kuwe na uhaba wa wataalamu hao hasa katika ngazi za kata.
Baadhi ya wahitimu wameshindwa kujiunga na kazi zinazohusiana na fani hii na
kukimbilia katika kada nyengine ili waweze kujikwamua kiuchumi. Hii ni mojawapo
ya sababu zinazofanya Serikali ya CCM isiwe na tija kwa muda wa miaka 10 ya
kipindi cha awamu ya nne.
Mheshimiwa Spika,
kumbukumbu rasmi za Bunge lako zinaonesha kuwa kwa kipindi cha miaka mitano
toka kuanza kwa Mkutano Wa Kumi (10), Kambi ya Upinzani katika kila mjadala wa
bajeti imekua ikiishauri Serikali kuajiri wahitimu wa vyuo vya maendeleo ya
jamii mojakwamoja na kuwapangia vituo katika kata mbalimbali nchini. Lakini kwa
kuwa Serikali imeendelea kupuuza maoni yetu ya Kambi ya Upinzani Bungeni, ni
dhahiri kuwa Serikali imeshindwa kutekeleza jukumu lake la kuwa mlezi wa jamii
zetu nchini.
Mheshimiwa Spika,
ni jambo la aibu kubwa kwa Serikali ya CCM ambayo toka utawala wa Baba wa Taifa,
Hayati Mwalimu Nyerere, haijaviendeleza hata vyuo vilivyoanzishwa na kujengwa
kati ya miaka 1950 na 1963. Ni aibu kwa Serikali inayojivunia mafanikio,
kujivunia kuchakaza majengo ya vyuo vilivyoanzishwa kwa nguvu za Baba wa Taifa
na kusababisha uchakavu mkubwa. Leo CCM inaposema inamuenzi Mwalimu Nyerere, je
inamuenzi kwa kuchakaza juhudi zake na kugeuza vyuo hivyo magofu? Ikiwa
Serikali ya CCM imeweza kuacha kutumia magari ya zamani chakavu na kununua
mashangingi kwa ajili ya viongozi wa Serikali, inashindwaje kuvipa hadhi vyuo
vilivyojengwa toka enzi za Mwalimu? Hii ni aibu kubwa.
Mheshimiwa Spika,
ni dhahiri kuwa kukithiri kwa vitendo kama kangamoko, vigodoro, singo n.k
(ambavyo pamoja na Kambi ya Upinzani kushauri kuvipiga marufuku na kuwatia
hatiani wahusika), vitendo hivi vinaelekea kuota mizizi na kusababisha
mmomonyoko wa maadili kutokana na Serikali kushindwa kutatua changamoto za maendeleo
ya jamii nchini! Ni imani yetu kuwa wananchi wamekua mashahidi wa jinsi
tulivyojitahidi kusimamia bajeti za Serikali ikiwemo mapendekezo ya kuinua na
kuipa hadhi sekta ya maendeleo ya jamii kwa muda mrefu lakini tumepuuzwa. Ni
kwa imani hiyo ambayo watanzania wanayo kwetu UKAWA, tunaamini kuwa mwaka 2016/2017 tutatoa vipaumbele wa kutatua
changamoto za maendeleo ya jamii ikiwemo ufinyu wa bajeti, uhaba wa waalimu na
wataalamu wa vyuo vya maendeleo ya jamii na vyuo vya maendeleo ya wananchi vyenye
kuleta mabadiliko chanya kwa watanzania wote.
Mheshimiwa Spika, Kambi
ya Upinzani inaamini kuwa matumizi makubwa ya Serikali na misamaha ya kodi
isiyo na tija kwa taifa, imekua chanzo kikubwa cha kudumaza Taifa. UKAWA
inajipanga kukabiliana na matumizi makubwa ya Serikali pamoja na kupunguza
misamaha ya kodi ili kujenga vyuo vya maendeleo pamoja na kuvikarabati vyuo
chakavu kwa mustakabali wa Taifa letu na vizazi vyetu.
Maendeleo ya Jinsia
Nchini
Mheshimiwa Spika, ni
ukweli usiopingika kuwa ili kuendeleza jamii yoyote kuwa jamii bora na yenye
maendeleo basi kipaumbele kikubwa kiwe kuhusisha masuala ya wanawake katika
mikakati ya kisera na ujumuishaji wake katika shughuli mbalimbali za
maendeleo. Pamoja na kuwa na ongezeko la
wanawake katika ngazi mbalimbali za maamuzi ikiwemo ongezeko la majaji, mawaziri
na wakuu wa wilaya pamoja na wabunge ni dhahiri kuna changamoto kubwa katika
kuhakikisha wanawake wanapewa nafasi hizo kutokana na sifa. Aidha, changamoto
kubwa pia ipo katika ngazi muhimu hasa katika ngazi za chini ambazo
zinamuathiri mwanamke moja kwa moja. Ngazi hizi za maamuzi ni pamoja na ngazi
za familia na vijijini ambapo mwanamke anaonekana kama mzigo ama chombo kisicho
na umuhimu katika maamuzi.
Mheshimiwa Spika,
ongezeko la ukatili dhidi ya wanawake nchini ni mojawapo wa viashiria kuwa,
ongezeko la viongozi wanawake katika ngazi za juu hakujamkomboa mwanamke hasa
wanaotoka katika mazingira duni kwa namna yoyote ile.
Uwezeshaji wa
Kiuchumi
Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa Sensa iliyofanyika mwaka 2012 inaonesha kuwa kati ya watanzania
milioni 45, wanawake ni milioni 23. Pamoja na kuwa kundi hili la wanawake
limechanganywa na watu walio chini ya miaka 18, inaleta taswira kuwa idadi ya
wanawake nchini ni kubwa na hivyo takwimu za uwezeshaji kwa kundi la wanawake
zinazotolewa na Serikali , zinaacha kundi kubwa la wanawake likiwa halijafikiwa
na mafunzo na mikopo ya uwezeshaji.
Kwa
mfano , kwa mujibu wa takwimu za Wizara hii zinaoesha kuwa ni wanawake 11350 tu
walioweza kufikiwa na Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) ambao kwa mujibu wa
taarifa hii ni sawa na asilimia 87% na
wanaume 1642 sawa na asilimia 13 kati ya mwaka 2009 na 2014. Hiki ni kiini
macho cha mchana kweupe kwa kuwa ikiwa kwa mujibu wa Sensa; wanawake na wanaume wenye umri juu ya miaka
15 ni takribani 25,200,000, basi kwa muda wa miaka 5, Benki hii imeweza kunufaisha asilimia 0.49%
ya wanawake na wanaume wa Tanzania nzima kwa miaka 5.
Ukatikili wa
Kijinsia
Mheshimiwa
Spika, Kama ilivyoandikwa katika Mwongozo wa Sera ya Ukatili wa Kijinsia (MOHSW
2011), ukatili wa kijinsia (GBV) ni tatizo kubwa ambalo linawanyima uhuru
wanaume, wanawake na watoto kufurahia haki za msingi za binadamu na kufanya
wapendavyo. Licha ya tatizo hilo kuwepo katika nchi nyingi duniani lakini
halipewi kipaumbele wala halishughulikiwi ipasavyo. Ukatili wa kijinsia
unatokana na tofauti za kijinsia na baadhi ya mila na desturi potofu ambazo
mara nyingi zinasababisha kuwepo kwa tofauti za kijinsia katika ngazi
mbalimbali za jamii. Wanawake kutothaminiwa katika familia, hali duni ya uchumi
na kutofahamu sheria kunawafanya washindwe kupata msaada pindi kunapotokea
ukatili wa kijinsia.
Mheshimiwa Spika,
takwimu zinaonesha kuwa asilimia 45 ya wanawake wametendewa ukatili wa
kijinsia. Pia, kwamba wasichana watatu kati ya 10 wametendewa angalau tendo
moja la ukatili wa kijinsia kabla ya kufikia umri wa miaka 18. Vilevile, zaidi
ya asilimia 13 ya watoto wa kiume wenye umri ule ule wamefanyiwa matendo ya
ukatili kabla ya kufikisha umri wa miaka 18. Leo Serikali inapoongelea kuhusu
kufanikiwa kudhibiti ukatili wa kijinsia, unazungumzia kufanikiwa katika
kuyalinda makundi haya ama katika kuandaa semina na warsha zinazowanufaisha
watu wachache?
Mheshimiwa Spika,
ni jambo la kusikitisha hata kuona na kusikia Waziri mwenye dhamana akifurahia
kujengea kamati ya Kitaifa uwezo wa kukabiliana na ukatili wakati huu ambao
ukatili na unyanyasaji dhidi ya wanawake majumbani na sehemu za kazi umeendelea
kuongezeka, kati ya wanawake watatu, wawili wanatendewa ukatili wa kijinsia na
wanaume.
Mheshimiwa Spika,
ni aibu kuona Serikali ya CCM inajivunia kuwa mtetezi wa wanawake na watoto
wakati kama nchi, bado tuna changamoto kwenye sheria za urithi na ndoa ambazo
zinarudisha nyuma juhudi za kupigania usawa wa kijinsia.
Mimba za Utotoni
Mheshimiwa Spika,
Kutokana na taarifa ya umaskini na maendeleo ya watu ya 2011, mimba za utotoni
zilifikia 1,056 kwa mwaka mmoja tu. Wasichana wote hawa waliacha shule. Leo hii
tukimaliza miaka kumi ya utawala wa Rais Kikwete, tunamaliza na maumivu ya
kauli yake aliyoitoa mwaka 2010 akiwa katika ziara mkoani Mwanza akisema kuwa
matukio ya mimba kwa wanafunzi wa kike nchini yanasababishwa na viherehere vya
wanafunzi wenyewe.
Mheshimiwa Spika,
kwa Rais kutoa kauli inayowatupia lawama wanafunzi wa kike bila uchambuzi,
kunaenda kinyume na azma ya Serikali
kuwajibika kwa wananchi kuhusu kufanyia kazi matatizo ya msingi yanayosababisha
wanafunzi wa shule za msingi na sekondari za Serikali kupata ujauzito.
Ikumbukwe kuwa kwa mujibu wa Wizara ya Elimu, mpango wa Serikali kuhusu shule za
sekondari za kata ulilenga shule hizo zijengwe karibu na makazi ya wananchi ili
watoto waweze kutoka nyumbani na kwenda shuleni na kurudi nyumbani kwa urahisi
kwa lengo la kuhakikisha kuwa watoto wengi wanapata elimu nzuri na bora zaidi. Lakini
kwa asilimia kubwa utekelezaji wa mpango huo haujafanyika kama ilivyokusudiwa
kwa sababu kuna maeneo mengi nchini ambapo wanafunzi wengi tena wenye umri
mdogo chini ya miaka 17, bado wanalazimika kutembea zaidi ya kilomita kumi kila
siku kwenda shuleni huku wakipita katikati ya mapori, mabonde na milima yenye
hatari mbalimbali kwa maisha yao ukiwemo ubakaji.
Mheshimiwa Spika,
ni wanafunzi hawa wanaopata mimba za utotoni ambao wanakaa katika maeneo ambayo
yanashida za maji na hivyo kulazimika kutembea umbali mrefu baada ya masomo ili
kupata maji kwa matumizi ya majumbani mwao. Kushindwa kwa sera za Serikali ya
CCM ndio kumepelekea watoto wa kike kukumbwa na mimba za utotoni. Kushindwa kwa
Serikali kusimamia utekelezaji wa ahadi zake za kipindi cha uchaguzi ndizo zinazosababisha
ongezeko la mimba za utotoni, hivyo kauli ya Raisi Kikwete si iliwaumiza
waathirika wa mimba za utotoni bali pia iliwadhalilisha wazazi masikini wa
kitanzania.
Kambi
ya Upinzani Bungeni, inaelewa kuwa kuna baadhi ya mimba za utotoni zinazosababishwa
na kuporomoka kwa maadili kwa baadhi ya watoto wa kike lakini asilimia kubwa ya
wasichana waliopata mimba za utotoni, wanahitaji nafasi kwa ajili ya
kurekebisha makosa. Mtoto akinyea mkono, ‘hauukati’ ni kauli ambayo sisi wazazi
tunatumia katika kurekebisha watoto wetu, hivyo kulitenga kundi hili na
kutolipa kipaumbele ni kuongeza mzigo katika taifa hasa watoto wa mitaani. Ni
rai yetu kwa watoto wote wa kike nchini, kutumia nafasi finyu waliyopewa katika
elimu ili kujikwamua. Sisi UKAWA tunaamini kuwa, kufanya kosa si kosa bali kosa
ni kurudia kosa. Tunawataka wazazi wote nchini kuwa walezi na marafiki nambari
moja wa watoto wao ili kujenga jamii yenye kuwajibika ili kuondokana na
umasikini na matusi ya viongozi wasio na uchungu na maisha yao.
Maendeleo
ya Watoto Nchini
Mheshimiwa
Spika, tafiti mbalimbali zilizofanyika zinazohusu watoto hapa nchini, zimeonesha
kuongezeka kwa idadi ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, wakati
watoto yatima wakifikia milioni 2.4. Katika tafiti hizo, zimeonesha kuwa,
tatizo la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi limeonekana Mijini na
Vijijini na zaidi kwenye Miji mikubwa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Tanga,
Moshi, Dodoma na Mbeya. Idadi ya watoto wanaoishi mitaani imeendelea kuongezeka
kutoka 1,579 mwaka 2007 hadi 2,010 mwaka 2011, wakati watoto 11,216 wanaoishi
katika Vituo vya Kulelea Watoto kati yao 6,089 ni wavulana na 5,127 ni
wasichana. Aidha, idadi ya Watoto Yatima waliopo nchi nzima wamefikia
2,400,000 kati ya hao Wasichana ni 1,055,000 na Wavulana ni 1,345,000, ambapo
idadi ya watoto 2,700 kati ya miaka 0-14 wanaoishi na Virusi vya Ukimwi nchini.[1]
Mheshimiwa
Spika, takwimu
hizo zinatoa viashiria na taswira pana juu ya watoto wanaoishi katika Mazingira
hatarishi hali ambayo inachangia kwa ongezeko la watoto mitaani pamoja na
kukithiri kwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto. Katika taarifa ya jumla ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali juu ya ufanisi kwa mwaka 2014, inaonesha
kua mfumo wa udhibiti takwimu na taarifa za watoto wanaoishi katika mazingira
hatarishi ni dhaifu na haukidhi matakwa ya watoto wanaoishi katika mazingira
hatarishi[2]
Ongezeko
la Watoto wa Mitaani na Athari zake katika Taifa
Mheshimiwa
Spika, wakati
piramidi ya Idadi ya Watu nchini Tanzania inaonesha kuwa idadi kubwa ya watu nchini
Tanzania ni watoto wenye umri wa chini ya miaka 15 na vijana. Asilimia 44 ya
watu wote hapa nchini ni watoto wenye umri chini ya miaka 15, ambapo ongezeko
la watoto wa mtaani limeendelea kuwa na athari huku sababu mbalimbali
kama umasikini katika familia, mifarakano na ukosefu wa amani kwenye familia na
Wazazi kutowajibika katika malezi na makuzi ya watoto wao vikipelekea watoto
hao kuishi katika mazingira hatarishi. Sababu nyingine ni vitendo vya ukatili,
udhalilishaji na unyanyasaji wa watoto kutoka kwa familia na jamii kwa ujumla,
nyingine ni kufariki kwa wazazi hasa kutokana na magonjwa mbalimbali, pia
huchangiwa na ndoa za umri mdogo pamoja na mimba zisizotarajiwa.
Mheshimiwa
Spika, Kambi ya
Upinzani Bungeni imenuia kujenga mfumo
wa utambuzi wa miji inayoongoza kwa watoto wa mitaani na kuwaweka watoto hawa
wa mitaani chini ya uangalizi wa walezi watakaokuwa wakiwezeshwa na Serikali (Foster Parents) ili kupunguza
idadi ya watoto wa mitaani. Aidha, Kambi ya Upinzani imejiandaa kuhakikisha
kuwa vituo vya kulelea watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi hasa yatima,
wanaweka mfumo wa kumbukumbu na taarifa kamili ili kufuatilia maendeleo yao
popote walipo nchini Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ya watoto kwa
kuwa vituo vingi vimeendeshwa bila kuwanufaisha watoto hasa wanaoishi katika
vituo hivyo na kwenye mazingira hatarishi.
Mheshimiwa
Spika, katika
hali ya masikitiko napenda kuzungumzia hali ya maendeleo ya watoto wenye
ulemavu mbalimbali hapa nchini. Pamoja na kuwa Wizara imepewa dhamana ya
kuhakikisha maendeleo ya watoto wenye ulemavu ni endelevu, bado mikakati ya
Serikali imeendelea kuweka kundi hili la watoto katika hatari kubwa. Kundi hili
la watoto wenye uhitaji maalumu kama walemavu wa viungo, macho, usikivu na
ngozi hajawekewa uzito wa kutosha na hivyo kuwafanya wanyonge na washindwe
kuendelea kwa kasi ile ile kama watoto wengine.
Mheshimiwa
Spika, wakati wa
mawasilisho ya hotuba ya Bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Barwany
ambaye ni waziri kivuli wa maendeleo ya jamii, jinsia na watoto lakini akiwa ni
mlemavu wa ngozi alionesha wasiwasi wake juu ya dhamira ya Serikali katika kuwalinda
watu wenye ulemavu wa ngozi. Waziri wa Sera, Uratibu na Bunge Mheshimiwa
Jestina Mhagama alisimama na kutoa maelezo kuwa Serikali imeandaa utaratibu wa
kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi kwa kuwaandalia tracking devices system
(mfumo wa kutambua mienendo ya mlengwa) ambayo inafanywa kwa kushirikiana na
wadau mbalimbali wa watu wenye ulemavu wa ngozi na masuala ya usalama. Mhe.
Barwany hakuridhishwa na kauli ile kwa kuwa yeye pia ni mmoja wa watu wanaoishi
kwa wasiwasi kwenye taifa hili.
Mheshimiwa
Spika, zikiwa
zimepita siku mbili toka Mhe. Barwany kuonesha wasiwasi wake juu ya mfumo wa
ulinzi kwa watu wenye ulemavu wa ngozi nchini Mwanamama Remi Luchoma alikatwa
mkono na watu wasiojulikana mkoani Katavi. Hii ni aibu kubwa kwa Serikali na ni
dhahiri kuwa imeshindwa kuwalinda watu wenye ulemavu kwa kuwa kwa masikitiko na
uchungu mkubwa, miezi mitatu (3) iliyopita mwili wa mtoto Yohana Bahati aliyekuwa na umri wa mwaka mmoja ambaye
alikuwa ni mlemavu wa ngozi maarufu kama Albino, ambaye alitekwa siku ya
Jumapili Februari 15, 2015 ulipatikana akiwa ameuawa katika eneo la Shilabela
Mapinduzi kilomita kadhaa kutoka nyumbani kwao kijiji cha Ilelema.
Mheshimiwa
Spika, nayazungumza
haya leo kwa kuwa tunapozungumzia maendeleo ya jamii, jinsia na watoto, huwezi
kuepuka kuzungumzia wanawake na watoto ambao wana ulemavu na hasa
uliosababishwa na vitendo vya Kikatili. Huwezi kuacha kuzungumzia matukio ya
kikatili na ya kutisha yanayoelekezwa kwa kundi hili muhimu katika jamii. Natoa maelezo haya nikiwa na masikitiko makubwa na
huzuni nyingi na huku nikiwa natafakari hatma ya watu wenye ulemavu nchini
kwetu wenyewe. Je, waikimbie Tanzania? Je ni nani atamfunga paka kengele? Ni
nani atawasaka na kuwazuia watekaji, watesaji na wauaji wa watu wenye ulemavu
hasa wa ngozi? Napinga kwa nguvu zangu zote na kuendelea kusikitishwa na
vitendo vya kikatili vinavyoendelea dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Mheshimiwa
Spika, pamoja
na Waziri Jenista Mhagama kueleza kuwa jambo la ulinzi wa watu wenye ulemavu wa
ngozi haliwezi kuzungumzwa hadharani kwa kuwa Serikali ipo katika Mkakati, je
leo hii anaweza kujibu ni idadi ya watu wangapi wenye ulemavu wa ngozi wauwawe
ili mfumo huo uanze kufanya kazi? Anawaambia nini watu wenye ulemavu kuhusu
kitendo cha kikatili cha ukataji wa kiungo cha mwanamke mwenzake kilichotokea
siku mbili tu baada ya yeye kama waziri mwanamke kuhakikisha kuwa Serikali
inawalinda watu wenye ulemavu wa ngozi?
Aidha, napenda kuchukua fursa hii kuiomba jamii
kubadilika na kuachana na imani potofu ambazo zinahatarisha maisha na usalama
wa watu wengine na ambazo zinarudisha nyuma jitihada zinazofanywa za kupiga
vita ukatili kwa watu wenye ulemavu wa ngozi, wanawake na watoto. Hali
kadhalika, tunawataka wananchi wote, kuwafichua wale wote wanaojishughulisha na
vitendo hivyo na kutoa taarifa kwa vyombo vya dola na mamlaka sahihi ili hatua
zaidi ziweze kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria.
Aidha, nitoe wito kwa watanzania wote kutowabagua
watu wenye ulemavu wa ngozi na kuchukua jukumu la kwanza la kuwa walinzi wa
haki ya walemavu wa ngozi kuishi kwa kuwa Serikali ya CCM imeshindwa kuwazuia
wauaji na watesi wa watu wenye ulemavu.
Mashirika
Yasiyo ya Kiserikali
Mheshimiwa
Spika, Serikali
ya CCM imeendelea kuuma na kupuliza kuhusu usimamizi wa mashirika yasiyo ya
Kiserikali. Ni Serikali hii ambayo kwa miaka kadhaa imekua ikiyapa usajili
mashirika yasiyo ya Kiserikali lakini Serikali hiyohiyo ikashindwa kuyafuatilia
utendaji wake kama inavyotakiwa kwa mujibu wa Sheria. Ni kweli kuwa kuna baadhi
ya mashirika yasiyo ya Kiserikali ambayo yamelenga kutumia mwanya uliopo
kufanya kazi kinyume na utaratibu ulioekwa lakini ni ukweli usiopingika kuwa
mashirika ambayo yamegeuka kuwa mwiba kwa Serikali hasa kwa kufichua uozo na
uovu wa Serikali hii ndiyo yamekuwa walengwa wa mkakati wa Serikali wa kuyafuta
kwa kuwa yanafanya kazi bila kufuata mashinikizo ya CCM.
Mheshimiwa
Spika,
tunaendelea kuamini kuwa Serikali inatekeleza mpango wa kuyafutia mashirika
yasiyo ya Kiserikali hasa kutokana na hofu ya kazi inayofanywa na mashirika
hayo kutoa elimu kwa umma na hasa tunapoelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba. Ni
jambo la kushangaza kuwa Serikali inaeleza changamoto mojawapo za mashirika yasiyo
ya Kiserikali ni kujikita mijini na sio vijijini kwenye wananchi wengi wenye
huhitaji, ikiwa nayo inashindwa kutekeleza wajibu na majukumu yake ya
kuhakikisha maendeleo ya jamii yananufaisha vijiji na si miji peke yake
inawezaje kuyafuta mashirika haya? Ni nini kinachoifanya Serikali ya CCM ifute
mashirika kwa kushindwa kujikita vijijini na nini kitaizua UKAWA kuifuta CCM
ambayo imeshindwa kutimiza wajibu wake kwa watanzania? Tunapenda kuikumbusha
CCM kuwa, ‘mwenzako akinyolewa upara, nawe tia maji kichwa chako’.
Aidha, ni jambo la kushangaza kuona kuwa taarifa ya
Wizara ya utekelezaji unaelezea changamoto kuwa mashirika haya yanategemea
ufadhili wa wa nje katika kutimiza majukumu yao, Je, si Serikali hii hii ya CCM
ambayo inategemea fedha za nje kuendesha miradi ya maendeleo nchini? CCM
imechoka na hii ndio lala salama yao. Amkani si shwari ‘No Longer at Ease’!
HITIMISHO
Mheshimiwa
Spika, ni katika
kadhia hizi ndipo tunaamini kuwa, kwa kuwa ushauri wetu kwa miaka mingi
umepuuzwa; Serikali ya CCM ijiandae kuachia ngazi ifikapo Oktoba 2015 kwa kuwa
Serikali itakayoongozwa na vyama vinavyoundwa UKAWA imepanga na inatarajia
kurudisha maendeleo ya jamii katika ngazi ambayo Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere,
alitarajia kutufikisha watanzania. Nimalizie kwa kunukuu maneno ya Baba wa
Taifa aliyowahi kusema
‘Uhuru na Maendeleo ni vitu vinavyohusiana sana; uhusiano wao ni sawa na
uhusiano baina ya kuku na yai! Bila ya kuku hupati mayai; na bila mayai kuku
watakwisha. Vile vile, bila ya uhuru hupati maendeleo, na bila ya maendeleo ni
dhahiri kwamba uhuru wako utapotea’
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni, naomba kuwasilisha.
.....................................................
Khalfan Barwany Salum (MB)
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI WA MAENDELEO YA
JAMII, JINSIA NA WATOTO.
25 MEI 2015.
No comments:
Post a Comment